MTANGAZAJI

TATIZO LA AFYA YA AKILI KWA WANAUME WAHAMIAJI MAREKANI

 


Katika harakati za kutafuta maisha bora nchini Marekani, takwimu zinaonesha kuwa wanaume wengi kutoka Afrika wanakutana na changamoto kali za kiuchumi ambazo sasa zinathiri afya zao za akili kwa kiwango cha kikubwa. Wakiwa mbali na familia, katika mazingira mapya na yasiyo na msaada wa kijamii wa karibu, wanaume hawa wanalazimika kubeba mzigo mkubwa wa matarajio, mahitaji ya kifamilia, na ugumu wa maisha ya ughaibuni  kimya kimya.
Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Afya wa Jimbo la California (CHIS) kwa mwaka 2023 , ulionesha wanaume waafrika wahamiaji wanaoishi chini ya kiwango cha kipato cha $40,000 kwa mwaka wako kwenye hatari mara mbili zaidi ya kupata msongo wa mawazo ikilinganishwa na wale wenye kipato cha kati au juu. 
Hii ni kutokana na gharama kubwa ya maisha, ukosefu wa ajira za kudumu, majukumu ya kifamilia ya pande mbili (nyumbani Afrika na Marekani), na ukosefu wa usaidizi wa kiuchumi.
Katika ripoti ya Januari 2024, wanaume wengi walikiri kufanya kazi za muda mfupi zisizo na bima ya afya, mafao, wala usalama wa ajira. 
Wengine waliripoti kufanya kazi zaidi ya saa 60 kwa juma huku wakiishi katika mazingira magumu ya kupanga nyumba kwa pamoja ili kugharamia kodi inayozidi uwezo wao. Mmoja wa wahamiaji kutoka Afrika Magharibi anasema, “Kwa nje tunaonekana tumefanikiwa, lakini ndani tunaumia. Kodi ni kubwa, familia nyumbani wanahitaji msaada, na hapa hakuna wa kumtegemea.”
Asilimia 79 ya wanaume waliohojiwa walisema walishuhudia au walikumbwa na ubaguzi kazini hali inayowaweka kwenye nafasi ya kupokea ujira mdogo na nafasi chache za kupanda kazini. 
Kwa wale walio nchini Marekani kwa chini ya miaka mitano, asilimia 77 hawana bima ya afya  jambo linalowanyima fursa ya kupata msaada wa kitaalamu wa afya ya akili, licha ya kuwa katika hatari kubwa.
Matatizo ya kiuchumi yanazidi kuwa mzigo kwa afya ya akili. Mwanaume mmoja kutoka Kenya anasema, “Kila mwezi unawaza kodi, ada ya shule ya mtoto Afrika, chakula hapa, na bado unahisi hujatimiza wajibu wako. Mwishowe unajikuta ukikosa usingizi na kuwa mkali kwa kila mtu.”
Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini Marekani (CDC) za mwaka 2023 , watu weusi wenye kipato cha chini wanaripoti viwango vya juu zaidi vya unyogovu sugu na msongo wa mawazo kuliko wenzao wenye kipato cha juu. Hali hii ni mbaya zaidi kwa wanaume waafrika wahamiaji kutokana na ukosefu wa mitandao ya kijamii na msaada wa kifamilia.
  Matatizo ya kiuchumi si suala la takwimu tu  ni maumivu ya kimya yanayoathiri afya ya akili ya wanaume waafrika waliokwenda Marekani kwa matumaini makubwa. 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.