MTANGAZAJI

MKUTANO MKUU WA WAADVENTISTA KUFANYIKA JULAI MAREKANI

 


Kanisa la Waadventista wa Sabato linajiandaa kwa Mkutano Mkuu wa 62 wa Konferensi Kuu (GC) utakaofanyika kuanzia Julai 3 hadi 12, 2025, mjini St. Louis, Missouri, Marekani.
Mkutano huu mkubwa unatarajiwa kuwaleta pamoja wajumbe 2,804 walioteuliwa kutoka duniani kote kwa ajili ya kupiga kura na kujadili masuala muhimu ya kanisa, ikiwemo uchaguzi wa viongozi wakuu wa Kanisa, Divisheni 13 duniani na vitengo mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Zaidi ya waumini 100,000 wa kanisa hilo wanatarajiwa kufika katika mji wa St. Louis kushiriki ibada, maonyesho ya huduma mbalimbali, pamoja na kushuhudia vikao vya mkutano huo wa kihistoria.
Mkutano huu unatarajiwa kuendeshwa na kuwezeshwa kidijitali, ambapo maudhui yatapatikana kwa lugha saba, zikiwemo Kiswahili, Kiingereza, Kihispania na Kijerumani. Pia kutakuwepo na tafsiri ya lugha ya alama kwa wenye uhitaji maalum.
Kupitia mitandao ya kijamii, YouTube, Facebook na WhatsApp, programu tumishi maalum ya simu, waumini ambao hawataweza kufika St. Louis wataweza kufuatilia kila tukio moja kwa moja.
Mkutano Mkuu wa Konferensi Kuu, unaofanyika kila baada ya miaka mitano, si tu mkutano wa kiutawala bali pia ni tukio la kiroho linalowaleta pamoja Waadventista kutoka mataifa yote wakijifunza, kuabudu, na kupanga namna bora ya kufikisha injili ya milele ya kanisa hilo duniani kote.
Hadi Disemba 31, 2023, Kanisa la Waadventista wa Sabato lilikuwa na jumla ya waumini 22,785,195 ambapo waumini wapya 1,465,000 walijiunga na kanisa hilo mwaka huo, ikiwa ni ongezeko kubwa zaidi la uanachama katika historia ya kanisa. Likitoa  huduma katika nchi 212 kati ya 235 zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.