KANALI Muammar Gadhafi (69), aliyekuwa Kiongozi wa Libya hadi miezi ya hivi karibuni, hayupo nasi duniani tena. Dikteta huyu amekufa kifo cha kinyama, cha aibu, cha fedheha na kisichokuwa na staha. Kuna mbwa wengi ambao wamekufa kifo cha heshima kuliko Gadhafi.
Lakini kwa nini mwanadamu, kiumbe wa Mwenyezi Mungu, afe halafu watu washangilie? Nadhani jibu ni lile lilitolewa na mwananchi mmoja katika mahojiano na Redio ya Umma ya Taifa (NPR) ya Marekani, kwamba Gadhafi hakuwa mtu, bali shetani. Ndivyo yalivyo madai ya Walibya wengi wanaoshangilia.
Gadhafi alifanikiwa kuwarubuni wananchi wengi wa Afrika na hata viongozi kiasi cha kudhani kwamba alikuwa mtetezi wa kweli wa Waafrika lakini ukweli wenyewe haukuwa hivi. Kufanikiwa huku kwa Gadhafi kudanganya watu wazima na akili zao kulitokana na ukweli kwamba Waafrika wana hasira na ukoloni, ubeberu na unyonyaji wa mataifa ya Magharibi, hivyo yeyote anayesimama na kujifanya kijogoo dhidi ya mataifa haya ya kibabe anapata wapenzi wengi.
Ni kweli Gadhafi alijitutumua, lakini si kwa sababu aliipenda Afrika; la hasha. Gadhafi alipenda ukubwa na ukuu. Hakuwa na la zaidi, lakini kutokana na umaskini wa mali na akili wa sisi Waafrika, Gadhafi hakupata shida kuturubuni. Naamini alikuwa akikaa chini wakati mwingine anatucheka.
Watu wanaimba kwamba Gadhafi alikuwa na mapenzi na Afrika lakini hawajui kwamba Desemba 1969, mwaka alioshirikiana na vijana wenzake wanajeshi kumpindua Mfalme Idris mwezi Septemba, ndiyo mwaka aliotangaza kwamba Libya, Sudan na Misri zitaungana kuwa taifa moja. Haikuwahi kutokea hivyo; alishindwa.
Ili kuonesha kwamba moyoni mwake alikuwa akiipenda dunia ya Waarabu na siyo ya Waafrika, mwaka 1977 Gadhafi aliibadili jina nchi yake na kuiita Jamhuri ya Kiarabu ya Watu wa Libya.
Kanali Gadhafi aliendelea na juhudi zake za kuyaunganisha mataifa ya Kiarabu chini yake lakini hakufanikiwa, na hatimaye hata kwenye Umoja wa Mataifa ya Kiarabu akaonekana kero, na akaanza kujijengea maadui. Gadhafi alifikia mahali pa kula njama za kumuua mfalme wa Saudi Arabia.
Lakini kwa bahati nchi ya Libya imo kaskazini mwa bara la Afrika, bara la watu waliofanyiwa uonevu kwenye karne ya 19 na 20 na watu wa Magharibi pamoja na Waarabu wa Ghuba. Waafrika ni watu wakarimu ambao wamemudu kuzipokea dini zote zilizoletwa, tamaduni, lugha, na kila kilichowezekana. Gadhafi hakusita kugeukia watu hawa wa Afrika wasio na hiana na mgeni.
Mwarabu mkorofi mwenye hamu na madaraka, mpenda sifa, mwenye akili zilizovurugika, taratibu akaanza kuyachota mataifa ya Afrika kwanza akitumia dini. Alianza kwa kuwa na marafiki kama Idi Amin na hata akafikia kumsaidia kupigana dhidi ya Tanzania. Alipigwa sawa sawa na wanajeshi wake kuuawa takriban 600, wengine kukimbia na waliobaki kutekwa.
Gadhafi akajenga kituo cha mafunzo ya wanamapinduzi duniani mjini Benghazi na kuwafunza wauaji wenzake kama Foday Sanko wa Sierra Leone aliyekuwa akiwaongoza askari wake kukata mikono watoto na kuwabaka akina mama. Mwanafunzi na mfuasi mwingine wa Gadhafi ni Blaise Compaore, Rais wa Burkina Faso aliyemuua Kiongozi Mwanamapinduzi Kapteni Thomas Sankara.
Gadhafi alikuwa na wahitimu wengi kuanzia Chad hadi mataifa ya Afrika Magharibi na hata nchini Uganda ambapo baada ya Amin kupinduliwa na majeshi shupavu ya Tanzania, baadaye alijiingiza kwenye kumsaidia Yoweri Museveni, ili mradi tu aonekane kuwa ni baba wa kila kiongozi barani Afrika. Alikuwa akitoa silaha na fedha nyingi kwa ajili ya mauaji Afrika na hata yeye mwenyewe kuiingiza nchi yake vitani, mathalani dhidi ya Chad.
Muda wote huu Wamarekani walishapata jina la kumwita, “Mbwa Kichaa wa Mashariki ya Kati,” siyo Afrika, hapana, bali Mashariki ya Kati. Alipewa jina hili na rais mbabe wa Marekani, Marehemu Ronald Reagan, mwaka 1986, baada ya ndege za Marekani kuitwanga Libya na kumuua binti wa kambo wa Gadhafi.
Wakati Gadhafi akifanya vituko vyake duniani, alikuwa pia akiendelea kupata umaarufu kama mpigania haki za wanyonge wa Afrika kutokana na kelele zake. Alijihusisha na matukio ya kigaidi yaliyompa sifa za kihuni, na pia aliingiza nchi yake katika vikwazo vya kijeshi na kiuchumi. Hata hivyo, uwingi wa kupindukia wa mafuta uliendelea kuineemesha Libya.
Kutokana na utajiri uliokithiri, na hamu ya Gadhafi kutaka kuonekana kwamba ni kiongozi mwanamapinduzi mzuri, na kwamba anawajali watu wake, ni kweli kwamba aliijenga Libya vema na kutoa huduma za jamii za kutosha kwa watu kuliko taifa jingine lolote la Afrika. Lakini, hii haikuwa zawadi kwa watu; bali walistahili zaidi ya hivi.
Wakati akiwalisha peremende watu wake, Gadhafi aliendelea kujilimbikizia mabilioni ya dola nje ya nchi na hadi sasa bado mataifa makubwa yanazisaka lakini zinazidi dola bilioni 80, yaani zaidi ya mara kumi ya deni lote la Tanzania. Hizi ni fedha za wizi tu, yeye na wanae wa kiume saba, binti mmoja na wake wawili.
Gadhafi alitumia pesa za Walibya kama pesa zake binafsi, na hasa baada ya kutaifisha viwanda vyote vya kuchimba mafuta. Mathalani watoto wake ndio waliokuwa na haki ya kusafirisha mafuta, na wengine walikuwa makamanda wakubwa kwenye majeshi ya Libya huku mmoja akiwa mshauri wa usalama wa taifa. Libya ilikuwa mali ya familia ya Gadhafi ama kwa hakika.
Wakati akifanya yote hayo, watu wa Afrika nao walikuwa wanaanza kugawiwa peremende kama matoto majinga. Gadhafi alikuwa na kawaida ya kugawa misaada na kusambaza miradi ya maendeleo barani Afrika, hata kulipia satelaiti kwa ajili ya nchi za Afrika, kuanzisha shirika la ndege la Afrika na kuzilipia michango kwenye Umoja wa Afrika (AU) nchi zote hohehahe.
Gadhafi pia alikuwa na kawaida ya kujenga nyumba za ibada, misikiti mikubwa, barani kote Afrika kila anapoombwa. Alianzisha pia mchezo wa kitoto wa kuwakusanya machifu wa makabila ya Afrika na kuwapeleka Libya, na kisha kuwafanyia sherehe na kuwapa zawadi kama watoto wa chekechea. Mwisho wake alitaka tu wamwite “Mfalme wa Wafalme.”
Gadhafi alikuwa pia akigawa magari ya kifahari kwa viongozi wa Afrika na hata kuwapa fedha taslimu inapolazimu ili wajisikie huru na wampende kama baba wa Afrika. Alipenda pia kuwaburuza wenzake kwenye vikao vya Afrika, na kuna wakati hawakupenda awe mwenyekiti, hivyo ikalazimu zitumike mbinu za kisanii. Gadhafi ameongoza UA mwaka 2009 baada ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kumaliza muda wake.
Wakati yote haya yakiendelea na Gadhafi akijipatia sifa barani Afrika, nyumbani kwake ilikuwa akiibuka mbaya wake anashughulikiwa haraka na kinyama. Mwaka 1996 mathalani, Gadhafi aliua watu zaidi ya 1,500 kutoka eneo moja baada ya jaribio la kutaka kumpindua kushindwa. Gadhafi alijiona kama Mungu na kwamba yeyote aliyempinga alistahili kufa.
Mwaka 2004 Gadhafi aligundua kuwa dunia ilikuwa inakwenda visivyo sivyo, hivyo akaamua kujisalimisha mbele ya Wamarekani kwa kusema kwamba anaachana na mpango wake wa silaha za maangamizi ya halaiki ya watu. Alikubali pia kuwalipa ndugu wa wahanga wa ndege ya Pan Am aliyoitungua kwenye anga la Uskochi.
Gadhafi pia anadaiwa kuwa alikuwa akishirikiana kwa siri na mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi licha ya kuwa alikuwa akijifanya hadharani kwamba hayapendi mataifa hayo. Alikuwa pia akigharamia kampeni za marais kadhaa, kama wa sasa wa Ufaransa. Alikuwa mtu mchafu, mnafiki, mwongo na aliyejua akili za Waafrika zinavyofanya kazi.
Hatimaye Februari mwaka huu wananchi wake waliibuka na kuandamana mjini Benghazi wakidai haki zao. Gadhafi alitoa amri kwamba wapigwe vibaya na kuuawa. Aliwaita kuwa ni panya na mende na magaidi wanaofaa kufa mara moja. Mwezi Machi Umoja wa Mataifa ukatoa kibali kwa mataifa ya Magharibi kuanza kurusha ndege angani kuzuia majeshi ya Gadhafi yasiende kuwaua watu wake. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho wa Gadhafi.
Baada ya miezi sita, yaani kufikia Agosti, mji wa Tripoli huku ukiwa umechakazwa na mabomu ya NATO, ulianguka mikononi mwa waasi. Mapigano yaliendelea na hatimaye kufikia kwenye mji wa nyumbani kwa Gadhafi wa Sirte. Hatimaye Alhamisi hii alidakwa na wananchi wake na kuuawa kifedhuli.
Inaelezwa kwamba msafara mdogo wa magari madogo kama 15 hivi, ulionwa na ndege ya Tornado ya Uingereza ukitoroka kutoka mjini Sirte. Rubani Mwingireza aliomba msaada kutoka kwenye ndege za mabomu zisizokuwa na rubani za Marekani ambazo zilifika na kuanza kushambulia. Ndege ya Rafale ya Ufaransa nayo ilifika na kuongezea balaa.
Walibya walioona baada ya mashambulizi hayo wanasema magari yalitawanyika na kuteketea kwa moto lakini Gadhafi na walinzi wake walipona ama kujeruhiwa kidogo na kukimbilia kwenye mtaro wa umbo la bomba wa barabarani. Waliingia humo ndani na kujificha hadi watoto wa kihuni wa Libya wenye silaha za bunduki walipokimbilia hapo na kuwakuta.
Walinzi wa Gadhafi waliuawa haraka, na yeye kutolewa huku akiwa hana ubishi na akiuliza: “Jamani, mimi ni kiongozi wenu, kuna shida gani?” Wananchi walijaza na kuanza kumshambulia na kusababisha ghasia kubwa huku watu wakimpiga ngumi, mateke, kwa viatu, kama mwizi. Aliuliza wakati fulani: “Ninyi mnajua baya na zuri ni lipi?”
Picha za Gadhafi wakati anafanyiwa fujo kabla ya kuuawa ni za kushangaza. Alikuwa ameloa damu, amechafuka, ametimuliwa nywele zake, akavuliwa shati wakati fulani, akavutwa suruali. Alikumbana na hali ngumu kabla hajapigwa risasi ya tumbo iliyomuua. Kuna madai kuwa alipigwa risasi ya kichwa pia.
Kwa vyovyote vile, Gadhafi aliuawa kinyama mno. Ingekuwa heri kama angepatikana akiwa hai ili asimame kizimbani kujibu mashitaka ya unyama wake, lakini basi wananchi wenye hasira, watu waliochoka na vita kali ya kuikomboa Libya hawakuwa na muda wa kufikiria kwamba anafaa kuishi kidogo. Waarabu wa Libya walikuwa na hasira.
Ni aibu kwamba watu wasiojua kwa nini Walibya hawa hawakumpenda Gadhafi namna hii, watu kama siye Watanzania, eti tunamlilia Gadhafi. Ni aibu kwa mtu kumlilia muuaji aliyetesa watu na kuwafanya Walibya wote wajinga isipokuwa watoto wake majambazi wa mali ya umma.
Lakini kifo cha Gadhafi kinatufundisha nini Waafrika? Je, hivi hakuna funzo la kuchukua hapo? Kwa hakika lipo. Ngoja nitaje machache.
Mosi, kutumia fedha za nchi kuwapatia huduma wananchi wako, si zawadi kwao bali ni wajibu wako na kama unaona ni mzigo basi acha uongozi. Pili, huwezi kuwatawala watu milele, au hata muda mrefu tu. Lazima siku moja utatoka.
Tatu, tabia ya kuwaweka watoto wa viongozi kwenye madaraka na ulaji wa nchi ni chafu na kwamba siku moja lazima itawatokea puani wahusika. Nne, wananchi wakiamua, hata iweje, kiongozi mbabe atatoka tu. Nchini Libya ilifikia mahali wanajeshi na polisi ndio waliokuwa makamanda wa kumtwanga bosi wao wa zamani. Nchi ni za wananchi.
Tano, na mwisho wa leo: Binadamu aliyezaliwa na mwanamke ni binadamu, na kwamba uwezo wake una kikomo. Gadhafi alifikia mahali akadhani kuwa yeye ni Mungu wa Afrika, lakini leo maiti yake imelazwa kwenye godoro na vijana wa Libya wanaichezea na kuipiga picha.
Gadhafi anaadhirika na waumini wenzake wa Kiislamu wamesahau hata maadili ya dini kwamba alipaswa kufunikwa na kufichwa na kuzikwa mapema, yaani kabla ya jua halijazama siku ya pili yake, Ijumaa iliyopita. Gadhafi ameacha majonzi kwa familia yake ingawa tayari mwanae mmoja alishauawa awali pamoja na wajukuu zake, na mwingine aliuawa Alhamisi pia katika tukio tofauti.
Kifo cha kinyama cha Gadhafi kiwe funzo kwa viongozi wa Afrika; kwamba nchi hizi wanazozitawala ni za wananchi na wala si zao. Kama wananchi wao hawataweza kuwatoa, basi dunia ya kibabe itawasaidia kama Waafrika walivyowasaidia wazungu kumpiga Adolf Hitler kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
TATHMINI KUTOKA WASHINGTON DC
Na Mobhare Matinyi, Majira Jumapili, Oktoba 23, 2011.
Post a Comment