WASOMAJI WA BIBLIA WAONGEZEKA MAREKANI
Baada ya miaka minne ya kupungua kwa kasi ya usomaji wa Biblia nchini Marekani, mwaka 2025 umeleta mwanga mpya,takribani Wamarekani milioni 11 zaidi wanasoma Biblia mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2024, kwa mujibu wa ripoti ya State of the Bible 2025 iliyotolewa na Chama cha Biblia cha Amerika (ABS).
Kikubwa kilichowashangaza watafiti ni kwamba ongezeko hilo linaongozwa na vijana wa kiume, hasa kutoka makundi ya millennials na Gen Z ambayo hapo awali yalionekana kutoshiriki sana na Maandiko.
Dkt. John Plake, Afisa Mkuu wa Ubunifu wa ABS, amesema kuwa hawawezi bado kusema kuwa ni mwelekeo rasmi, lakini ni dalili ya mabadiliko chanya. Aliyasema hayo katika kongamano la Evangelical Press Association lililofanyika Branson, Missouri.
Ripoti hiyo, ambayo ni ya mwaka wa 15 sasa, hufuatilia mwenendo wa uhusiano wa Wamarekani na Maandiko, ibada, na imani. Takwimu za mwaka huu, zilizokusanywa Januari 2025, zinaonyesha kuwa baada ya kushuka mfululizo kutoka asilimia 50 mwaka 2021 hadi asilimia 38 mwaka 2024, mwaka huu kiwango kimepanda hadi asilimia 41—ongezeko la asilimia 3.
Katika eneo la Bay Area, asilimia 40 ya millennials walihesabika kuwa ni “watumiaji wa Biblia” (yaani wale wanaosoma Maandiko angalau mara tatu hadi nne kwa mwaka nje ya ibada), dhidi ya wastani wa kitaifa wa asilimia 39. Kwa upande wa Gen Z, Bay Area ilirekodi asilimia 37, dhidi ya asilimia 36 kitaifa.
Kando na usomaji wa Biblia, Wall Street Journal iliripoti mnamo Oktoba 2024 kwamba mauzo ya Biblia yaliongezeka kwa asilimia 22 ukilinganisha na mwaka uliopita. Sehemu kubwa ya wanunuzi walikuwa vijana waliokuwa wananunua Biblia kwa mara ya kwanza, jambo linalodokeza ongezeko la udadisi wa kiroho miongoni mwa kizazi kipya.
Dkt. Plake anaeleza kuwa kuna Wamarekani milioni 71 wanaoitwa “kundi la kati linaloweza kusogezwa”watu wanaopendezwa na Biblia lakini bado hawajaanza kusoma kikamilifu. Wanaonyesha kiu ya kiroho lakini wanahitaji msaada wa kuelewa Maandiko na maana yake kwa maisha yao.
Post a Comment