GHARAMA ZA MAISHA CHANZO CHA VIJANA WAHAMIAJI KUISHI BILA NDOA
Miongoni mwa vijana wahamiaji kutoka Afrika Mashariki wanaoishi Marekani hukutana na mazingira mapya ya kiuchumi, kijamii na kihisia ambayo mara nyingi huathiri namna wanavyoanzisha na kuendeleza mahusiano.
Moja ya mwenendo unaoonekana ni kuishi pamoja bila ndoa, jambo ambalo limekuwa likikua kwa kasi katika jamii ya Marekani. Sababu kubwa inayochangia hali hii ni gharama za maisha, hasa kodi ya nyumba.
Kwa mujibu wa ripoti ya Apartment List ya mwaka 2026, kodi ya wastani nchini Marekani imefikia dola 1,645 kwa mwezi, ikiwa imeongezeka kwa asilimia 3.6 ndani ya mwaka mmoja. Katika miji mikubwa ikiwemo San Francisco, kodi imepanda hadi dola 4,401 kwa mwezi, ongezeko la dola 148 ndani ya mwezi mmoja. Kwa wahamiaji wanaoanza maisha kwa kazi za kuanzia, kuishi pamoja kunapunguza mzigo wa kodi, bili na chakula, hivyo kuwa mkakati wa kiuchumi unaowezesha kuhimili gharama za maisha.
Mbali na gharama za makazi, shinikizo la kiuchumi pia linachangia kwa kiasi kikubwa. Wahamiaji wengi huanza kazi za muda mfupi au zenye kipato cha chini, na ripoti za soko la ajira katika miaka ya karibuni kumeongeza ushindani na kupunguza nafasi za kazi za kuanzia. Hii ina maana vijana wengi kutoka Afrika Mashariki hulazimika kugawana gharama za maisha ili kuokoa pesa kwa ajili ya masomo, uhamiaji au kujijenga kiuchumi.
Changamoto za kihisia na kijamii zinazoambatana na uhamiaji huongeza uwezekano wa kuishi na mwenza bila ndoa. Utafiti wa Kampuni ya Bima ya Afya, Cigna wa mwaka 2024 unaonyesha kuwa asilimia 42 ya Wamarekani huhisi upweke angalau mara moja kwa juma, na upweke huwa mkubwa zaidi kwa watu wanaoishi peke yao.
Kwa wahamiaji, upweke huongezeka kutokana na kukosa familia karibu, tofauti za lugha na utamaduni, na msongo wa mawazo unaotokana na kujenga maisha upya ughaibuni. Ripoti ya Taasisi ya Utafiti wa Sera za Uhamiaji (MPI) inaonyesha kuwa asilimia 70 ya wahamiaji wenye umri wa miaka 18–34 huripoti changamoto za lugha zinazoathiri afya ya akili, na asilimia 29 huripoti dalili za msongo wa mawazo au wasiwasi. Katika mazingira haya, kuishi na mwenza kunatoa utulivu wa kihisia, msaada wa karibu na hisia ya usalama.
Ushawishi wa utamaduni wa Marekani pia una nafasi kubwa. Marekani ni jamii inayokubali kuishi pamoja bila ndoa, na takwimu za Ofisi ya Sensa ya Marekani za 2024 zinaonyesha kuwa asilimia 59 ya Wamarekani wenye umri wa miaka 18–44 wamewahi kuishi na mpenzi bila ndoa, huku asilimia 75 ya wanandoa huanza kwa kuishi pamoja kabla ya ndoa.
Kwa wahamiaji vijana, kuingia katika jamii inayokubali kuishi pamoja bila ndoa kunawafanya waone tabia hii kama sehemu ya maisha ya kawaida. Zaidi ya hapo, gharama za kufunga ndoa Marekani ni kubwa kiasi kwamba vijana wengi huchelewa kufunga ndoa. Utafiti wa Taasisi ya Utafiti na Mipango ya Harusi Marekani The Knot wa mwaka 2026, unaonyesha kuwa gharama ya wastani ya harusi ni dola 34,200, na katika miji mikubwa ikiwemo New York inaweza kufikia kati ya dola 55,000 hadi 75,000. Kwa wahamiaji wanaojijenga kiuchumi, kuishi pamoja bila ndoa huwa chaguo rahisi na la muda.
Kizazi kipya cha vijana nchini Marekani, hususan Millennials na Gen Z, kina mtazamo tofauti kuhusu ndoa na mahusiano. Utafiti wa taasisi ya Pew unaonyesha kuwa asilimia 68 ya Wamarekani wanaona kuishi pamoja bila ndoa kama jambo linalokubalika kimaadili, na asilimia 53 ya Millennials wanaamini kuwa kuishi pamoja ni njia nzuri ya kupima uhusiano kabla ya ndoa.
Hali hii inaathiri pia wahamiaji vijana, ambao huiga mitazamo ya kizazi wanachokutana nacho. Kwa ujumla, sababu za vijana wahamiaji kutoka Afrika Mashariki kuishi pamoja bila ndoa nchini Marekani zinahusisha gharama za maisha zinazopanda, shinikizo la kiuchumi, upweke wa uhamiaji, changamoto za lugha na afya ya akili, utamaduni wa Marekani unaokubali kuishi pamoja bila ndoa, gharama kubwa za harusi na mitazamo ya kizazi kipya kuhusu mahusiano.

.png)
Post a Comment