KONGAMANO LA CONNECT TO CONNECT (C2C) LAJA TANZANIA
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania imesaini mkataba wa makubaliano na kampuni ya Extensia Limited ya Uingereza, lengo likiwa ni kuandaa Kongamano litakalowakutanisha wadau wa sekta ya mawasiliano wa ndani na nje ya nchi linalojulikana kama Connect To Connect.
Kongamano hilo pia linalenga kuzidi kukuza matumizi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufungua wigo wa mifumo, ubunifu na uwekezaji katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema Kongamano la Connect To Connect (C2C) litafanyika kwa siku mbili Septemba 7 hadi 8 Septemba, 2022 ambapo nchi nyingi zinatarajiwa kushiriki ikiwa ni pamoja na nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki.
Amesema kuwa Tanzania inaunganisha nchi saba za jirani ambazo ni Kenya, Uganda,Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na Msumbiji kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo kuwa na fursa kubwa ya kupeleka huduma na kuchichimua uchumi kupitia TEKNOHAMA.
Dkt. Yonazi ameeleza kuwa Kongamano litatoa pia fursa kwa nchi zitakazoshiriki kufanya majadiliano, kujifunza na kuweka mikakati ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuchangia uchumi , kuongeza fursa za uwekezaji, ajira na elimu.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Extensia Limited, Bw. Tariq Malik amesema kuwa Kongamano hilo lilifanyika Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2023 hadi 2025 na kuleta mafanikio makubwa. Aidha, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano kwa mara nyingine ambapo itapaisha zaidi Tanzania kama kitovu cha mawasiliano.
Post a Comment