SERIKALI YA TANZANIA YASEMA HAITOVUMILIA VITENDO VYA UKEKETAJI
Serikali
ya Tanzania imeonya haitovumilia kuona vitendo vya ukatili hasa Ukeketaji
vinaendelea kufanywa katika jamii kwani vinasababisha madhara makubwa
kwa watoto wa kike na wanawake.
Hayo
yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akiwa wilayani Serengeti, mkoa wa
Mara alipotembelea kituo cha Hope for Girls and Women kuona shughuli
zinazofanywa na kituo hicho katika kupambana na ukeketaji.
Mpanju
ameongeza kuwa Wizara itashirikiana na Wizara za kisekta na wadau ili
kuhakikisha mapambano dhidi ya vitendo vya Ukeketaji yanaenda kwa kasi
zaidi kwa lengo la kutokomeza vitendo hivyo katika Mikoa mbalimbali.
Ameitaka jamii na wadau kuwalinda Watoto wa kike na wanawake dhidi ya
vitendo vya Ukeketaji na kusisitiza kuwa hakuna Jamii ambayo inaruhusu
kukatiza ndoto na maisha ya watoto wa kike kwa kuwafanyia vitendo vya
Ukeketaji.
"Tunaweza
kuishi katika jamii ambayo haina vitendo vya Ukeketaji katika maeneo
yenu tuwalinde Watoto wetu wa kike kwani ni Hazina na tegemeo kwa
maendeleo ya Taifa" alisema Mpanju
Pia
amewataka Viongozi wa Kimila kuachana na Mila zilizopita kwa wakati ili
kuwaokoa Watoto wa kike na vitendo vya Ukeketaji ambavyo vinasababisha
Watoto wengi kupoteza ndoto zao katika maisha.
Akitoa
taarifa ya Wilaya Afisa Maendeleo ya Jamii Wa Wilaya ya Serengeti
Sunday Wambura amesema Wilaya inashirikiana na wadau Wilayani humo
katika kutoa elimu kwa wananchi hasa mangariba na Wazee wa Kimila ili
waweze kuachana na vitendo hivyo ambavyo vinasababisha hofu, vifo na
matatizo ya kisaikolojia kwa watoto wa kike na wanawake.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Hope for Girls and Women Robi
Samwel amesema Kituo hicho kimelenga kimewasaidia Watoto wanaokimbia
kukeketwa kwa kuwapa hifadhi na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuachana
na vitendo vya ukatili hasa vitendo vya Ukeketaji kwa kuwawezesha
mangariba walioacha kukeketwa kupata fursa za kujikwamua kiuchumi na
kuachana na vitendo hivyo.
"Pia
tunawaendeleza wahanga wa Ukeketaji na waliokimbia vitendo hivyo kwa
kuwawezesha kupata ujuzi katika fani mbalimbali ili waweze kujitegemea
katika kuendesha maisha yao na wengi wamefika katika hatua za juu
akiwemo mmoja aliyepo Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam" alisema Robi.
Post a Comment