MTANGAZAJI

PROGRAM TUMISHI YA ANWANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI NCHINI TANZANIA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania Dkt. Zainab Chaula amefungua mafunzo ya programu tumishi (mobile app) ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi kwa watendaji 175 wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, halmashauri za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela na wenyeviti wa Serikali za Mtaa wa Halmashauri hizo mkoani Mwanza.

Dkt. Chaula amefungua mafunzo hayo ya kujenga uelewa kwa watendaji hao ili
kufanikisha utekelezaji, matumizi na manufaa ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi ambapo mfumo huu utawawezesha watendaji wa Serikali ya Mtaa kuwa na taarifa za wakazi kiganjani kwa kuwa kila mwananchi atafahamika nyumba na mtaa anaoishi na kila mwananchi atakuwa na anwani ya makazi ya mahali alipo iwe mahali pa kazi, ofisini au biashara hivyo kuwezesha upatikanaji, upokeaji na upelekaji wa huduma kwa wananchi.

“Mtu akiamka kitandani kitu cha kwanza anaangalia simu kuona je ametafutwa, kuna ujumbe wowote hivyo hii inaonesha mawasiliano ni jambo la msingi katika kipindi hiki tofauti na miaka ya nyuma ambapo mawasiliano yalionekana ni anasa na sasa programu tumishi (mobile app) ya mfumo huu itarahisha utambulisho wa watu,kuwezesha utambuzi wa mwelekeo na maeneo ambapo mtu anataka kwenda, kuwezesha biashara mtandao, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kufanikisha usalama wa nchi”, amefafanua Dkt. Chaula.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekeleza
amesema kuwa utekelezaji wa mfumo huu unaendelea kwenye Halmashauri ya jiji la Mwanza na ya Manispaa ya Ilemela ambapo Taasisi ya Teknolojia ya Dar es
Salaam inaweka nguzo za majina ya mitaa zipatazo 5,300 na vibao vya namba za
nyumba 92,796 kwenye kata 18 na kazi imeanza kutekelezwa mwezi Februari, 2021 na itakamilika kwa muda wa kipindi cha miezi sita kwa gharama ya shilingi
1,357,356,832.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichalwe aliwaeleza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuwa TEHAMA ni mwambata wa Sekta ya Afya na mifumo yake inatumika kuhudumia wananchi kwa kuwapatia matibabu, vipimo, dawa, vifaa tiba na vitendanishi, bima ya afya hivyo TEHAMA inaboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hivyo amewataka wasimamie utekelezaji wa mfumo huu kama wanavyofanya kwenye sekta nyingine za elimu na maji.
No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.