MTANGAZAJI

COSOTA WAKEMEA TAARIFA ZA UPOTOSHAJI

 
 



Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imejibu hoja zilizotolewa na taasisi ya
Creative Industry Network Tanzania (CNIT) kwa kushirikiana na Twaweza na kusisitiza suala la ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha siyo la uanaharakati  ni suala la kisheria.

Kauli hiyo imetolewa Februari 22, 2022 na Afisa  Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Tanzania Doreen Anthony Sinare katika mkutano wake na waandishi wa habari.
 
Afisa huyo ameeleza  kuwa Kanuni ya usajili wa wanachama na kazi zao inataka wabunifu wa Hakimiliki, Asasi na Makundi yanayojihusisha Hakimiliki kujisajili COSOTA ili waweze kutambuliwa , hivyo taasisi ya CNIT wala Mkurugenzi Mtendaji wake Robert Mwampembwa pamoja na Twaweza hazitambuliki na COSOTA.
 
"Kwa mdau yoyote aliyekuwa na maswali, hoja au maoni kuhusu mgao wa mirabaha uliyofanyika hivi karibuni anakaribishwa  ofisini kuuliza na siyo kuanza kufanya upotoshaji kwa kuandika au kuzungumza vitu visivyo vya kweli COSOTA inakemea vikali tabia hii"alisema Doreen. 

Pamoja na hayo Bi. Doreen alifafanua kuwa COSOTA haijakusanya mirabaha kutoka katika Redio Saba tu kama ilivyoelekezwa bali imekusanya kutoka vyanzo mbalimbali kama Baa, Hoteli, Kumbi za Sherehe, Kumbi za Starehe na vyombo vya habari kama Kebo, Redio na Televisheni.

Hivyo COSOTA inatoa wito kwa wabunifu wote kuendelea kusajili kazi zao kwa ajili ya kuziwekea ulinzi, na inasisitiza kuwa mgao wa mirabaha unatokana na matumizi ya kazi kibiashara na siyo kwamba unaposajili tu kazi yako unakuwa unastahili kulipwa mrabaha.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.