MTANGAZAJI

MAONYESHO YA ASALI JIJINI DAR ES SALAAM



Maandalizi ya maonyesho ya Asali yatakayofanyika Dar es salaam katika viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba) vilivyopo barabara ya Kilwa tangu tarehe 3 hadi 7 Oktoba 2012 yamekamilika. Wananchi wanakaribishwa kuhudhuria maonyesho hayo ambayo hayatakuwa na kiingilio. 

Katika maonyesho hayo watu wataelimika kuhusu manufaa yatokanayo na asali, pia watapata utaalam wa kufuga nyuki na wataonja na kununua asali bora kwa bei nafuu. Kaulimbiu ya maonyesho hayo ambayo ni ya kitaifa ni ASALI KWA AFYA NA USTAWI (HONEY FOR HEALTH AND PROSPERITY). Maonyesho hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na wadau wengine wa Sekta ya Ufugaji Nyuki. Lengo kuu la maonesho ni kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya nyuki. Tarehe 3 Oktoba ni siku iliyotengwa maalum kwa ajili ya kufanyika Kongamano la Ufugaji Nyuki. Hivyo wafugaji nyuki, wataalam na wadau mbalimbali wa Sekta hiyo wanakaribishwa kuhudhuria kungamano hilo ambalo litafanyika katika ukumbi wa J. M. Kikwete ulioko kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere . 
 

Ufunguzi rasmi wa maonyesho hayo utafanyika tarehe 5 Oktoba 2012 ambapo Mgeni Rasmi anategemewa kuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb). Waonyeshaji waliothibitisha kushiriki ni Halmashauri za Wilaya zote, kampuni zinazonunua asali, watengenezaji wa mizinga na vifaa vingine vya kisasa vya ufugaji nyuki, na watengenezaji wa bidhaa zinaotumia asali na nta kama malighafi. Inategemewa kuwa katika maonyesho hayo waonyeshaji watajitangaza ili waweze kupata wanunuzi wa asali na mazao mengine ya nyuki. 
 

Pia wanunuzi wa mazao ya nyuki watapata fursa ya kuwafahamu wafugaji. Aidha inategemewa kuwa utaundwa mtandao ambao utawaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wataalam na wadau wa sekta ya nyuki.
 
 George Matiko
 MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 
30 Septemba 2012



No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.