MTANGAZAJI

TAARIFA KWA UMMA TOKA CHADEMA


TAARIFA KWA UMMA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinahimiza wanachama wake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kutoa maoni kwa tume ya mabadiliko ya katiba ili taifa lipate katiba mpya.

Aidha, CHADEMA kinatoa mwito kwa wananchi kuondokana na mtizamo kwamba haiwezekani kutoa maoni ya katiba mpya bila kwanza kuifahamu kwa kina katiba iliyopo bali waelewe kwamba mchakato huu unahusu kuandika katiba mpya hivyo jambo la msingi ni wananchi kujitokeza kwa wingi mbele ya tume ya mabadiliko ya katiba mpya na kutoa maoni kwa kueleza maudhui ya Tanzania wanayoitaka.

Pamoja na kutoa maoni kuhusu maudhui ya masuala ya kuzingatiwa katika katiba mpya, CHADEMA kinatoa mwito kwa wanachama na wananchi kutoa pia maoni kuhusu mchakato wa katiba mpya ili kuiwezesha tume kuishauri serikali kuendelea kuiboresha sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011 ikidhi mahitaji ya kujenga kuaminiana na muafaka wa kitaifa kwa mawasiliano na mashauriano na wadau mbalimbali.

Pia, CHADEMA kinatahadharisha kuwa uamuzi wa tume kutoa elimu wakati huo huo ikikusanya maoni utaathiri mchakato wa katiba; hivyo pamoja na kutoa mwito kwa umma kwenda kutoa maoni kwa tume, CHADEMA kinaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kwa wanachama na umma kuhusu mabadiliko ya katiba.

Wanachama na wananchi kwa ujumla wazingatie ratiba ya kukusanya maoni kwenye mikoa minane kuanzia tarehe 2 Julai 2012 hadi tarehe 30 Julai 2012 iliyotangazwa na tume ya mabadiliko ya katiba katika vyombo vya habari na katika tovuti ya www.katiba.go.tz

Mikoa hiyo ni Tanga, Kagera, Dodoma, Pwani, Shinyanga, Manyara, Kusini Unguja na Pemba; na kwa namna ya pekee CHADEMA kinawakumbusha wananchi wa wilaya za Lushoto, Biharamulo, Bahi, Mafia, Kahama, Mbulu na Kusini ambapo tume ya mabadiliko ya katiba itaanzia tarehe 2 Julai 2012 kujitokeza kutoa maoni kuwezesha nchi kupata katiba mpya. 

 
Izingatiwe kwamba wajibu wa kisheria wa tume ya mabadiliko ya katiba ni kuyapokea maoni na maudhui hayo na kuandika ripoti na hatimaye kuyaweka katika muundo wa kikatiba wakati wa kuandaa rasimu ya katiba.

“Wananchi waelewe kwamba mchakato wa katiba mpya unahusu hatma ya nchi na maisha ya wananchi, kwa mfano kwa muda mrefu pamekuwepo migogoro katika jamii mingine kuhusu ardhi na rasilimali nyingine. Kupitia mchakato wa katiba mpya wananchi watoe maoni juu ya misingi ya kikatiba ya kushughulikia hali hiyo na kulinda haki za msingi za binadamu”.

“Aidha, taifa lipo katika hali tete hivi sasa kutokana na tishio la migomo ya madaktari, walimu na watumishi wengine wa umma; chanzo kikiwa mgawo usio sawa wa rasilimali za nchi unaofanyika wakati wa bajeti, huku mamlaka makubwa ya kikatiba ya ugawaji na usimamizi wa fedha za umma yakiwa kwa Rais na serikali badala ya bunge ambacho ndicho chombo kikuu cha kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Hivyo, wananchi wajisikie huru kwenda kueleza maudhui ambayo wamekuwa wakiyasema mara kwa mara ya kutaka madaraka ya Rais kupunguzwa na pia kuweka misingi muhimu ya kudhibiti ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa maoni kwenye tume ya mabadiliko ya katiba.”

Ifahamike kwamba miaka mitano iliyopita CHADEMA kilisambaza kwa ngazi zake zake za chini za chama waraka na. 4 wa 2007 kuhusu madai ya katiba mpya ambao ulitoa elimu kwa umma baadhi ya masuala ya kuzingatiwa juu ya katiba. Katika waraka huo CHADEMA kilielekeza viongozi na wanachama wake kwamba hoja ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi iwe ya kudumu katika vikao vya kikatiba vya chama pamoja na mikutano na wananchi mpaka pale taifa letu litakapokuwa na katiba mpya.

Kwa upande mwingine, ikumbukwe kuwa CHADEMA kilishawatahadharisha watanzania kuzingatia  kwamba marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba yaliyofanyika mwezi Februari 2012 yalikuwa  ni ya hatua ya kwanza ya kuwezesha kuundwa kwa tume shirikishi ya katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa ripoti na rasimu ya katiba mpya. 
 
Hivyo, ili kuwa na uhakika na mustakabali wa maoni yanayotolewa, wananchi watoe pia maoni kwa tume kuhusu mchakato wa katiba na pia kuitaka serikali itoe ratiba ya kufanyika kwa marekebisho mengine muhimu ya awamu nyingine kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba mpya na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki kabla ya mchakato kufikia katika hatua husika.

Wakati huo huo; CHADEMA kinatoa tahadhari kuhusu uamuzi wa tume ya mabadiliko ya katiba kutangaza moja kwa moja ratiba ya kukusanya maoni ya wananchi bila kwanza kuwa na ratiba ya kutoa elimu kwa umma kuhusu mchakato wa katiba, katiba, ukatiba na masuala ya katiba. 

Uamuzi wa tume kutoa elimu wakati huo huo ikikusanya maoni unaweza kuathiri mchakato wa katiba; hivyo pamoja na kutoa mwito kwa umma kwenda kutoa maoni kwa tume, CHADEMA kinaendelea na mpango wake wa kutoa elimu kwa wanachama na umma kuhusu mabadiliko ya katiba na inazitaka ngazi zote za chama kuzingatia waraka na. 3 wa mwaka 2011 kuhusu sheria ya mabadiliko ya katiba na kutoa elimu kwa wananchi kuwezesha nchi kupata katiba mpya na bora.

Imetolewa tarehe 1 Julai  2012 na:

John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.