MTANGAZAJI

MCHUNGAJI AKIRI KUMTEKA BINTI WA MIAKA 13

 


Mchungaji mmoja wa Ohio, Marekani  ambaye alipewa likizo ya kiutawala na uongozi wa kanisa  baada ya kukamatwa mwaka jana amekiri kosa katika kesi ya jinai inayomhusisha msichana wa miaka 13.

Jesse Santos, mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato la Canton, aliwasilisha maombi ya kukiri kosa juma hili kwa shitaka la utekaji nyara, kwa mujibu wa kituo cha habari cha eneo hilo cha  WOIO. 

Santos alikamatwa  Februari 2025 baada ya wachunguzi kumhusisha na tuhuma zinazomhusu msichana huyo mdogo. Awali alishtakiwa kwa utekaji nyara, mashtaka mawili ya kufanya vitendo vya ngono kinyume cha sheria, na kuhatarisha usalama wa watoto. Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo lilitokea mwezi Septemba 2025 katika eneo la kambi lililopo kwenye kipande cha barabara cha namba 3000 cha Ashland County Road, katika Kambi ya River Run huko Loudonville.

Vyombo vya habari  viliripoti awali mwezi Februari 2025 kwamba Santos, ambaye wakati huo alikuwa mchungaji wa mtaa anayesimamia makanisa kadhaa ya Waadventista wa Sabato huko Ohio, alishtakiwa baada ya mamlaka kudai kuwa alimchukua mwanafamilia wa karibu mwenye umri wa miaka 13 kwenye safari ya kambi na kufanya jaribio la kuanzisha mahusiano ya kingono, huku ushahidi wa vinasaba (DNA) ukiunga mkono maelezo ya mhanga. 

Baada ya kukamatwa kwake, Konferensi ya Ohio ya Kanisa la Waadventista wa Sabato ilimweka  Santos likizo ya kiutawala na kusema itashirikiana kikamilifu na vyombo vya sheria. Anatarajiwa kuhukumiwa mwezi Machi na jaji wa Kaunti ya Ashland. 

Mamlaka nchini Marekani zinaeleza kuwa tukio la mtu mzima kufanya au kujaribu kufanya vitendo vya kingono dhidi ya mtoto ni kosa kubwa la jinai. Kisheria, mtoto hawezi kutoa ridhaa ya kushiriki katika masuala ya kingono, hivyo hata jaribio la kutoa maneno, ishara au mguso wa kingono huhesabika kuwa kosa.

 Endapo mtu mzima atamchukua au kumsafirisha mtoto bila idhini ya mzazi au mlezi, kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa kama utekaji, hata kama wahusika wana uhusiano wa kifamilia. 

Sheria za Marekani pia hutambua ushahidi wa kisayansi ikiwemo wa vinasaba (DNA) katika kuthibitisha kesi kama hizi, huku adhabu kwa wanaopatikana na hatia zikiwa kali, zikiwemo kifungo cha gerezani, kusajiliwa kama wahalifu wa kingono, na kupoteza haki na nafasi za kazi. Lengo kuu la sheria hizo ni kulinda watoto na kuhakikisha haki inatendeka bila upendeleo wowote.

 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.