DAR ES SALAAM:AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 60 JELA KWA KOSA LA KUBAKA MTOTO
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaa imemhukumu
Goodluck Aloyce (31) mkazi wa Tabata Msimbazi jijini humo , kifungo cha miaka
60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kumlawiti shemeji yake mwenye
umri wa miaka 11 mara kwa mara.
Akisoma hukumu hiyo katika Mahakama
ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan amesema, mashahidi
sita walioletwa na upande wa mashitaka waliisaidia mahakama kuthibitisha kwamba
mshitakiwa alimbaka na kumlawiti mtoto huyo.
Amesema ripoti kutoka kwa daktari
(PF3) iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo, ilionesha kuwa mtoto huyo
alikuwa akiingiliwa kimwili mara kwa mara na mshitakiwa.
Kabla ya kusomewa adhabu, Wakili wa
Serikali, Felista Mosha aliitaka mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili
liwe fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo hivyo ambapo mshitakiwa aliiomba
mahakama hiyo imwachie awe huru, ombi ambalo halikutiliwa maanani na mahakama
hiyo.
Katika kesi hiyo, mshitakiwa alikuwa
anakabiliwa na mashitaka mawili ya kubaka na kulawiti mtoto huyo mwenye umri wa
miaka 11 kinyume na sheria.
Post a Comment