MTANGAZAJI

NENO LA LEOMatatizo yetu mengi yanatokana na sisi wenyewe. Wenzetu Ulaya na Marekani wanasema; “Time is Money”. Kwa tafsiri ya moja kwa moja, unamaanisha kwamba muda ni pesa. Lakini, tafsiri sahihi hapo ni umuhimu wa muda.

Kwamba muda ni kitu cha thamani sana. Na hakika, kwa mwanadamu, jinsi unavyoutumia muda wako hivi leo ni ishara tosha ya jinsi kesho yako itakavyokuwa.

Tumekuwa watu wa kulalamika sana. Na tumemwachia Mungu jukumu la kutukomboa kutoka kwenye umasikini wetu. Hapana, Mungu hausiki na umasikini wako. Jukumu la kwanza la kujikomboa kutoka kwenye umasikini ni lako mwenyewe. Na hakuna njia ya mkato, bali ni kufanya kazi, kufanya kazi na kufanya kazi. Achana na ndoto za kuamka na kuvuna mamilioni. Bila kufanya kazi!
 
Inakuwaje basi kwa  mwanadamu mmoja awe na muda na mwingine asiwe nao?
 
Kuwa au kutokuwa na muda inatokana na mipangalio yako ya maisha. Binadamu unapaswa kuwa na bajeti ya muda wako. Ni jinsi unavyoutumia muda wako.  Jinsi unavyopangilia mambo yako, ratiba zako na mengineyo.
 
Ukiwa na utaratibu huo, basi, waweza kabisa kuwa na muda wa kutosha kufanya mambo mengine mengi uyapendayo ikiwemo mapumziko, kuwa na muda na familia yako, kuwa na muda wa kujisomea na mengineyo.
 
Ndio, lililo muhimu ni kuwa na vipaumbele. Unapoandika orodha ya shughuli zako za siku, juma, mwezi na hata mwaka, basi weka kipaumbele katika mambo ambayo ni muhimu zaidi. Hayo yaweke juu kabisa katika orodha yako. Kipaumbele kinaweza kutokana na umuhimu wako binafsi kwa jambo fulani.
 
Usiwe mtu unayesukuma mambo mbele. Mtu mwenye hulka ya kuahirisha mambo. Linalowezekana kufanyika lifanye. Kauli za ’ hili nalifanya kesho’ au ’ namwachia Mungu,’ ni kauli za mtu aliyekata tamaa kwenye mapambano ya maisha.
 
Wahenga walinena; ’’Linalowezekana leo lisingoje kesho!’’ Hulka ya kusukumia mbele mambo ina tafsiri moja tu; kuwa unaongeza mzigo wa mambo ya kufanya. Huna unachokipunguza. Ni mwanzo wa kupatwa na msongo (stress). Ni mwanzo wa kuchanganyikiwa. Ndipo hapo utamwona mwanadamu mwenzako akitembea huku akiongea peke yake.
 
Ni muhimu pia kuwa na muda na marafiki. Naam, weka bajeti ya muda. Okoa muda upate muda wa ziada. Na baadhi ya marafiki zako waweza kuwa sababu ya matumizi mabaya ya muda wako. Ndio, marafiki wengine ni marafiki wa kukupotezea muda tu. Angalia, ni marafiki wa aina gani ulio nao.
 
Inasemwa, ukitaka kumfahamu mtu alivyo, basi, angalia aina ya marafiki zake. Kwa mfano kama una rafiki ambaye hazingatii muda, hana miadi ya uhakika, basi,  huyo anaweza kuwa mzigo katika suala zima la matumizi ya muda.
 
Usiwe mtu mwenye kufuata mkumbo, eti kwa vile wengine hawazingatii muda, basi, na wewe unajifanya ni mtu usiyejali muda. Hapo utakuwa unajipoteza mwenyewe. Ni muhimu, hata unapokuwa na marafiki zako, uwe mbele katika kuhakikisha mnatumia muda wenu vizuri.

Uwe tayari na mipango kichwani hata kabla hujakutana na rafiki au marafiki zako. Kisha mshirikishe rafiki au marafiki zako katika mipango uliyoifikiria kwenye mambo ya kufanya. Na usiwe mtu mwenye kupanga mambo mia moja kwa wakati mmoja. Uwe na mipango miwili au mitatu ya kujadili na wenzako. Kesho ndio uje na mingine.
 
Ni bahati mbaya kwetu wanadamu, kuwa muda mwingi sana huwa tunaupoteza kutokana na kutopangilia vizuri mambo yetu. Upo umuhimu kwa mfano wa kupangilia shughuli zetu kutokana na sehemu za kijiografia.
Kwa mfano, kama una shughuli ambazo zinahitajika kufanyika mjini, hakikisha kwamba unapokwenda mjini, unazikamilisha zote kwa wakati mmoja. Kwanini uende mjini zaidi ya mara nne kwa siku?
 
Naam, Mungu hahusiki na umasikini wako. Muda ni mali. Panga bajeti ya muda wako, sasa! Na hili ni Neno La Leo.
( Makala haya yamechapwa kwenye gazeti Mwananchi, leo Jumapili)

2 comments

Anonymous said...

hakuna serikali ya wapumbavu hapa tanzania elizabeth michael hawezekani aachiwe huru hivihivi lazima ahukumiwe tu vinginevyo tutaanadamana mpaka kieleweke hii ni mader kesi tena ni muuaji huyu afungwe tu

wambura said...

hakuan lulu kuachiwa hapa haiwezekanai aue halafu aachiwe kizembe full kipigo tena serilikari ijiangalie sana juu ya hili swala.kabisa sisi watanzaia tumesema

Mtazamo News . Powered by Blogger.