MTANGAZAJI

ANWANI ZA MAKAZI MIEZI MITANO-WAZIRI NAPE 
 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania, Nape Nnauye amesema kuwa Serikali ya nchi hyo  itatekeleza uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa muda wa miezi mitano badala ya miaka mitano kama ilivyokuwa itekelezwe hapo mwanzo.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa semina ya utekelezaji mfumo huo katika Mkoa wa Pwani, Waziri Nape alisema kuwa zoezi hilo linafanyika kutokana na misingi mitatu ikiwemo ile ya Ilani ya Chama, Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na Tanzania kuwa sehemu ya dunia kwani ni mwanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU).

“Msingi wa anwani za makazi unajengwa na msingi mitatu ikiwemo Ilani ya chama  ya 2020 - 2025, Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na Tanzania kuwa mwanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja  wa Posta Duniani (UPU), suala hili linatekelezwa kwa miezi mitano tu badala ya miaka mitano kama Ilani inavyoelekeza, kwani itasaidia sana katika utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti mwaka huu”, amesema Waziri Nape.

Nape alisema kuwa katika utekelezaji wa zoezi hili hakuna mbadala isipokuwa ni kutekeleza kwa nguvu zote kwani Serikali ya Awamu ya Sita inadhamiria kuwasaidia wananchi katika kuboresha mawasiliano katika sehemu mbalimbali ikiwemo makazi yao, sehemu zao za biashara na maeneo mengine ya huduma za kijamii.

“Hapa hatuna kitu kingine zaidi ya utekelezaji wa zoezi hili, iwe mvua, iwe jua lazima jambo hili litekelezwe, Pwani mko nyuma sana mna kata 3 ambazo zimetekeleza jambo hili na nguzo 439 zimewekwa lakini bado kata 139, mahitaji yenu ni nguzo 75,392 na vibao 912,640 kwa hiyo utekelezaji wenu umefikia asilimia 1 bado asilimia 99”, amesema Waziri Nape.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa zoezi la uwekeji wa anwani za makazi litarahisisha utambuzi wa maeneo ya shughuli mbalimbali za mkoa wa Pwani yakiwemo maeneo ya viwanda.

“Anwani za Makazi na Postikodi ni mfumo mzuri ambao utatuonesha maeneo yetu mbalimbali kama mnavyofahamu kuwa Pwani ina viwanda vingi sana kwa hiyo uwepo wa anwani za makazi zitawarahisishia wananchi na zitarahisisha usafirishaji katika maeneo yetu”, alisema Kunenge.
 
Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza alisema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni Sekta mtambuka ambayo inawezesha sekta nyingine kuendelea.
“Kama mnavyofahamu kwamba Sekta ya Mawasiliano ni sekta mtambuka, sekta zote zinategemea sekta hii, kwa hiyo uwekaji wa anwani za makazi itarahisisha mawasiliano kwa wananchi, Wizara ya Mawasiliano inashirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ili kutekeleza jambo hili”, amesema Mhandisi Ichwekeleza.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.