MTANGAZAJI

DANNY MWAKITELEKO KAFARIKI DUNIA-TUNAJIFUNZA NINI?

Marehemu Danny Mwakiteleko, kulia akiwa mjini Arusha hivi karibuni akihudhuria Mkutano Mkuu wa Wahariri Tanzania, kushoto ni baadhi ya wahariri wenzake kutoka vyombo mbalimbali vya habari.(Picha na THE HABARI)

                                       Gari la Marehemu Danny Mwakiteleko baada ya ajali

Wana habari wa Tanzania, na waungwana wengine wote,
Huu ni msiba mwingine mkubwa kwetu. Kifo cha Danny Mwakiteleko, kama vilivyo vifo vingine vya ajali, ni cha kustua mno na kwa kweli kinasikitisha. Ajali aliyoipata ilikuwa ya kutisha na ilipofikia hatua ya kufanyiwa operesheni ya kichwa kwenye hospitali yetu hii ya Muhimbili tunayoijua, kwa kweli ilitisha kupita kiasi. Pole kwa wanafamilia yake, wafanyakazi wenzake wa New Habari Corporation, wanahabari wenzake, ndugu, jamaa na marafiki. Huyu bwana niliwahi kufanya naye kazi miaka mingi huko nyuma, na ninakumbuka mwaka jana nilipokuwa nyumbani nilimpitia ofisini na tukaenda kupata ugali mchana pamoja; ni vigumu kuamini kwamba haiwezekani tena kuwasiliana naye. Basi, hatuna la kufanya katika hatua hii kwa ajili ya Danny zaidi ya kutoa pole kwa wafiwa na kumwomba Mungu awape faraja.

Lakini baada ya masikitiko, kuna haja ya Watanzania kujiuliza iwapo sasa tumekubali kabisa kwamba ajali zitutawale. Hii hali si nzuri -- ya kukubali kila siku kwamba - Kila mtu ana siku yake; ni mapenzi ya Mungu; siku ikifika huwezi kuikwepa; ajali haina kinga, ...... na maneno mengine ya kishirikina na kiroho, na hata kisiasa kama: "Tusilaumu, wote tutakufa." Hapana.

Wazungu husema kwamba Mwafrika ni mtu anayesukumia kila kitu kwa Mungu kwa sababu anaamini yeye hawezi kurekebisha hali inayomkabili, mathalani, umeme ni tatizo Tanzania kwa sababu Mungu hakuleta mvua; lakini hatusemi kwamba ni Mungu huyo huyo aliyetupa njia lukuki mbadala na akili na muda. Sasa wengi wetu, kuanzia rais hadi wauze nyanya, tunalalamikia kudra za Mwenyezi Mungu. Ndivyo ilivyo kwenye ajali - tunaamini kwamba ni mapenzi ya Mungu lori lisilokuwa na taa wala kiakisi mwanga kusimama barabarani (siyo pembeni) usiku wa giza nene na kisha mwendesha gari kuliingia na kupoteza maisha - - Watanzania tunaamini kuwa ni "mapenzi ya Mungu." Dah!

Wamarekani baada ya kuona ajali ni tatizo mwaka 1967 walianzisha Bodi ya Taifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) licha ya kuwa wana serikali za mitaa, polisi, na mamlaka za leseni zinazoangalia usalama huo huo. Mathalani, ingawa wana Mamlaka ya Usafiri wa Anga (FAA), lakini bado Bodi hii inafanya uchunguzi kila inapotokea ajali ya ndege. Bodi hii huchunguza vyanzo vya ajali za barabarani, relini, majini, angani, na na kwenye mabomba ya mafuta, kisha kutoa ushauri/amri/uamuzi/kuongoza sera, n.k. ili kulinda maisha ya watu.

Sisi nasi tuna Mamkala ya Usafiri wa Anga, na pia tuna Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), na polisi yetu; lakini vitu hivi havikidhi mahitaji mwa jinsi vilivyo. Je, kwa nini tusivibadilishe muundo wake, utaalam wake, na uwezo wake, au ikibidi kuunda kingine kama walivyofanya wenzetu? Juzi juzi hapa Marekani jimboni Virginia, basi moja la watalii lilipinduka asubuhi na kuua watu wanne baada ya dereva kusinzia na kuacha njia. Ilipofika saa saba mchana kampuni ya mabasi hayo ilifungwa Marekani nzima na NTSB kwa tuhuma za kudharau kanuni za usalama. Sisi ikitokea ajali, kwa mfano wiki hii mabasi mawili yamewaka moto katika ajali ambazo ukielezwa hata maelezo hayaingii akilini, lakini viongozi wetu na sisi tutaishia kusema: "Kazi ya Mungu." Kwa Marekani watu wasingelala kwa mabasi mawili kupata ajali za namna hii.

Tuna uwezo wa kufanya kitu ili kupunguza ajali hizi, tukianzia na kukubali kwamba kuna tatizo kwenye seti nzima ya suala la usalama barabarani, yaani barabara zetu, vyombo vyetu, madereva, abiria, watembea kwa miguu, polisi, serikali, n.k. Hii ya kumsukumia Mungu kila kitu inaishia kuthibitisha maneno ya Wazungu kwamba Waafrika ni watu bure kabisa - - wanaamini matatizo yao lazima yatatuliwa na Mungu.

Tanzania bila ajali inawezekana, lakini kwanza tuanze na Tanzania bila ukuku wa mawazo.

Mobhare Matinyi-USA

2 comments

wan said...

oh my GOD...

Anonymous said...

Matatizo:
1.Hulka za watumiaji wa barabara: (madereva na abiria yaani wasafiri wenyewe...)
2. Ubora wa miundombinu (jinsi barabara zilivyoandaliwa...(barabara zetu hazina ubora wa kuhimili mwendokasi ambao baadhi ya madereva hulazimisha)

3. Imani zetu... huwa hatujaamini kuwa maisha ni ya muhimu.
4. Ukosefu wa elimu ya vyombo vya moto...na thamani tunayopatia vyombo hivi ukilinganisha na maisha ya wanadamu.
5. Mengineyo.

Mtazamo News . Powered by Blogger.