MTANGAZAJI

ANUSURIKA KIFO TOKA KWA MUMEWE BAADA YA KUGAWA MOTO KWA JIRANI


  Rispa Joshua akiwa amelazwa hospitali ya Halmashauri ya mji wa Tarime baada ya kupigwa na mumewe kwa sababu ya kugawa moto 
Rispa Joshua akihojiwa na Waitara Meng'ang'anyi wodi namba 6 katika Hospitali ya Halmashauri mji wa Tarime(picha zote na Frankius Cleophace).  
 
Mwanamke mmoja Rispa Joshua miaka 34 mkazi wa mtaa wa Songambele, kata ya Sabasaba katika halmashauri ya mji wa Tarime amenusurika  mauti baada ya kushambuliwa  na mumewe sehemu mbalimbali za mwili  kwa kutumia mateke, kunyigwa na fimbo kwa kosa la kugawa moto kwa jirani .

Akiongea kwa shida katika wodi namba sita katika hospital ya mji wa Tarime Bi Rispa alisema kuwa tukio hilo lilitokea  mapema wiki iliyopita baada ya kutoka shambani na jirani yake kufuata moto ambapo alimkubalia na kumpa  jambo lililomkasirisha mumewe kwani hataki jirani ama mtu yeyote kuingia kwake akidai  wanamroga.

Bila kutambua kuwa muwe alikuwa karibu, Bi Rispa akiendelea kuchochea moto alianza kushambuliwa na mume huyo katili kwa kumkanyaga kwa mateke mgongoni na kuanguka kisha kuanza kumnyiga kabla ya kuendelea kumshambulia kwa fimbo hadi kuzimia.

“Jirani alifuata moto nikampa,hataki mtu aje kwake anasema wanamroga” alisema Rispa

Mume huyo katili hataki jirani ama mtu yeyote kukanyaga kwake kwa kudai kuwa wanamroga wanapoingia kwake kwa  kuwa kati ya watoto wane waliojaliwa kupata watatu walifariki hivyo kuwatuhumu majirani kuwa ndio wachawi wa familia yake.

Baada ya kutimiza azima yake ya kumsurubu mkewe, Joshua alindoka na kumwacha mkewe chini akiwa amezimia na kutoroka kwa kudhani kuwa amekwishamuua ambapo jirani na shemeji zake Rispa walikuja kumchukuwa kumkimbiza hospitalini.

“Sijui ni nani walionileta hapa na sijui ni nani ananihudumia” alisema Rispa kwa taabu huku akibubujikwa na machozi.

Cretus Deus ni mganga aliyekuwa zamu aliyempokea Rispa wakati alipopelekwa na shemeji zake akiwa hajitambui ambapo alilazimika kumhudumia ingawa hawakuwa na barua kutoka polisi maarufu kama PF3.

“Baada ya kupata maelezo kuwa alikuwa amepigwa na mumewa na kutokana na hali aliyokuwa nayo nilimpokea na kuanza huduma ya utabibu ambapo nilipima viashilia vya uhai na baada ya kuona kuwa viko sawa nilimlaza wodini akiwa hajitambui lakini leo asubuhi nimepata taarifa kuwa amejitambua na kuanza kuongea ingawa ni kwa shida” alisema Deus siku ya jumamatano ofisini kwake.

Matukio ya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake unatokea katika jamii yetu kwa kiasi kikubwa ingawa jamii yetu hailioni hili kuwa ni tatizo hali inayoifanya isiripoti sehemu husika ili kupewa utatuzi na pengine kutatuliwa na kuweza kupungua.

Kati ya wanawake 10 watatu hufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki yao ya ndoa,kukeketwa, kubakwa, kutopewa mahitaji ya familia kama vile matumizi huku wakiendelea kuombwa chakula na waume zao hali inayoonesha kuwa mfumo dume ni mkubwa katika jamii yetu ya Tanzania.

“Mwanzoni nilidhani kuwa ni tatizo la jamii lakini nikaja kughundua kuwa eneo la Tarime lina kesi za namna hii nyingi na mwezi haupiti bila kupokea mwanamke amepigwa ama kakatwa na kutolewa pengine kiungo na hii inaonesha kuwa elimu ya kijinsia bado haijawafikia wananchi ipasavyo” alisema Deus.

Aidha aliomba taasisi na mashirika ya serikali na ya  binafsi wakiwemo watu binafsina hata  familia zenyewe kusaidia kukemea watu wenye tabia hizi chafu zinazoonesha mfumo dume katika jamii.

“Jamii itusaidie kulikemea hili kwani tunapata kazi za ziada kuwashughulikia majeruhi hawa ambapo tungeweza kuwahudumia wagonjwa wengine kwa kuwa tunapata wagonjwa wengi ambao wengine wanakuwa na magonjwa ambayo yanahitaji huduma nyeti lakini unalazimika kumhudumia huyo kwa kumwonea huruma kuwa anaweza kupoteza maisha ikiwa hutafanya hivyo kwa muda huo” Dues alisema

Chama cha waandishi wanawake Tanzania (TAMWA) kimekuwa kikionesha jitihada za dhati  kuhakikisha kuwa ukatili wa kijinsia unapungua katika jamii ya Tanzania ili kuleta usawa. Kwa kulielewa hili wanatoa semina mbalimbali kwa waandishi wa habari na kwa jamii yenyewe ili kupitia elimu hiyo iachane na tabia hii.

Godfrida Jora ni afisa programu wa  TAMWA hivi karibuni akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hii alionesha kusikitishwa kwa tabia za wahanga walio wengi kutoripoti matendo ya kikatili wanayofanyiwa na waume zao ama viongozi wa kazi maofisini kwa kuogopa kuachika ama kufukuzwa kazi hali inayowafanya wanaume hao waendee na tabia yao hiyo chafu.

“TAMWA tuna sisitiza kuwa mwanamke yeyote anayetendewa ukatili wa aina yoyote atoe taarifa katika vyombo husika ili aweze kupewa msaada wa kisheria kwa kuwa mtandao wetu ni mkubwa na upo kila Wilaya, wapo waandishi wa habari na hata maafisa wa jeshi la polisi ambao hufuatilia matukio haya kwa ukaribu” alisema Jora.

Hata hivyo mahakama zimekuwa zikichelewesha kutoa hukumu ya vyesi vinavyohusu ukatili wa kijinsia ama watuhumia kufungwa muda mfupi ama kuachiwa huru hali inayoifanya jamii kuona kuwa hakuna haja kwao kuendelea kuhangaika na vyesi ambavyo vitapoteza muda na mwisho haki isitendeke.

“Kwa sasa wapo maafisa wa polisi wanaofuatilia kesi za  namna hii mahakamani kuhakikisha kuwa hazichukui muda mrefu kutolewa hukumu hivyo nitoe rai kwa wale wanaotendewa ukatili wahudhurie vyesi vyao hadi wahakikishe kuwa wamepata haki yao” alisema Bi Jora.

Mwandhishi wa habari hizi alipotaka kupata kwa uhakika habari hizi na kjujiridhisha kama zimeripotiwa katika vyombo vya sheria ilionekana kuwa jeshi la polisi lilikuwa halijazipata.

“Mpaka sasa hatujapata taarifa ya namna hiyo ndugu mwandhishi, na hata OCD naye hajapata pengine vijana wetu hawajakamilisha naomba uje kesho saa mbili asubuhi utazituta, tunashukuru kwa taarifa tutaifanyia kazi kwa haraka” alisema stafu sajenti Sweetbert Njawike.
Na Waitara Meng'anyi-Tarime

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.