MAKAZI YA WAZEE TANGA KUKARABATIWA
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeazimia kukarabati makazi ya wazee ya Muheza mkoani
Tanga hivi
karibuni ili kuimarisha mazingira ya kuishi kwa wazee wanaolelewa katika
makazi hayo.
Akizungumza
na wazee hao alipotembelea makazi hayo Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema
wazee wana haki ya kupata huduma bora kwa ustawi wa afya zao.
Dkt.
Chaula amewahakikishia wazee hao 20 wanaoishi kwenye makazi hayo kuwa
muda si mrefu shughuli ya kukarabati majengo na miundombinu ya umeme,
maji na barabara itaanza.
Ameongeza
kuwa, Serikali haijawaacha wazee kwa kuhakikisha wanaishi vizuri katika
makazi yote 14 yaliyopo nchini hivyo ziara yake ina lengo la kuona
namna ya kuboresha makazi hayo ili yafanane na ustawi wa nchi.
"Tumekuja
kuangalia ni namna gani tutaboresha makazi haya yafanane na nyumba
nzuri tunazopenda kuishi, kwa hiyo Serikali imetupa jukumu la
kuhakikisha ustawi wenu unaimarika" amesema Dkt. Chaula.
Awali,
Afisa mfawidhi wa makazi hayo Mwamvita Kilima amebainisha kuwa,
changamoto za makazi hayo ni maji, umeme, uzio na uchakavu wa majengo.
Hata hivyo Mwamvita amesema, anapata ushirikiano mzuri wa Halmashauri katika kuwatunza wazee hao hususani huduma za afya.
"Namshukuru
Mkurugenzi wa Halmshauri na timu yake, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa
Uviko wazee wote walipatiwa elimu na wote wamechanja ameongeza Mwamvita.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Issa
Misumari aliyekuwepo kwenye Ziara hiyo, aliwahakikishia wazee hao kuwa,
Halmashauri itaendelea kuwaangalia na kutoa ushirikiano kwa kuwawekea
mazingira bora zaidi.
Akizungumza
kwa niaba ya wazee wenzake Mzee Joseph Misigaro ameishukuru Serikali
hususani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kuwajali wazee.
Post a Comment