MTANGAZAJI

WAZIRI WA FEDHA AAGIZA WATUMISHI 22 WA TRA WASIMAMISHWE KAZI

 

Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, amemwagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Dkt. Edwin Mhede kuwasimamisha kazi watumishi 22 wa Mamlaka hiyo wakiwemo baadhi ya Meneja wa TRA wa Mikoa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kujihusha na vitendo vya kifisadi na uzembe kazini vinavyoikosesha Serikali mapato.

Dkt. Mpango alitoa maagizo hayo Jijini Dodoma, alipokutana katika Kikao Kazi na Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Mameneja wa mikoa wa Mamlaka hiyo, kupanga mikakati namna ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali.

Aliagiza uchunguzi wa kina ufanyike kwa watumishi hao wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kutosimamia ipasavyo matumizi ya mashine za kutolea stakabadhi (EFD), kuwabambikia kodi kubwa wafanyabiashara na kuagiza apatiwe taarifa ya utekelezaji wa maelekezo yake ndani ya siku 90 kuanzia leo.

Dkt. Mpango aliagiza watumishi wanaopaswa kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi huo. Tanga: Afisa wa TRA Brighton Kasilo, Rukwa: Kaimu Meneja Nkasi Rogers Mkama, Shinyanga: Meneja wa kitengo cha ukaguzi Sara Senso na Meneja wa EFD Kwibin Nyamuhanga, Dodoma: Meneja wa Mkoa Bw. Kabula Mwemezi, Kigoma: Meneja wa Mkoa Jacob Mtemang'ombe, Kasulu: Meneja wa TRA Benward Mwakatundu, Songwe: Afisa TRA Janeth Mlack, na Joshua Daudi Samwel.

Wengine ni Kilimanjaro: Msimamizi wa kituo cha Tarakea Maududi Tingwa, Same: Adam Benta na Adam Ruhusa, Njombe: Maafisa Hilda Samuel Mahenge, Ibrahim Lyndama na Geofrey Mwinuka, Kagera: Meneja Biharamulo Alex Chacha, Ilala: Maafisa Stephen Kauzen, Kimweli, Ngobya, Raphael Meng'alai, Benedict Kasele na Nicodemus Mwandago, na Lindi: Kaimu Meneja Ruangwa, Florian Rubambwa.

“Nakuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Dkt. Edwin Mhede uwapumzishe kazi (relieve them from duty) kuanzia leo kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 na umwagize Mkuu wa Idara ya Mambo ya Ndani (internal Affairs) awachunguze wahusika wote ndani ya siku 90 na nipatiwe nakala ya taarifa hiyo ya uchunguzi na hatua zilizochukuliwa dhidi ya kila mmoja wao” Alisema Dkt. Mpango

Vilevile, Dkt. Mpango alimwagiza Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Edwin Mhede, kufanya uhamisho wa lazima wa Maafisa waliokaa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi na kwamba anatambua zoezi hilo litagharimu fedha nyingi lakini ni bora kufanya uhamisho wa watumishi hao kwa kuwa kukaa kwao muda mrefu kwenye vituo vyao kuna athiri utendaji kwa kuwa wengi wao wana mitandao ya kuiba fedha za umma.

Aidha Dkt. Mpango aliiagiza TRA kusimamia kikamilifu matumizi ya mashine za kutolea stakabadhi (EFD) nchini kote na kubaini stakabadhi za kughushi na mashine bandia zinazotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu na pia kutoa muda wa siku 15 kuanzia sasa hadi tarehe 31 Desemba, 2020 kuhakikisha changamoto ya kufutikafutika kwa stakabadhi zinazotolewa na machine hizo za EFD linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.


No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.