MTANGAZAJI

MAHOJIANO YA BBC NA RAIS WA TANZANIA MHESHIMIWA JAKAYA KIKWETE KUHUSU TATIZO LA UMEME NCHINI

 
Rais wa Tanzania Mhe Jakaya Kikwete ametoa ufafanuzi wa tatizo la umeme katika mahojiano maalum na mwandishi wa BBC, Omar Mutasa yaliyofanyika nchini Afrika Kusini, kwanza Mutasa alitaka kujua, pamoja na kutafuta wawekezaji ambao kimsingi watahitaji nishati ya umeme ya uhakika, kwa nini tatizo la umeme halijapatiwa ufumbuzi?

BBC: Suala la umeme mheshimiwa Rais Kikwete unaweza kulizungumzia vipi?
KIKWETE
: Tatizo la umeme kimsingi, ni kwamba ni tatizo la ukame tu, kwa sababu mabwawa yetu ya kuzalisha umeme, yanayotoa umeme karibu megawati 600, sasa hivi yanatoa... yanatoa umeme kidogo sana, maji ni pungufu, na ndio maana kuna tatizo hilo!

BBC: Lakini mheshimiwa hili suala sio la leo, wala si la jana, limekuwepo kwa muda mrefu, kwanini serikali haina njia mbadala ya kuweza kutatua suala hili? Tanzania ina raslimali nyingi Mheshimiwa Kikwete!

KIKWETE: Kwanza, la kwanza serikali haina uwezo wa kufanya mvua inyeshe, unajua hilo, eeh kwa sababu (kicheko) kwa sababu serikali ingekuwa na uwezo wa kufanya mvua inyeshe mabwawa yale yangejaa, kweli Tanzania inazo raslimali za kutosha na kwa kipindi hiki toka tumepata uhuru... Sisi tumeingia tumekuta tatizo la ukame, na mwaka 2007 tukapata matatizo ya kwanza, baada ya pale tukafanya uamuzi kwamba sasa tuanze kuwekeza katika vyanzo vingine, tuongeze uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vya kutumia gesi asilia, twende kwenye makaa ya mawe, vyanzo vya gesi asilia tayari tuna mtambo pale Ubungo eeh, toka mwaka 2009 mpaka sasa tumeongeza megawati 145, na itakapofika Desemba tutakuwa tumeongeza megawati 160 nyingine, tutakuwa tumeongeza megawati 300, siyo kidogo!


BBC: Mheshimiwa Kikwete, mmoja kati ya Wabunge bwana John Mnyika ambaye ni Mbunge wa upinzani, ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati, amekuwa akilalamika na akisema kwamba, amewahi kusema kwamba hili tatizo ni tatizo linawahusu Watanzania wote, akisema kwamba mje pamoja na kuona vipi mtatatua tatizo hili, na sasa hivi bungeni wamesimamisha muswada wa kutoa bajeti ya Wizara ya Nishati ya Tanzania. Wewe unayachukulia vipi matamshi kama haya toka kwa Wabunge?

KIKWETE: Mimi nasema hivi, yeye si Mbunge? Atoe maarifa yake tu, anayo maarifa gani? Anapendekeza kitu gani? Kwa sababu toka uhuru mabwawa tuliyotengeneza ni Kidatu megawati 200, mtera megawati 80, Kihansi 185 mimi nilipokuwa Waziri wa Nishati, pale Pangani tumeongeza! Sasa ufikirie, toka uhuru tumeweza kuzalisha umeme karibu megawati 600, lakini toka 2009 mpaka Desemba mwaka huu tutakuwa tumeongeza megawati 300, ni jitihada kubwa, mimi nasema usipozitambua hizo ni kwamba wewe mwenyewe sio mkweli, sio mkweli, eeh sasa ni hivi unajua hii mitambo ya umeme, si mitambo unakwenda kuinunua kama jaketi lako hili, ni kwamba ukitaka mitambo ya umeme lazima uweke oda wakutengenezee, huu mtambo itakapofika mwaka huu Desemba utakuwa umekamilika, oda tuliweka Juni mwaka wa jana 2010, inachukua muda huo kutengeneza. Sasa ingekuwa tunakwenda kutafuta mitumba, mitumba ya mitambo tu ya kununua iko mingi kweli, lakini hatuwezi kufanya hivyo, masema hivi kitu kikubwa ni kufanya subira, tumefanya jitihada kubwa, na hiyo ni lazima watu watambue kwamba tumefanya jitihada kubwa, katika miaka hii, toka 2009 mpaka sasa hivi 2011 Desemba tutakuwa tumeongeza megawati 300, ukilinganisha na megawati 600 tulizoziongeza katika miaka yote, nasema lazima watu watambue. Sasa kama kuna mtu ana maarifa ya haraka zaidi, nasema mtu atoe maarifa hayo, na sisi kama yapo tutayafanyia kazi tu.


BBC: Kuna njia kama umeme wa jua, na kama umeme wa kutokea chini kwenye ardhi, wa mvuke, kwanini serikali haitafuti njia mbadala za kualisha umeme kwa njia hizo......?

KIKWETE:  Sikiliza bwana... Nasema hivi, hata umeme wa jua lazima ujenge, hata umeme wa mvuke lazima ujenge, sio kitu cha mwezi mmoja, eeh lazima na huo ndio ukweli wenyewe, na wakati mwingine na nyinyi mjifunze haya mambo ya kitaalamu kulikoni kuuliza tu hivi, unajua ungekuwa na wewe unauliza kwa hoja, kwamba unajua hiki kitu hiki, ungekuwa umeme wa jua miezi miwili tu upo, ungeweza kufanya hivyo. Sisi sasa hivi, kwa mfano sasa hivi tunajiandaa kuzalisha umeme wa kutumia (hew... )upepo pale Singida, tuna mwaka wa tatu sasa toka tuanze na Wakorea Kusini, umeme haujakuwepo, kwa hiyo nasema hayo ni maelezo rahisi, eeh unasema mbona jua lipo, si katengeneze umeme wa jua kama jua kwa sababu lipo (kicheko).


BBC: Watanzania wamekuwa wakisema kwamba, mwisho kabisa kwamba Tanesco ingebinafsishwa ili wapate makampuni mengine.....

KIKWETE: Kwani... Kwani... Kwani ukibinafsisha kesho utapata mitambo kesho?  Hilo wala.. wala sio jambo, nasema hivi, ni vizuri kuelewa tu, kwanza umeme nasema, tatizo letu la msingi ni maji kukauka kwenye mabwawa, maji yasingekauka kwenye mabwawa tatizo hili halipo, na maji yanakauka kwenye mabwawa kwa sababu ya ukame, hakuna mtu ana uwezo wa kuzuia ukame usiwepo, na sasa hiki ndicho kiini cha tatizo, sasa nasema sisi jitihada tuliyofanya ni ya kupunguza kutegemea mno umeme wa kutegemea nguvu ya maji, na toka 2009 mpaka Desemba tutakuwa tumeongeza megawati 305, hiyo ni jitihada kubwa, eeh jitihada kubwa, nasema ni vizuri mkaitambua jitihada hiyo, kulikoni kusema kitu tu, kama una jambo rahisi tuambie tu.


BBC: Nashukuru sana Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nakutakia kila la kheti katika safari yako hapa Afrika Kusini!

KIKWETE: Kwa heri!

BBC: Asante sana.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.