MAPENZI BILA MIPAKA : FAIDA NA HASARA ZAKE.
Katika ulimwengu wa sasa ambao umekuwa kama kijiji kimoja, mahusiano ya kimataifa yamekuwa jambo la kawaida. Moja ya mahusiano yanayozidi kushamiri ni ndoa kati ya Waafrika na Wazungu kutoka Marekani. Ni jambo la kawaida katika zama hizi kusikia mtu anasema mimi nataka kuoa ama kuolewa na mzungu. Ingawa upendo ni lugha ya ulimwengu wote, muunganiko huu unakuja na mambo ya kipekee ya kuzingatia
Ndoa kati ya Mwafrika na Mzungu wa Marekani ni muunganiko unaoakisi mabadiliko makubwa ya kijamii duniani, ambapo takwimu za hivi karibuni nchini Marekani zinaonyesha ongezeko kubwa la ndoa za mbari tofauti. Kwa mfano, ripoti za kituo cha utafiti cha Pew zinaashiria kuwa takriban 18% ya watu weusi waliofunga ndoa hivi karibuni nchini Marekani wameoana na watu wa mbari tofauti, ikiwa ni ongezeko kutoka 5% mwaka 1980.
Uzuri wa hali hii unajikita katika mabadilishano ya elimu ya maisha ambapo Mwafrika anapata fursa ya kufurahia mifumo ya kimaendeleo ya Marekani kama vile huduma bora za afya na soko la ajira (japo si wazungu wote wa Marekani wanamafanikio kiuchumi) huku mwenzi wa Kimarekani akijifunza tunu za kijamii za Kiafrika kama mshikamano na ukarimu.
Faida hizi huenea hadi kwa kizazi kijacho, ambapo watoto wanaozaliwa katika mazingira haya hupata urithi pacha unaowajengea uwezo wa kipekee wa lugha na ujasiri wa kijamii. Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wanaokua katika familia zenye mchanganyiko wa tamaduni hupata alama nzuri za kimasomo na uwezo mkubwa wa kutatua matatizo kutokana na kuishi katika mazingira yanayohimiza fikra pana. Ikiwa wazazi wao waliwapa msingi mzuri wa malezi na elimu.
Zaidi ya hayo, ndoa hizi huimarisha uhusiano wa kimataifa; Mwafrika nchini Marekani aliye na vibali na mwenye mipango mizuri mara nyingi hupata fursa ya elimu, utulivu wa kifedha unaomwezesha kusaidia miradi ya maendeleo nyumbani, jambo ambalo huchangia katika ukuaji wa uchumi wa familia yake ya asili Afrika.
Hata hivyo, undani wa changamoto za uhusiano huu unajidhihirisha pale misingi miwili tofauti ya malezi inapokutana, hasa katika mgongano kati ya mfumo wa kijamii wa Kiafrika (collectivism) na ule wa Marekani unaosisitiza uhuru wa mtu binafsi (individualism).
Moja ya vikwazo vikubwa ni usimamizi wa matarajio ya kifamilia, ambapo Mwafrika anaweza kuona ni wajibu kusaidia ndugu, jambo ambalo mwenzi wa Marekani anaweza kulichukulia kama mzigo.
Takwimu zinaonyesha kuwa ndoa za mbari tofauti zinaweza kukabiliwa na hatari ya kuvunjika kwa 41% ndani ya miaka 10 ya kwanza ikilinganishwa na 31% kwa ndoa za mbari moja, hali inayochangiwa na misongo ya kijamii na tofauti za kimsingi za kimtazamo.
Ubaya mwingine unahusisha changamoto za ubaguzi wa kimfumo na kisaikolojia, ambapo mwenzi Mwafrika anaweza kupambana na changamoto za rangi nchini Marekani ambazo mwenzi wake Mzungu hajawahi kuzipitia wala kuzielewa kikamilifu. Hali hii inaweza kuleta msongo wa mawazo na hata kuathiri afya ya kiakili na kimwili ya wanandoa ikiwa hakutakuwa na mfumo thabiti wa kusaidiana.
Mwafrika anayehamia Marekani, miaka ya kwanza inaweza kuwa ya upweke
sana kutokana na kukosa marafiki na msaada wa karibu. Aidha, mchakato wa
kupata vibali vya ukaazi halali ama uraia unaweza kuwa wa muda mrefu (si chini ya miaka 10) na wenye msongo
mkubwa wa mawazo.
Uhusiano huu unahitaji mawasiliano ya kina na uelewa wa hali ya juu ili kuvuka vihunzi vya ubaguzi, urasimu wa kisheria wa uhamiaji, na upweke anaoupata Mwafrika anapojaribu kuzoea maisha mapya ugenini bila msaada wa karibu wa ndugu wa asili.

.png)
Post a Comment