MTANGAZAJI

UONGOZI WA WAADVENTISTA TEXAS WAOMBA MAOMBI KWA AJILI YA MCHUNGAJI ALIYEKAMATWA

 

 
Uongozi wa Konferensi ya Texas ya Kanisa la Waadventista wa Sabato umetoa wito kwa waumini kuungana kumwombea Mchungaji Luis Morales na familia yake, baada ya mchungaji huyo mwenye asili ya Venezuela anayehudumu katika eneo la Houston kukamatwa  na maafisa wa uhamiaji wa Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa George W. Bush juma lililopita wakati akisafiri na mke wake katika safari binafsi.
 
Taarifa ya Konferensi hiyo iliyochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook Agosti 12,  inaeleza kuthibitisha kukamatwa kwa mmoja wa wachungaji wake, Luis Morales, katika uwanja wa Ndege wa George W. Bush mnamo Agosti 7, 2026.
Kwa sasa, taarifa kamili kuhusu sababu za kukamatwa kwake hazijafahamika, na uongozi wa Konferensi ya Texas umesema unaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu.
 
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Mchungaji Morales amehudumu katika Konferensi ya Texas tangu Januari 2023, akisimamia makanisa manne katika eneo la Houston na kuwa ana kibali halali cha kufanya kazi nchini Marekani na kwamba amekuwa mtumishi mwaminifu katika utume wa kanisa na jamii anazohudumia.
 
Uongozi wa Konferensi ya Texas uko katika mawasiliano ya karibu na familia ya Mchungaji Morales pamoja na viongozi wa makanisa husika, huku ukisisitiza umuhimu wa kuheshimu faragha ya familia wakati huu mgumu.
 
Kituo cha habari cha Telemundo Houston na mwandishi wa habari Lidia Terrazas waliripoti kuwa Luis Morales alikamatwa Agosti 6, 2026, ambapo baadaye alipelekwa katika kituo cha kizuizi cha uhamiaji kilichopo Livingston, Texas umbali wa maili 59 kutoka uwanja wa ndege wa George W.Bush.
 
Kwa mujibu wa Terrazas, Mchungaji Morales amekuwa akiishi Marekani kwa miaka kadhaa tangu alipoingia kwa visa na baadaye kuomba hifadhi ya kisiasa. Familia yake inasema kuwa kesi yake ya hifadhi bado inaendelea na kwamba ana kibali cha kazi, kitambulisho cha ukaazi halali, na nyaraka nyingine za uhamiaji. 
 
Waumini wa makanisa anayoyaongoza Morales pia wamejitokeza kuiunga mkono familia yake. Katika kipande cha video alichokiweka kwenye mtandao wa Instagram Terrazas, kinaonesha ujumbe wa maombi na faraja pamoja na Biblia uliowekwa na waumini nyumbani kwa Morales ili mke wake aweze kumfikishia wakati wa mawasiliano ya simu kutoka kizuizini.
 
 “Mchungaji mpendwa, tunakupenda. Tunaomba kwa ajili yako,” ulisomeka mmoja wa ujumbe huo.
 
 Telemundo iliripoti kuwa Morales amekuwa na uwezo wa kuwasiliana kwa simu akiwa kizuizini. Tovuti ya kanisa lake inamtaja kuwa ni mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato la Kihispania la Deer Park huko Pasadena, Texas, na ukurasa wake wa Facebook unaeleza kuwa yeye ni mchungaji wa Konferensi ya Texas, mume na baba wa mabinti wawili.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.