MTANGAZAJI

HISTORIA YA MAISHA YA MAREHEMU MCHUNGAJI JOSHUA KAMENYA KAJULA ALIYEWAHI KUWA KIONGOZI WA WAADVENTISTA WA SABATO TANZANIA

 

KUZALIWA KWAKE
Mchungaji Joshua Kamenya Kajula alizaliwa tarehe 28 Disemba 1939; huko Maeneo ya Majengo wilaya ya Mbeya Mjini katika Mkoa wa Mbeya. Yeye ni mtoto wa Pili kuzaliwa kati ya watano kwa mama yake. Baba yake alikuwa na wake wawili.

Kwa upande wa mama yake ambaye ndiye alikuwa mke wa ndoa kwa baba walizaliwa wanaume watano. Alikuwa na ndugu wengine wawili waliozaliwa na baba yake kwa mke mwingine ambaye alirithiwa na baba yake baada ya kufiwa
na kaka yake. Hivyo, kwa ujumla anatoka katika familia ya watoto saba kwa baba na kwa mama watano. 

ELIMU YAKE
Marehemu mchungaji Kajula alipata elimu yake ya awali katika Shule ya kati (Middle School) huko Iganzo. Alisoma hapo mpaka darasa la sita mwaka 1955. 
 Hatimaye alipelekwa Suji Upper Primary darasa la Saba na la Nane. 

Aliendelea na masomo yake katika kiwango cha darasa la tisa na la kumi (Standard 9 and 10). Ni sawa na kusema form two kwa lugha ya leo. Hatimaye alijiunga na chuo cha Ualimu huko Ikizu, mkoani Mara. 

Alisoma Diploma ya ualimu kwa miaka miwili hatimaye kwenda kuajiriwa mwaka 1962. Wakati huo aliamua kujiendeleza na elimu ya kidato cha nne bado akiwa kazini kwa kusoma kwa njia ya binafsi (private). 

Alifanya kazi kuanzia mwaka 1962 kwa miaka miwili hatimaye akaenda kuchukua kozi ya miaka miwili ya Elimu ya Afya (Health Education) huko Hospitali ya Heri, mkoani Kigoma. 

Huo ulikuwa ni mwaka 1964 hadi 1966.Hatimaye ndipo alipoenda kuchukua mafunzo ya kichungaji mwaka 1967 hadi 1968 huko Bugema, Uganda. Alipata diploma ya uchungaji. 

Safari yake ya elimu iliendelea mwaka 1985 hadi 1988 alipenda India katika chuo cha Poona Spicer Memorial College kwa masomo ya digrii yake ya kwanza. Na akahamia huko Ufilipino kwa masomo yake ya digrii ya pili. Alianza mwaka 1989 hadi 1991. Na kurejea Nyumbani. 

KUAMINI KWAKE
Marehemu mchungaji alipata imani kupitia kwa mzungu mmoja aliyekuja kufanya kazi huko Misheni ya Iganzo. Mchungaji Kajula alikuwa akifanya kazi kwake ya house boy. Ndipo akawa mtu wa kwanza kupata imani katika familia yao.
Tunaweza kusema kuamini kwake ndio chanzo na mlango wa kuwafanya ndugu zake wote watano kujiunga na kanisa hili la Waadventista WaSabato. Hatimaye mama yake alikuja kuamini baadaye kabisa. Mchungaji Joshua Kajula alibatizwa mwaka 1952. Mchungaji aliyembatiza ni Mchungaji Jacques
aliyekuwa mmishonari huko Mbeya. 

MAISHA YA NDOA
Marehemu mchungaji Joshua Kajula alifunga pingu za maisha tarehe 12 Septemba 1964 na Merry Justine Kimera (ni mtoto wa mchungaji Justine Salimu Kimera). Ndoa hii ilifungwa na Mchungaji Rufoko aliyekuwa ni mwenyeji wa Rwanda huko Heri Hospital ambako mchungaji Kajula alikwenda kuchukua masomo ya elimu ya afya. Mungu ameibariki familia hii kuwa na watoto watatu. Wa kwanza Gloria, wa pili ni Enidi, na watatu ni Suzzana. Na kuwa na wajukuu watano. 

KAZI YA UTUMISHI NDANI YA KANISA
Marehemu mchungaji Kajula alianza rasmi kazi ya utumishi ndani ya kanisa kama mwalimu huko Masoko, Rungwe Historia Ya Maisha Ya Marehemu
mkoani Mbeya. Alianza kufundisha shule hiyo ya kanisa mwaka 1962. Hatimaye alihamishiwa katika Shule ya msingi Iganzo mwaka huo mwishoni. Alifanya kwa awamu mbili ya mwaka 1962 hadi 1964. Akaenda Heri Hospital na aliporudi mwaka 1966 alirudi tena Iganzo kama mwalimu. 

Wito wa kichungaji: Marehemu mchungaji Kajula alikuwa na wito huo kwa muda mrefu ndipo alipopelekwa kusomea uchungaji katika chuo cha Bugema. Aliporudi alipangwa kuwa mchungaji wa Morogoro kuanzia 1969 hadi 1971. Lindi mwaka 1972 – 1973. Songea mwaka 1973 kwa miezi sita tu. Hatimaye alirudi Lindi tena mwaka 1973 mwishoni mpaka 1975. 

KUWEKEWA MIKONO:
Marehemu mchungaji Kajula aliwekewa
mikono ya kichungaji Novemba 1974. Hii ni ngazi ya mwisho ya kichungaji kama uthibitisho wa kudumu wa kutumika katika utumishi huo.
 
Aliitwa kuwa mchungaji wa Zanzibar mwaka 1975 kwa wiki moja. Alienda kuripoti tu hatimaye akaambiwa abaki Dar-es-Salaam kuwa mchungaji wa Magomeni mwaka 1975 hadi 1977. 

Mwaka 1978 hadi 1985 aliitwa kuwa Mkurugenzi wa Lay Activities (Idara ya Huduma za Washiriki) wakati huo ikiwa pamoja na vijana, Dorkas, AMO na nyinginezo. Hatimaye ndipo alipokwenda masomoni huko India na Ufilipino. 

Mwaka 1991 Disemba alirudi masomoni. Na Januari 1992 alipangwa kuwa mwalimu wa chuo cha TASC (Tanzania Adventist Seminary College) kwa miezi sita tu. Mwaka huo huo alipelekwa kuwa Mwenyekiti wa Mara Conference kuanzia 1992 hadi 1996. Hatimaye aliitwa huko Tanzania Union Mission, Arusha makao makuu mwaka 1996 kama mkurugenzi wa idara ya Uchapaji na maeneo mapya ambapo alifanya kazi hiyo mpaka Januari mwaka 2000. Alipelekwa katika Field ya South West Tanzania kuwa mwenyekiti wake kuanzia 2000 mpaka 2005. Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Union hiyo ya zamani (Tanzania Union Mission) mwaka 2005 mpaka 2010. Ndipo alipostaafu kazi ya utumishi ndani ya kanisa Novemba 2010. 

JAMBO ATAKALOKUMBUKWA KATIKA UTUMISHI
Marehemu mchungaji Joshua Kajula atakumbukwa kwa mambo mengi ambayo ameyafanya wakati alipokuwa akitumika ndani ya kanisa kwa moyo wake wote. Aliishi maisha ya kawaida na kiwango cha chini kwa ajili ya kuwafikia waumini wote. Hakuwa na ubaguzi wa kikabila wa kitabaka. Aliheshimika na watu wote. Ndio maana hata alipokuwa anakaribia kustaafu rasmi 2006; bado kanisa likaona ni vyema aendelee kulitumikia kwa muda wa ziada ya miaka mingine mitano ambayo ilikuwa tayari ni nje ya miaka ya kustaafu. Kanisa litamkumbuka sana kwa unyenyekevu wake na upole
wake na pia swala la kuzielewa taratibu za kanisa na kuzisimamia vyema. Jambo la pekee sana ni pale alipokuwa anapenda kusali kwenye makanisa madogo madogo na makundi ya kanisa. Ni jambo ambalo ni nadra sana kwa viongozi wa ngazi kama yake kutenda hivyo kwa sababu ya majukumu mazito
waliyonayo. 

Ndugu na jamaa nao wanamkumbuka kama kaka yao ambaye alikuwa na upendo wa dhati kwa ndugu wote. Mtiifu kwa wazazi. Mlezi mwema kwa wazazi wake. Mdogo wake
Steven Kajula anasema “Kaka alifanya mambo ambayo kwa
tamaduni na desturi za wanaume wa Kinyakyusa hawafanyi.”
Alikuwa mfano wa kuigwa kama Mkristo kwa familia yake na
kwa jamii alimoishi. Alikuwa mcheshi anayechangamana na
watu. Anakumbukwa pia kama mtu aliyekuwa na hobby ya
kuendesha gari. Pamoja na umri mkubwa alikuwa na uwezo
wa kuendesha gari kutoka Dar-es-Salaam hadi Mbeya bila kuchoka katika uzee wake huu. Pia alikuwa mtu anayejali sheria
za barabarani kwani mpaka anafariki hajawahi kupata ajali
kwa maisha yake yote. Alikuwa makini sana barabarani. Ni
jambo la kujifunza kwetu sote.
MAJUKUMU MENGINE BAADA YA KUSTAAFU KWAKE
Marehemu mchungaji Kajula alijishughulisha na shughuli zake
ndogo ndogo kwani hakupenda kukaa tu nyumbani bila kazi.
Alifanya shughuli ndogo ndogo kama mtu ambaye amezoea
kufanya kazi muda wote. Lakini bado kanisa lake alilokuwa
anasali, alianza kusali bado likiwa kundi tu hatimaye likapangwa kuwa kanisa. Alifanya ushirika na kanisa la Kunduchi tarehe 6 Mei 2012. Na kuanzia mwaka 2013 mpaka mauti inapomkuta alikuwa na majukumu ya uzee wa kanisa, kiongozi wa uhuru wa Dini, na pia kwa hekima yake alichaguliwa awe mshauri wa wazee wa kanisa akishirikiana na mchungaji wa mtaa. Alifanya kazi hiyo huku akionyesha utii wa kuhudhuria semina mbalimbali zilizoitwa na viongozi wa juu bila kujali aliwahi kuwa kiongozi mkubwa wa kanisa katika ngazi ya
Union. 

 Na huku akiunga mipango mikutano yote iliyopangwa na ngazi za juu kwa kusimamia vyema katika utekelezaji
wa kanisa lake mahalia. 

MATATIZO YA KIAFYA NA KIFO CHAKE
Marehemu mchungaji Joshua Kajula alianza kuugua mwishoni mwa utumishiwake ugonjwa wa kisukari. Lakini aliweza kupata tiba miaka michache akapona kwani sukari yake ilirudi katika hali ya kawaida kutokana na matibabu aliyoyapata kutoka sehemu mbalimbali.
 
Mnamo mwaka jana alianza kupata tatizo la joto la mwili kupanda juu sana bila kushuka. Ndipo alipolazwa katika hospital ya Rabinisinia iliyoko maeneo ya Tegeta mwezi wa Disemba tarehe 24 hadi 25. Baadaye iligundulika kuwa ilikuwa ni malaria iliyosababisha joto kupanda sana. 

Alitibiwa malaria na Alitoka akawa na udhaifu wa miguu ikawa imepoteza nguvu ya kutembea. Hatimaye alianza kupata nafuu ya miguu. Lakini ghaflatena mwezi machi mwanzoni joto la mwili likapanda tena. Alipelekwa Rabinisia ambako alipimwa. Alilazwa kwa siku moja,aliporuhusiwa alirudi nyumbani. Usiku huo huo hali yake ilibadilika na ndipo alipopelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi. Siku ya jumatatu alipelekwa Muhimbili akapokelewa kama mgonjwa wa dharura (emergency patient) na kupelekwa wodini siku ya jumanne mpaka alhamisi. Na hali yake ikazidi kuwa mbaya ndipo alipoingizwa Chumba maalumu (ICU) siku ya Alhamisi jioni ambako alikaa mpaka Jumamosi Jioni alipofariki hakutoka tena hapo. 

Hivyo marehemu mchungaji Joshua Kamenya Kajula alifariki tarehe 19 MACHI 2016 SAA MOJA USIKU. 

Hapo ndipo ulipokuwa mwisho wa maisha ya Mtumishi wa Mungu Mchungaji Joshua Kamenya Kajula

1 comment

Unknown said...

Historia hii inatia moyo ninaamini mengi hayajaandikwa,lakini ingawa amekufa A ngali akinena.

Mtazamo News . Powered by Blogger.