MTANGAZAJI

NENO LA LEO: JAMII YA WALO WEMA IMSAMEHE ELIZABETH "LULU"MICHAEL

Ndugu zangu,

Jana amemezikwa Steven Kanumba , kipenzi cha wengi.
 Mauti ya Steven Kanumba yanatukumbusha wanadamu ukweli huu; kuwa maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana. Hivyo, lililo jema kwetu wanadamu ni kuishi kwa kutenda yalo mema. Kuwatendea mema hata tunaodhani wametukosea, maana, tutawasaidia kujifunza kutenda mema. Na ni mwanadamu gani asiyekosea?

Na moja ya adhabu kubwa  mwanadamu unaweza kuipata humu  duniani kutoka kwa wanadamu wenzako ni adhabu ya kutengwa na wanadamu wenzako.

Msichana Lulu ameshapata na anaendelea kuipata sasa, adhabu kubwa sana kutoka kwa wanajamii. Adhabu ya kupewa hukumu ya mauaji na kutengwa na wengine. Lulu , ambaye ni mmoja wa waliokuwa karibu na marehemu Kanumba hata katika dakika zake za mwisho maishani, na ambaye alikuwa mpenzi wa Kanumba, hakuweza kushiriki mazishi ya mpenzi wake. Hiyo nayo ni adhabu kubwa kwa Lulu kupewa na wanadamu wenzake.

Yumkini Lulu ana mapungufu yake kama mwanadamu, lakini, kwa sasa hastahili adhabu kali hiyo kutoka kwa wanajamii. Kwa kosa ambalo hakuna aliye na hakika leo kuwa amelitenda. Ndio, Lulu aweza kuwa mwanadamu mwenye mapungufu yake mengine, lakini , hayo yasitufanye wanadamu tuwe na haraka ya kumpa hukumu isiyo ya  haki.  Na kwenye mienendo ya maisha, ni mwanadamu gani asiye na mapungufu?
  
Maana, tangu mara ile ilipofahamika, kuwa msichana Elizabeth ‘ Lulu' Michael alikuwepo kwenye mazingira ya kutokea kwa kifo cha Kanumba, basi, jamii, huku ikisaidiwa na vyombo vya habari, haraka ikapata wa kumnyoshea kidole. Na hukumu ya Lulu kutoka kwa wanajamii walo wengi ikawa imetolewa hapo. Kwamba Lulu ndiye muuaji. Kwa sasa, hukumu hiyo haiwezi ikawa ya haki mpaka pale wenye mamlaka ya kututhibitishia hilo watakapofanya hivyo.

Na  hata kama ugomvi, uliotokana na wivu wa kimapenzi ,  wa  Lulu na mpenzi wake ulipelekea mauti ya Kanumba, bado  maelezo tuliyoyasikia  hayamwonyeshi Lulu kuwa na dhamira ya kutaka kutenda maovu anayohukumiwa na wanajamii kuwa  kayatenda. Hivyo, naye, kama mwanadamu, anastahili msamaha kutoka kwa  wanajamii wengi walo wema.

Katika wakati huu mgumu sana kwa msichana Lulu, vyombo vya habari viwe  mbele katika kumsaidia Lulu kama mwanadamu mwenzetu, badala ya kutumia balaa lililomkuta kama mtaji wa kuandika na kutangaza  udaku wa kuuzia magazeti na kuvutia watazamaji wa runinga na wasikilizaji wa  redio. 

Maana, kwa adhamiriae kutumia magumu yanayomkabili  msichana Lulu kuvuna, basi, hana atakachokivuna zaidi ya kuvuna dhambi.

Badala yake, media isaidie katika kutufanya wanajamii tujitafakari.  Kwa vile, habari za matukio ya mahusiano yasiyo na staha na matendo ya kiuhuni yanayofanywa na baadhi ya wanajamii wakiwemo wasanii,  huwa yanashabikiwa na vyombo vya habari  badala ya vyombo hivyo kushiriki kukemea na kuelimisha jamii. inasikitisha, kuwa katika wakati huu, vyombo hivyo vya habari vyaweza kabisa kuwa  kwenye harakati za kuandaa stori zaidi za ‘ kumning’iniza’ zaidi Lulu ambaye tayari ameshaning’inizwa hadharani.

Ndugu zangu,

Kama wanajamii, na wengine kama wazazi. Lulu anabaki kuwa ni msichana mdogo anayehitaji kusaidiwa katika wakati huu mgumu kwa maisha yake. Yumkini vyombo vya dola vinaweza vimtie au visimtie hatiani. Hivyo,  kumwachia huru Lulu.  

Lakini, bado hukumu ya jamii ikabaki pale pale. Hukumu ya Lulu kutengwa na jamii.  Hiyo ni hukumu mbaya zaidi  inayoweza kuchangia hata kuyafupisha maisha ya msichana huyu mdogo. Jamii haina faida na hukumu kama hiyo.  Ni heri ikamwacha huru aende akapambane na yanayomkabili mbele yake. Ndio, akapambane na  maisha haya magumu ya dunia hii bila kujisikia kutengwa na wanajamii wenzake.

Na naamini, leo  kuna wengi kama mimi,  wenye kufikiri hili, kuwa jamii ya walo wema imsamehe Elizabeth ‘ Lulu’ Michael.

Na hilo ni Neno La Leo.


Maggid Mjengwa
Dar es Salaam.
0788 111 765
http://mjengwablog.com

1 comment

Unknown said...

ni kweli kabisa wengi wetu tunashindwa kufikiri kwa kina na kutanguliza hukumu bila haki.kiukweli LULU hana makosa kama inavyosadikika siamini kabisa kama binti yule ana nguvu kias hicho za kumsukuma kwa nguvu kanumba pia ugomvi ni sehemu ya maisha ya wapendanao kwahiyo hakuna cha ajabu me nafikiri tuachie mahakama itende kazi na baadhi ya vyombo vya habari waache kufanya yasiyowahusu tu kwakuangalia historia ya lulu na chuki zao dhidi yake wanapotosha jamii na kujenga chuki kwa binti wa watu.kifo ni mipango ya mungu hajui mtu cku wala saa.nakuombea lulu naimani siku moja utakuwa huru

Mtazamo News . Powered by Blogger.