MTANGAZAJI

MKAKATI WA KUIPELEKA JAMII YA TANZANIA KIDIJITALI WAELEZWA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Zainab Chaula
akiongoza kikao cha kamati ya kujadili na kupitisha mpango mkakati wa kuipeleka
jamii ya Tanzania katika mfumo wa dijitali, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mji wa
Serikali Mtumba jijini Dodoma, kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.
Jim Yonazi.


Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WMTH) imeeleza mkakati wake wa Mpango wa kuipeleka jamii ya Tanzania katika mfumo wa dijitali kwa kuanza na Sekta ya Elimu na Sekta ya Afya ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt  Zainabu Chaula ameendesha kikao cha kamati ya utekelezaji wa mkakati huo katika ukumbi wa Wizara hiyo mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kwa lengo la kujipanga na kuuridhia mkakati huo ili kuhakikisha kunakuwa na uratibu mahsusi unaokidhi malengo yaliyokusudiwa.


Kamati hiyo inayojumuisha taasisi za Serikali ina mpango wa kuwashirikisha wadau mbalimbali wanaopeleka intaneti katika shule za umma, hospitali na vituo vya Afya ili kuhakikisha kinachotolewa na wadau kinakidhi mahitaji na vigezo vilivyokusudiwa vya kuipeleka jamii ya kitanzania katika mfumo wa dijitali, Aliongeza Dkt Chaula.


“Sisi kama Wizara tuna malengo na matamanio yetu, kupitia Sera ya TEHAMA ya Wizara ya mwaka 2016 na Sera ya Elimu ya TEHAMA ya mwaka 2014 ili kwa pamoja kama Serikali tujipange, turidhie na tushirikishe wadau wote wanaotuwezesha katika eneo hili ili kurahisisha ukusanyaji wa takwimu na kujua maeneo yaliyofikiwa”, alisisitiza Dkt Chaula.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Jim Yonazi amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu mbalimbali katika Sekta ya Afya na Elimu na kuongeza idadi ya shule,hospitali, Vituo vya Afya, barabara pamoja na ufikishaji wa umeme vijijini kupitia REA na kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya upelekaji wa huduma za intaneti katika maeneo hayo.


Aliongeza kuwa wananchi wanaofikiwa na  huduma hizo wanatakiwa kushiriki katika uchumi wa dijitali na Wizara ina jukumu la kuhakikisha huduma za mawasiliano na data zinawafikia Wananchi kwa kushirikiana na wadau ili juhudi za Serikali ziwe na matokeo chanya katika utoaji wa huduma bora katika Sekta ya Elimu na Afya.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku amesema kuwa mkakati huo una lengo la kuhakikisha miundombinu ya TEHAMA na huduma za mawasiliano zinatumika katika Sekta ya Afya na Elimu na kutimiza lengo la Serikali kupitia Wizara hii iliyopewa dhamana la kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 asilimia 80 ya wananchi wamefikiwa
na huduma za intaneti.


Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Ofisi ya Rais Tawala na Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Erick Kitali amesema kuwa mkakati huo utasaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kwa gharama nafuu kama vile vituo cha kutolea huduma jumuishi ‘one stop centre’ na huduma za tiba mtandao ambapo mpaka sasa ni vituo 12 ndio vimeunganishwa na huduma hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba amesema kuwa UCSAF ina jukumu la kuhakikisha TEHAMA inaleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi, na mpaka sasa wamekwishapeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 711, intaneti katika shule 481 pamoja na kuwezesha Tiba Mtandao.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.