MTANGAZAJI

RAIS WA ZAMBIA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAFANYABISHARA WAADVENTISTA WA UGANDA.

 



 Jumuiya ya Wafanyabiashara Waadventista wa Uganda (UABC), chini ya mwamvuli wa klabu ya Celestial Billionaires, imekutana na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema katika Ikulu ya Lusaka kujadili masuala ya biashara ya pande mbili na manufaa ya pamoja kati ya nchi hizo ikiwemo ushirikiano wa kibiashara na fursa za uwekezaji.
 
Ujumbe huo wa watu kumi na saba uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa National Resistance Movement (NRM) Namayanja Rose Nsereko, Dkt. Benon Luggya wa Maganjo Group of Companies, James Kayita wa Hallmark Construction, na Godfrey Babi Kimera wa City Sites Group.
 
UABC imekuwa ni moja ya majukwaa muhimu yanayowaunganisha wafanyabiashara, wataalamu, na wawekezaji Waadventista nchini Uganda. Ingawa ni jukwaa changa, safari yake imejaa hatua za kimkakati, ushirikiano wa kikanda, na dhamira ya kuinua uchumi wa waumini kupitia maadili ya kikristo na ubunifu wa kibiashara nchini humo na nje ya nchi.
 
Katika ziara hii, Celestial Billionaires walikutana pia na Waziri anayehusika na Biashara nchini Zambia pamoja na washirika mbalimbali wa kibiashara waliopo nchini humo. Rais wa Zambia Hakaide Hichilema ni miongoni mwa waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato nchini humo.
 
 Jukwaa hilo linaloelezwa kuanzishwa  kati ya mwaka 2022 na 2023 historia yake inajengwa zaidi kupitia shughuli, mikutano, na ushirikiano wa wafanyabiashara Waadventista nchini Uganda likiendelea kujijenga kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wafanyabiashara hao, kukuza ubunifu, na kuhamasisha uwekezaji wenye maadili barani Afrika.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.