MTANGAZAJI

TAMKO LA BAVICHA KUHUSU KUFUKUZWA KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU

Kwa miaka ya hivi karibuni Vyuo mbalimbali vimekua na tabia ya
kuwafukuza ama kuwasimamisha masomo wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini mwetu kutokana na mashinikizo mbalimbali kutoka kwa viongozi wa kiserikali kwa kisingizio kuwa
wanafunzi hawa wanafanya siasa vyuoni.

Itakumbukuwa kuwa migomo na maandamano ya wanafunzi kwa vyuo vikuu

hapa nchini haijaanza pale mfumo wa vyama vingi uliporuhusiwa kuanza
mwaka 1992 ,bali migomo na maandamano haya yamekuwepo tangu kuanzishwa kwa vyuo hivyo.

Mathalani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa na historia ya migomo

na maandamano ya mara kwa mara tangu kuanzishwa kwake , na hivyo dhana
ya kuwa wanafunzi wanagoma kutokana na misukumo ya kisiasa sio sahihi
hata kidogo bali ni mbinu ya watawala kujaribu kuficha madhaifu yao .

Wanafunzi hawa wamekuwa wakigoma kutokana na serikali ya CCM kuendesha

mambo yake kibabe na kwa dharahu ya hali ya juu ambapo imefanya elimu
kuwa Privilage na si haki kwa watanzania.

Kwa mantiki hiyo basi, kutokutendewa haki kwa wanafunzi hawa na

serikali yao, kukosekana kwa miundombinu bora ya kusoma na kujifunzia,
wanafunzi hawa kunyanyaswa na watawala wa vyuo hivyo, kukosekana kwa
mikopo kwa wakati muafaka, serikali kuingilia uendeshaji wa
vyuo ,serikali kuvunja serikali za wanafunzi bila kutoa sababu za
kimsingi na sababu nyingine mbalimbali ndio chanzo cha vurugu na
migomo vyuoni.

Hivyo basi , kutokana na sababu tajwa hapo juu Baraza la Vijana na

CHADEMA (BAVICHA) tunatamka wazi kuwa kitendo cha Vyuo Vikuu vya Dar
Es Salaam, Dodoma na Muhimbili kuwafukuza wanafunzi kwa ujumla wake
zaidi ya 100 ni kitendo cha uonevu kwa wanafunzi hawa na kamwe
hakivumiliki hata kidogo na haswa ikizingatiwa kuwa ni watoto wa watu
masikini na ambao kimsingi wanajilipia ada wenyewe kwani wanakopa na
baada ya muda watapaswa kulipa fedha hizo.

Kwa nini tunapinga uamuzi huu wa kuwafukuza wanafunzi vyuoni;

1. Ni kinyume na Tamko la Ulimwengu la mwaka 1990 la uhuru wa
kitaaluma (Academic Freedom) ambalo tulisaini mnamo mwezi April tarehe
29 hapa Dar Es Salaam , linasema wazi kuwa ni lazima Vyuo vijiendeshe
kwa uhuru kamili bila kuingiliwa na serikali .


2. Kufukuzwa kwa wanafunzi hawa ni utekelezaji wa Maazimio ya vikao

vya CCM vilivyofanyika na haswa vile vya Halimashauri Kuu ambavyo
vimetoa maelekezo mbalimbali kwa Serikali juu ya kuwachukulia hatua
wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakiikosoa serikali waziwazi ,
na hata wahadhiri ambao wamekuwa wakitumia taaluma zao kwa uwazi na
kusema juu ya mapungufu ya serikali wachukuliwe hatua ya ama kufukuzwa
kazi na au ajira zao kusitishwa. Hivyo hii ni muendelezo wa
utekelezaji wa maamuzi hayo.

3. Kuvunjwa kwa taasisi za wanafunzi na haswa serikali za wanafunzi ,

hii ni kutokana na tangazo la serikali kuhusiana na kanuni za serikali
za wanafunzi lililochapishwa tarehe 12/06/2009 ambalo ni tangazo namba
178 lilivunja rasmi nguvu za serikali za wanafunzi kuanzia na muundo
wake, majukumu yake na hata jina la vyeo husika kwa kufuta rasmi cheo
cha urais kwenye serikali za wanafunzi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa
mara baada ya taasisi hizi kuvunjwa wanafunzi wamekosa chombo cha
kuwasilisha matatizo yao kwa menejimenti za vyuo husika.

4. Wanafunzi waliofukuzwa vyuoni hawajatendewa haki kwani hawajapata

fursa hata ya kusikilizwa na kujitetea mbele ya vyombo husika vya vyuo
hivyo, na wakati huo huo walikuwa wanamadai ya kimsingi kabisa .Hivyo
hii ni kinyume kabisa haki za kimsingi (Natural Justice).

5. Waziri wa Elimu na mafunzo ya Ufundi, Dr Shukuru Kawambwa amekuwa

na tabia ya kuingilia taasisi za elimu ya juu , kwa mfano mnamo tarehe
22/06/2011 aliandika dokezo sabili kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
akitoa maelekezo kwa Bodi ya mikopo kusimamisha mikopo kwa Wanafunzi
kwa ajili ya Mafunzo kwa vitendo hadi hapo uongozi wa UDOM utakapoamua
nani alipwe na nani asilipwe. Pamoja na ukweli kuwa wanafunzi wana
mikataba na bodi ya mikopo bado waziri anaweza kuagiza mikataba hiyo
kuvunjwa na bodi husika. Na hata kitendo cha kuwafukuza wanafunzi hawa
ni muendelezo wa serikali kuingilia vyuo hivi na utendaji wake.

6. BAVICHA , tunapinga na kulaani tamko lililotolewa na Makamu Mkuu wa

Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuwa vijana hawa wasipate fursa yeyote ya
kudahiliwa na vyuo vingine hapa nchini , hii ni kinyume na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kila mtu ana haki ya kujiendeleza
kwa kadiri ya uwezo wake. Hivyo kitendo hiki kamwe hakivumiliki kwa
mtu mmoja kuwa na mamlaka ya kuwanyima wengine fursa ya kupata elimu
kwa sababu ambazo hazielezeki na ni vitisho visivyovumilika hata
kidogo.

Hivyo basi BAVICHA tunaitaka serikali na management zake za vyuo

ziache tabia ya kutibu matokeo au matawi ya matatizo vyuoni humo kwa
kukimbilia kufukuza wanafunzi bali kutatua kiini cha matatizo.

Pia tunawahimiza vijana wote wanaosoma katika vyuo ,

Sekondari ,taasisi mbalimbali za kitaaluma, wanaharakati na wadau wa
elimu na maendeleo ya kweli hapa nchini kuungana pamoja ili kuupinga
utamaduni huu mpya wa kuwanyanyasa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Jambo hili likiachwa ili liendelee bila kuchukua hatua litaathiri sana

taifa kwani watawala wanataka kutengeneza taifa la watu waoga na
wasiokuwa na uwezo wa kuhoji masuala mbalimbali.

Sambamba na haya, kuna wanafunzi wengi waliopaswa kuanza mwaka wa

kwanza wa masomo mwaka huu lakini wameshindwa kufany hivyo kwa kile
kinachoelezwa na bodi ya mikopo kutokua na bajeti ya kuwakopesha.
Wanafunzi hawa wamesharudi makwao.

Majibu haya ya bodi ya mikopo kwa wanafunzi hawa ni kielelezo cha

serikali ya CCM kutokujali wala kuthamini elimu na kwamba anasa na
kutapanya mali za umma ndio kipaumbele chake. Serikali haina fedha za
kusomesha wanafunzi lakini ina fedha za kulipa posho kwa viongozi wake
wachache. Katika hili, BAVICHA tunaitaka serikali itafakari upya swala
la elimu na hata sera ya elimu ya juu hapa nchini

Tamko hili limetolewa na;
 John Heche
Mwenyekiti wa BAVICHA TAIFA.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.