KIONGOZI MSTAAFU WA WAADVENTISTA AKABIDHIWA JEZI YA MESSI
Kijana mdogo Osvaldo Rigacci alisimama mbele ya darasa la shule ya sekondari nchini Argentina akiwajibika badala ya mwalimu ambaye hakuwepo siku hiyo, bila kujua kuwa siku hiyo ingekuwa mwanzo wa safari yake ya kiroho na uongozi wa kipekee.
Wanafunzi walimuuliza maswali mazito kuhusu maisha na imani, na alijibu kwa kutumia Biblia aliyofundishwa na wazazi wake utotoni. Lakini swali moja kutoka kwa vijana aliowafahamu kwa miaka kadhaa lilimgusa sana, ikiwa kweli anaamini kile anachofundisha, kwa nini hakuishi kama muumini? Swali hilo lilimrudisha kwenye misingi aliyokuwa ameanza kuipoteza baada ya kifo cha baba yake miaka mitano kabla ya hapo, na likawa chanzo cha safari ambayo hatimaye ingemfanya kuwa kiongozi anayeheshimika sana katika Kanisa la Waadventista wa Sabato.
Baada ya takribani miaka 44 ya utumishi wa kanisa, Rigacci aliyekuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato upande wa Huduma za tamaduni mbalimbali wa Unioni Konferensi ya Kusini Magharibi mwa Marekani katika kanisa hilo (SWUC) tangu mwaka 2021 amestaafu rasmi kwenye Mkutano wa 32 wa uchaguzi Aprili 26, mwaka huu.
Katika huduma yake yote, amejipambanua kwa kujitoa katika uanzishaji wa makanisa mapya katika kila makanisa ya Konferensi ya Texas aliyohudumu kwa takibani miaka 40, mchango wake mkubwa katika kuandaa programu ya masomo ya Biblia kwa watoto iitwayo Mi Conexión Bíblica, na moyo wake wa kipekee wa kulea viongozi wapya kwa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwawezesha kukua katika huduma.
Katika hafla ya kumpongeza, alikabidhiwa jezi ya mchezaji wa mpira wa miguu wa Argentina, Lionel Messi iliyosainiwa, ikiwa ni ishara ya heshima kwa asili yake ya Argentina na shukrani kubwa kwa uongozi wake wa muda mrefu. Messi, akiwa alama ya ubora, nidhamu na uongozi, alionekana kuakisi sifa ambazo pia zimeonekana wazi katika maisha ya huduma ya Rigacci.
Zawadi ya jezi hiyo inawakilisha mambo matatu, kwanza, ni Mhargentina, na Messi ni alama kubwa ya taifa hilo, hivyo jezi hiyo ni ishara ya kumheshimu kwa namna ya kibinafsi na ya kihisia. Pili,ni zawadi ya shukrani kwa uongozi wake wa miaka 44, hasa katika uanzishaji wa makanisa mapya, huduma kwa tamaduni mbalimbali, na kulea viongozi wapya ndani ya kanisa. Tatu, Messi anawakilisha ubora, nidhamu na uongozi wa utulivu, sifa zinazofanana na jinsi Rigacci alivyojulikana katika huduma yake.
Rigacci na mkewe Monica, ambao wameishi pamoja kwa miaka 44, wana watoto wawili watu wazima Fernando na Aniella pamoja na wajukuu sita, zikiwemo seti mbili za mapacha watatu. Katika maisha yake ya kustaafu, anapanga kuendelea kuhubiri, kueneza injili, kutafsiri na kuandika vitabu na machapisho mbalimbali , ikiwemo kukamilisha kitabu cha kilichoongozwa na mjomba wake aliyefariki.
Katika hotuba yake ya kuaga, alisema “Bado mimi ni mwanafunzi ninayeendelea kukua. Kuwa mwaminifu, kuwa thabiti, na usikate tamaa.” Safari yake, kutoka kijana aliyesimama mbele ya darasa nchini Argentina hadi kuwa kiongozi wa juu anayeheshimika wa Unioni Konferensi ya Kusini Magharibi mwa Marekani ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (SWUC) ni ushuhuda wa nguvu ya wito, uaminifu na kujitoa kwa Mungu.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka Juni 30, 2025, SWUC yenye waumini wapatao 129,876 kutoka katika makanisa 602 katika eneo lenye wakazi 44,595,013 ijumuisha Konferensi tano ambazo ni Arkansas–Louisiana, Oklahoma, Kusini Magharibi, Texas na Texico.



Post a Comment