MTANGAZAJI

DKT. CHAULA AWATAKA WAMACHINGA KUTUMIA TEKNOLOJIA

 

 
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Dkt. Zainab Chaula amewataka Wamachinga kutumia fursa zilizopo nchini humo  ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shughuli zao ili kupiga hatua kiuchumi.
 
Akifungua kikao cha kuwajengea uwezo Viongozi wa shirikisho la Wamachinga, kilichofanyika Jijini Dodoma Februari 22, 2022 Dkt. Chaula amesema kwa sasa Teknolojia inakuwa kwa kasi hivyo uwezekano wa kupata masoko na bidhaa umerahisishwa ikilinganishwa na kipindi cha Nyuma ambapo Teknolojia ilikuwa duni.
 
Dkt. Chaula amesema, fursa nyingine zilizopo ni pamoja na amani na utulivu uliopo nchini, mikopo ya Maendeleo kutokana na mapato ya Halmashauri, pamoja na ardhi.
 
 Amewataka pia, kuimarisha ushirikiano miongoni mwao, Serikali na Wadau wengine ili kukuza zaidi mitandao ya biashara zao na kuboresha maisha kwani wao wenyewe ni fursa katika kukuza uchumi wa Taifa. Pia wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote ili kuwatenganisha.
 
Dkt. Chaula amebainisha kuwa Serikali nchini humo imetoa jumla ya sh. bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Wamachinga hivyo Serikali itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa ufanisi.
 
Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akitoa maelezo kuhusu kikao hicho amesema hadi tarehe 31 Januari usajili wa shirikisho la machinga ulikuwa umekamilika.
 
Mpanju amesema lengo la kikao hicho ni kuwasikiliza na kuwapa fursa ya kupata elimu ya masuala mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.
 
"Nia ya Serikali ni kuhakikisha kundi hili linapata Maendeleo kupitia shughuli zao hivyo kikao hiki kinawajengea uelewa wa mambo muhimu ikiwemo sheria, kanuni na taratibu za Serikali" amesema Mpanju.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Machinga nchini (SHIUMA), Ernest Matondo, wameishukuru Serikali kupitia benki ya NMB kwa kuwakutanisha kwani wana imani matokeo ya kikao hicho ni kuboreshwa zaidi kwa mazingira ya shughuli zao.
 
"Miundombinu kwenye masoko haijakaa vizuri, hivyo kama alivyosema Katibu Mkuu fedha hizo zitaboresha miundombinu ili Wamachinga waweze kufanya kazi vizuri zaidi, tunamshukuru pia Mhe. Rais kwa kulitambua kundi hili na kuliweka katika Wizara mahususi" amesema Matondo.
 
 

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.