MTANGAZAJI

TAARIFA RASMI YA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA KUHUSU MGOMO WA MADAKTARI NCHINI

UTANGULIZI
Mgomo wa Madaktari ambao umedumu kwa takriban wiki mbili nchini sasa ni dhahiri kwamba umelitikisa Taifa na kuathiri huduma za tiba katika hosipitali kadhaa nchini. Mgomo huu ulianza taratibu na kuendelea kukua kutokana na mvutano, pia vita ya maneno baina ya Serikali na Madaktari.

HALI ILIVYO SASA
 1. Kutokana na taarifa zinazofikishwa katika vyumba vya habari, ni dhahiri kwamba hali ni mbaya sana katika baadhi ya hosipitali nchini hasa Hosipitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo mgomo huu umesababisha vifo vya watu ambao huenda wangepona kama wangepata huduma.

 1. Wagonjwa mahututi wanaofikishwa MNH kwa ajili ya huduma za rufaa hawapokelew,maiti wanaofikishwa kwa ajili ya kuhifadhiwa chumba cha kuhifadhi maiti (mortuary), hawapewi hifadhi na badala yake wanarejeshwa walikotoka.

 1.  Hata katika hosipitali ambazo madaktari wameripotiwa kurejea kazini, huduma zinazotolewa ni hafifu hii ikimaanisha kwamba mgomo bado unaendelea hata kama si kwa madaktari kukutana kwenye kumbi kama ilivyokuwa mwanzo.

 1. Madaktari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wamepelekwa katika hosipitali za Serikali kuokoa jahazi, hawatoshelezi lakini katika baadhi ya maeneo wamepata upinzani kutoka kwa wauguzi wa hosipitali husika.

MAPENDEKEZO
Kutokana na hali ilivyo sasa, Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika kikao cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kilichokutana leo Jumanne 31 Januari 2012, wamesema “Inatosha” kwa na kwamba hali isiachwe ikaendelea na kupendekeza yafuatayo:

 1. Pande husika katika mgogoro huu ambazo ni Serikali na Madaktari wakubali kukaa katika meza moja ya mazungumzo kutafuta mwafaka wa suala hili, wenye lengo la kupata suluhu ya tatizo lililopo, huku kila upande ukiangalia madhara kwa binadamu yanayotokana na mgogoro huu.
 2. Majadiliano yalenge kutatua matatizo ya madaktari kwa upande mmoja, lakini pia yazingatie uwezo wa Serikali kwa upande mwingine. Nia iwe ni kuwawezesha madaktari kadri uwezo wa Serikali unavyoruhusu lakini pia kuwaokoa wagonjwa ambao wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na kukosa tiba.

 1. Madaktari wakubali kurejea kazini haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya watu ambao wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma za tiba, wakati wagonjwa wakiwa si sehemu ya mgogoro uliopo.

 1. Serikali ifute amri zake zote dhidi ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo (hasa ile ya kuwafukuza wasiofika kazini jana Jumatatu Januari 30, 2012) ili kuwezesha mazungumzo kufanyika baina ya pande hizo mbili.

 1. Baada ya makubaliano kufikiwa, iwepo kalenda ya utekelezaji wa makubaliano husika ili kuepusha kutokea kwa mgomo mwingine ambao unaweza kuleta athari kubwa zaidi kwa wananchi.

 1. Baada ya maafikiano kuwapo, usiwepo mpango wowote wa wazi au wa kificho wa kuwaadhibu kwa namna yoyote ile viongozi wa madaktari waliogoma kwani tunaamini kwamba madai yao yalikuwa halali.

 1. Serikali kuanzia sasa ifanye mapitio ya mishahara, maslahi na stahili nyingine za wafanyakazi wote katika sekta ya Umma na kuyaboresha, ili kuepuka kufanya hivyo kwa shinikizo la migomo inayofanywa na watumishi hao kwa makundi.

HITIMISHO
Wakati tukiamini kwamba busara itatumika kuliondoa Taifa letu katika mtanziko uliopo, tuseme wazi kuwa sisi Wahariri tunaamini yafuatayo:

 1. Kwanza tunatambua umuhimu wa kada ya udaktari kwa umma, hivyo kutambua haki yao ya kupata mahitaji muhimu. Ikiwa madaktari hawapati mahitaji muhimu, basi ni dhahiri kwamba hawawezi kutoa huduma kwa wagonjwa ipasavyo.

 1. Pili tunatambua pia ufinyu wa rasilimali za nchi ambazo pengine ndicho kikwazo kwa Serikali kushindwa kuwalipa watumishi wake vizuri au kadri ya madai yao, licha ya kwamba wawakilishi kama wabunge wamepewa nyongeza ya posho za vikao kwa viwango ambavyo vimezua manung'uniko kutoka kwa umma.

 1. Lakini tofauti zozote zilizopo, ziwe za kiutendaji au kiutawala kamwe haziwezi kuondolewa bila pande husika kukubali kukaa na kuzijadili ili kupata mwafaka kwa faida ya Watanzani wote.

Ni matumaini yetu kwamba busara zitatumika ili kuwaokoa Watanzania.


Neville Meena
KATIBU WA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF)

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.