MTANGAZAJI

WANANCHI WAKOSA MAWASILIANO YA SIMU YA TANZANIA, WATUMIA MTANDAO WA SIMU WA KENYA

 

 Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Mhandisi Kundo Mathew amefika katika kata ya Ikoma na kata ya Bukura ulipo Mpaka wa Kirongwe wilayani Rorya mkoani Mara, na kukuta hakuna mawasiliano kwa upande wa Tanzania hali inayowafanya wananchi wa kata hizo kutumia roaming ya Safaricom ambao ni mtandao wa nchi jirani ya Kenya.

“Ziara yetu sio ya kuona na kuondoka bali tunachukua hatua maeneo yenye changamoto kwasababu ni jukumu letu kuwafikishia wananchi huduma ya mawasiliano hili la watanzania kutumia mtandao wa nchi jirani sio sahihi kwasababu mbali na kutumia gharama kubwa kuwasiliana kupitia roaming pia wanalipa kodi nchi nyingine” amesema Mhandisi Kundo.

Akiwa katika ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mara na kutembelea Wilaya ya Tarime na Rorya amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepanga kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kupeleka mawasiliano katika Kata 11 za Wilaya ya Tarime na kiasi cha shilingi Milioni 290 katika kata 2 za Wilaya ya Rorya ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022.
 
Ameongeza kuwa Kata ya Ikoma na Bukura hazipo kwenye orodha ya kupelekewa miradi ya mawasiliano ndani ya mwaka wa fedha 2021/22 lakini wamejadiliana na wataalam alioambatana nao na kuamua kata hizo mbili zitapelekewa huduma ya mawasiliano kwa mpango wa dharura tofauti na utaratibu wa kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime Luteni Kanali Michael Mtenjele amesema kata 11 za wilaya hiyo kupelekewa huduma ya mawasiliano ni hatua muhimu ya kuimarisha ulinzi na usalama katika wilaya hiyo hasa inapotokea dharura yeyote mpakani mawasiliano yatasaidia maafisa waliopo mpakani au wananchi kuweza kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo Makao Makuu ya Wilaya kwa ajili ya msaada.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Rorya  Juma Chikoka ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa maamuzi waliyochukua ya kupeleka mawasiliano katika Wilaya hiyo kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma ya mawasiliano na mtandao ambapo kukosekana kwake kunasababisha ufinyu wa makusanyo ya mapato ikizingatiwa kuwa mashine za posi zinazotumika kukusanyia mapato zinatumia mtandao lakini pia ni mawasiliano ni muhimu ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya
mipakani.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.