MTANGAZAJI

TUNATUMIAJE VIPAJI VYA WAJASIRIAMALI WETU WATANZANIA?

Tanzania imeingia katika mhamo wa ruwaza (paradigm shift) ambapo mkazo umewekwa katika ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa njia ya kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara wadogo kusimamia uchumi wa nchi. Mhamo huu umeanza tangu kuingia kwa sera za mfumo huru wa biashara (liberal economic policies) katikati ya miaka ya 1980 ambapo serikali ilianza kujiondoa katika kusimamia biashara. Kazi hii ilifanyika kupitia tawala za awamu ya pili na ya tatu zilizoongozwa na marais wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.

Tangu awamu ya nne kuingia madarakani, mfumo wa uzalishaji umefanyiwa marekebisho makubwa na sasa tumeingia katika mkakati wa “KILIMO KWANZA” ambapo mojawapo ya maswala makubwa ni kuingiza somo la kilimo na ujasiriamali katika mfumo rasmi wa elimu kama inavyolezwa katika kitabu cha “KILIMO KWANZA” ukurasa wa 23 na 24 kilichozinduliwa Juni 2-3 katika hoteli ya Kunduchi beach na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Kufuatia hatua hiyo, kurunzi imefanya utafiti wa kina kuhusu maana, historia, changamoto na fursa zilizopo katika ujasiriamali na namna ambavyo somo la ujasiriamali linaweza kuingizwa katika mfumo wetu wa elimu ili liweze kukabiliana na changamoto la kuwatoa wasomi watanzania katika adha ya kuwa watafuta ajira (job seekers) na kuwafanya wawe ni watengeneza ajira (job creators). Hebu fuatana nami na, nina hakika kwamba mwishoni mwa makala hii, utakuwa katika nafasi nzuri ya kushiriki katika mkakati huu wa kuikomboa Tanzania kutoka kwenye makucha ya ujinga, maradhi na umaskini kwa njia hii ya makakti wa “KILIMO KWANZA”.

Neno “ujasiriamali” hutafsiriwa kama mchakato mzima wa kutambua fursa za kiuchumi, uzalishaji au mbinu mpya ya utoaji huduma na kutumia raslimali kama ardhi, nguvukazi, mtaji, teknolojia n.k. ili kukidhi mahitaji ya kiuchumi au kibiashara kwa lengo la kupata faida na wakati uo huo kuwa tayari kupata hasara inayoweza kujitokeza.

Watu wengi wamekuwa wakilichanganya sana neno hili na neno “biashara” ambalo lina maana ya shughuli yoyote halali inayohusisha uzalishaji mali, uuzaji bidhaa na utoaji wa huduma kwa lengo la kupata faida.

Kwa mujibu wa tafsiri ya Mariott ya mwaka 2001, “mjasiriamali” ni mtu anayeratibu na kuendesha biashara kwa ubunifu kwa lengo la kupata faida huku akiwa tayari kukabiliana na hasara yoyote itakayojitokeza.

Kwa ufupi tu ni kwamba mjasiriamali huvumbua vitu hata kama ni kwa kupata hasara na matokeo ya uvumbuzi huo ni upatikanaji wa bidhaa mpya ambayo yeye au mfanyabiashara mwingine huizalisha kwa wingi, kuiuza na kupata faida.

Msomi hufanya utafiti wa namna ya kuweka kumbukumbu sahihi za ubunifu, kuuboresha na kuuweka katika mifumo rasmi ya kanuni za kisayansi ili utumike mahali pengine kwa wakati huo na katika vizazi vijavyo. Msomi na mfanyabiashara ni matunda ya mjasiriamali. Kwa maana hiyo ni kwamba, hakuna mahali utakapotaja neno “ujasiriamali” ukaacha kuwataja wafanyabiashara na wasomi. Ni watu wanaotegemeana sana.

Katika hao watu watatu, serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba kazi za wajasiriamali zinalindwa sana ili kuhakikisha kwamba hakuna maharamia wa kazi za watu (pirates) wanaozipora na kumwacha mjasiriamali na hasara zake. Inapotokea kazi ya mjasiriamali imeandikiwa taarifa za kitafiti, basi ilindwe na chama cha hakimiliki cha Tanzania (Copyright Society of Tanzania - COSOTA) ili wajasiriamali wengine wakubali kutoa taarifa zitakazowezesha kazi zao kuandikwa kisayansi kamainavyofanyika katika nchi nyingi zilizoendelea
Wajasiriamali waliowahi kujiolea hata kupoteza maisha au heshima yao ni wengi na ndio wanaofanya nchi zao kung’ara kiuchumi mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa.


Leo hakuna mwanadamu anayeweza kusema hajawahi kuguswa na matokeo ya kazi za wajasiriamali. Teknolojia ya hali ya juu tunayoitumia leo ni matokeo ya kazi za wajasiriamali. Mifumo ya kompyuta na tovuti tuzitumiazo leo ni matokeo ya mjasiriamali Bill Gates ambaye, kutokana na kutumia muda wake mwingi katika ubunifu alipata hasara ya kupoteza masomo chuo kikuu. Leo teknolojia hii ndiyo inayoendesha dunia.

Ndege zinazopaa hewani ziligunduliwa na mjasiriamali ambaye, katika jaribio lake la kwanza la kurusha ndege, alipata hasara ya kupoteza uhai wake.

Yule mwanasayansi wa kwanza aliyesema dunia ni mviringo na huzunguka jua alionekana ni mwasi na aliadhibiwa na kanisa la wakati huo. Yule mvumbuzi wa teknolojia ya elektroniki Albert Einsten aliwahi kutamka kwamba mada inaweza kuumbwa au kugawanyika.

Huyu alipata hasara ya kupoteza masomo yake chuo kikuu kwa kuonekana mtu mwenye mawazo yanayopingana na wafikiriaji wakubwa wa wakati huo kama akina Isaac Newton.Kwa mujibu wa jarida la wikipedia linalotolewa katika tovuti kupitia www.wikipedia.org/wiki/king_C._Gillette, Mmarekani ajulikanaye kwa jina la King Gillette ndiye mgunduzi na mjasiriamali wa nyembe za kawaida tunazozifahamu na kuzitumia leo.

Mtu huyu alifanya ugunduzi huo mwishoni mwa miaka ya 1900 akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kuchoshwa na visu butu vilivyokuwa vikitumika kunyolea kwa wakati huo ambavyo vilikuwa na makali upande mmoja na vilihitaji kunolewa ili kuweza kunyoa nywele na ndevu.

Gillette alikuwa na ndoto ya kuwa na wembe mwembamba wenye makali pande zote mbili na ambao mtumiaji angeutumia na kuutupa pale anapoona umekuwa butu.

Akiwa na wazo hili, alikwenda katika taasisi ya teknolojia ya Massachussetes ya Marekani ili kupata wataalam watakaoweza kumtengenezea wembe huo. Alijiunga na mbia mmoja ambapo kwa pamoja walitumia miaka mitano kubuni mashine itakayoweza kufanya kazi hiyo. Mwanzoni walilazimika kuuza nyembe hizo kwa bei ya chini kuliko gharama za uzalishaji na walikabiliana na tatizo hilo kwa kuzalisha nyembe nyingi sana ili bei ya wembe mmoja ishuke chini. Baadaye aliunda kampuni ya “Gillete Safety Razors” ambayo ilikuja kumpa utajiri mkubwa.

Katika kutafuta soko la nyembe zao, Gillette alikuwa tayari kuwapa watu bure visu vyake vya zamani ili waamini kuwa visu hivyo wanavyotumia havina thamani kuliko nyembe zinazouzwa alizogundua.

Wengi wa wanasayansi wavumbuzi wengi ambao kurunzi imewamulika leo tayari wametangulia mbele za haki japo uvumbuzi na nadharia zao bado zi hai na tunazitumia hadi wa leo. Mtu ambaye kwa leo bado tunamwona ni mvumbuzi wa mifumo ya kompyuta na tovuti Bill Gates. Huyu kwa sasa ni mtu tajiri na kazi zake zinalindwa sana na serikali ya Marekani.

Licha ya hapo, kuna watafiti wengi sana walioandika habari za Bill Gates na kazi zake na wameweka kazi zao katika maandishi yanayotumika duniani kote katika shule na vyuo ngazi zote za elimu. Leo kompyuta zinazalishwa na kuuzwa duniani kote na wafanyabiashara. Hakuna mfanyabiashara yeyote leo anayeweza kudiriki kutamka kwamba anauza bidhaa ambayo haijapitia katika matokeo ya ujasiriamali wa Bill Gates.

Kurunzi haina shaka kwamba mifano iliyotajwa hapo juu ndio hasa tunayotakiwa kuitumia sisi watanzania ili tujikomboe na lindi la umaskini mbaya tulio nao. Tanzania ina wajasiriamali wengi sana ambao wengine wanapata misukosuko ile ile waliyopata wajasiriamali wa zamani.

Tofauti yake tu ipo kwamba hawa watu hawana uhusiano wa moja kwa moja na taasisi za elimu na utafiti kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zao zitumike sasa na vizazi vijavyo. Kwa sababu ya kuogopa maharamia wa kazi za watu, wajasiriamali wetu wanafanya kazi kwa kanuni zile zile za uchawi ambapo mtu hugundua teknolojia yake na kuibakiza siri hadi afe.

Inapotokea kwamba teknolojia yake imefahamika kwa watu na yeye mwenyewe kufaidika, mjasiriamali huyu hutafutiwa kila mbinu na kupigwa vita yumkini hata na watawala wa nchi pamoja na vyombo vya kutunga na kusimamia sheria.

Kwa mfano tuna mjasiriamali Reginald Mengi. Huyu ni mtaalam aliyesomea ukaguzi wa maheabu (audit). Yeye aliacha kazi za ajira katika miaka ya 1980 na kutumia chumba alichokuwa akilala kama kiwanda cha kuunganisha kalamu za wino.

Yumkini kwa sababu Benki zetu zina ukiritimba unaozuia wajasiriamali wadogo kujiendeleza, mjasiriamali huyu alipata mkopo kutoka Kenya ili kupanua wigo wa uzalishaji na biashara yake ya kalamu. Biashara yake ilikua na kuzaa makampuni ya IPP tunayoyaona leo.

Tuna wajasiriamali wengine kama akina Joseph Mlangila Mfugale ambaye alianza na kazi za ufundi seremala kule kijijini kwao Kihanga mkoani Iringa. Huyu alianza na mtaji wa shilingi mia nane tu. Leo anamiliki hoteli ya peacock iliyopo katikati ya jiji la maraha la Dar es salaam.

Wajasiriamali wengine ni akina Saidi Bakhresa walioanza na biashara ndogondogo na leo wanamiliki viwanda, akina James Shigongo ambao walianza katika changamoto nyingi sana na leo wanamiliki vyombo vya habari na biashara zingine.

Kurunzi imemulika maisha ya wajasiriamali wengi sana hapa nchini lakini nafasi ya kuwaandika kwenye makala hii na wasifu wao haitoshi. Sidhani kama kuna mtu aliyewahi kuwauliza siri za mafanikio yao kwa nia ya kuwapatia ari watanzania wengine kuingia katika ujasiriamali.

Kama kurunzi ilivyomulika hapo juu, watu hawa wanakumbana na changamoto nyingi sana hadi leo. Kituo cha uwekezaji (TIC) kimejikita kupita kiasi katika kuwahudumia wawekezaji kutoka nje badala ya kuwaendeleza wajasiriamali tulio nao hapa nchini. Utakuta kituo hiki kikimbizana na makaratasi na kuhakikisha kwamba wawekezaji wa kigeni wanapata hatimiliki na misamaha ya kodi haraka haraka na kuanza kufanya biashara kwa faida kubwa kupindukia.

Wakati huo, wengi wa wawekezaji watanzania wanahajihangaikia wenyewe huku wakipambana na vikwazo vya kila aina. Kama kuna watu walio karibu nao sana ni watu wa mamlaka ya mapato (TRA) ambao huwabana kulipa kodi tu pale wanapoona wamejihangaikia na kupata faida. Matokeo ya hali hii tumeanza kuyaona kwani baadhi ya hao wawekezaji wameonekana ni matapeli au watu wasio na ujuzi na kazi zao wala uchungu na nchi yetu.

Matokeo yake wanatumia taaluma na nguvukazi za watanzania katika kuhamisha raslimali tulizo nazo kwa faida yao na mataifa wanakotoka.

Tumefikia mahali ambapo sasa TIC, kwa kushirikiana na taasisi za elimu na utafiti kuwafanyia utafiti watu hawa wajasiriamali wa kitanzania ili vitabu viandikwe juu yao na kufanya kizazi kinachochipuka leo kuvitumia katika mfumo wa elimu na baadaye tukaibuka na wajasiriamali waliosoma na kubobea.

Ili nchi yetu iweze kuendelea, inatakiwa kuelekeza zaidi macho yake katika kuwaendeleza vijana wetu ili wawe wajasiriamali na wasimamizi wa uchumi wetu. Haitoshi tu kuzalisha watafuta kazi (job seekers). Tumefikia sasa mahali ambapo mfumo wetu wa elimu unatakiwa kuzalisha watengeneza kazi (job creators). Wahenga wetu walisema mcheza kwao hutuzwa na kwamba tusiache mbachao kwa msala upitao. Busara hii ina maana leo kuliko kipindi ilipokuwa inatamkwa na kuandikwa.

Mwandishi wa makala hii ni mmiliki wa shule na mshauri wa kujitegemea katika maswala ya usimamizi wa elimu. Pia ni katibu mkuu wa chama cha wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali (TAMONGSCO) na ni mjumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC). Anapatikana kwa namba 0715/54/84-316570 au baruapepe tamongsco@yahoo.com

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.