MTANGAZAJI

MWANZA :SHILINGI BILIONI 230 ZIMEPOTEA NCHINI TANZANIA KUTOKANA NA AJALI ZA BARABARANI


Picha na wavuti blogImeelezwa kuwa  zaidi ya Sh. bilioni 230 zimepotea katika kipindi cha mwaka uliopita wa 2014  kutokana na ajali za barabarani nchi nzima.

Akizungumza katika ufunguzi wa semina ya madereva wa magari makubwa, mabasi ya masafa marefu na daladala jijini Mwanza juzi, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga amesema kiasi cha Sh. bilioni 230 zilipotea katika ajali zilizotokea kipindi hicho licha ya baadhi ya ajali hizo zingeweza kuepukika.

Katika semina hiyo ya kuwaelimisha madereva juu ya makosa ya kibinadamu yanavyochangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani, Konisaga amesema uzembe, ulevi, uchakavu wa barabara, ubovu wa magari ni miongoni mwa sababu za kutoa kwa ajali.
  
Meneja wa Usalama Barabarani  na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), Geofrey Silanda, amesema tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini Tanzania  zinaonyesha asilimia 75 za ajali za barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Mkoani Mwanza (Uwamata), Shabani Wandiba, aliitupia lawama serikali kuwa ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa kusababisha ajali za barabarani kutokana na kupanga muda wa magari kusafiri bila ya kuangalia umbali.
  
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Mrakibu wa Polisi Mohamed Likwata, anasema ajali nyingi zinasababishwa na madereva ambao wanashindwa kufuata sheria na alama za usalama barabarani kikamilifu.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.