MTANGAZAJI

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA KUFUNGA KIFAA MAALUM KWENYE PAMPU ZA MAFUTA

Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) imeamua kufunga kifaa maalum cha kuratibu mauzo ya mafuta kwenye pampu za mafuta katika vituo vyote vya mafuta nchini.

Mamlaka hiyo imesema  tayari taratibu zimekamilika kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinafungwa vifaa hivyo maalum,ili kuondoa wizi wa kodi ya mafuta.

Afisa Mwandamizi Mkuu wa Elimu TRA Makao makuu,Hamisi Lupenja, amewaambia waandhishi wa habari jijini humo kwamba mashine hizo zitakazofungwa kwenye pampu za mafuta, zitakuwa na uwezo wa kutuma taarifa za mauzo ofisi za TRA kila siku.

Amesema,wamekuwa wakikamilisha taratibu za kutumia kifaa hicho,ili kukomesha wizi na ukwepaji kodi katika vituo vya mafuta; na zoezi hili litafuta zoezi linaloendelea la matumizi ya Mashine za EFDs.

Lupenja, amesema mashine hizo za kuratibu mauzo ya mafuta na kodi ni muhimu pia katika utunzaji wa kumbukumbu za biashara na kodi.

Kauli hii ya TRA inakuja hivi sasa wakati mfumo wa kutoa risiti wa kielektroniki(EFDs) unaposababisha migogoro na migomo ya wafanyabiashara hapa nchini.

Kuhusu wafanyabiashara kununua mashine hizo kwa bei ya shilingi 200,000 katika nchi jirani ya Kenya,Mamlaka hiyo imesema, mashine za EFDs zinazouzwa hapa nchini zimeongezwa thamani zaidi na zina ubora .

Rupenja amesema,mashine hizo zina uwezo wa kutumia lugha mbili ya Kiingereza na Kiswahili,ili kuwawezesha wasioelewa lugha mojawapo kuzitumia; na  zinauwezo wa kutunza kumbukumbu na kuratibu mauzo yote ya mwaka,na ya mwezi  mzima.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.