MTANGAZAJI

KONFERENSI YATOA TAMKO LA HAKI YA WAPIGA KURA MAREKANI.

 


Konferensi ya Kusini ya Kati ya Waadventista wa Sabato nchini Marekani imetoa tamko linalothibitisha haki za kupiga kura, utu wa binadamu, na ushiriki wa kidemokrasia katikati ya wasiwasi kuhusu maamuzi ya kisheria na juhudi zinazoathiri upatikanaji wa kupiga kura, upangaji upya wa maeneo ya uchaguzi, na uwakilishi kote Kusini mwa Marekani. Tamko hilo lililoandikwa Mei 19, limechapishwa kwenye tovuti na ukurasa rasmi wa mtandao wa Facebook wa Konferensi hiyo Mei 25, mwaka huu.

Konferensi hiyo, inayojumuisha Alabama, Kentucky, Mississippi, Tennessee, na sehemu ya Florida iliyoko magharibi mwa Mto Apalachicola, tamko lake linaeleza  uhusiano wa kina wa eneo hilo lenye wamarekani weusi na mapambano ya kihistoria ya haki za kiraia na upatikanaji sawa wa sanduku la kura. Uongozi wa Konferensi unaeleza kuwa washiriki wengi wana kumbukumbu binafsi na za kizazi kuhusu dhabihu zilizotolewa ili kuhakikisha haki za kupiga kura.

Ingawa tamko hilo linabaishisha kwamba Kanisa la Waadventista wa Sabato  haliungi mkono vyama vya kisiasa wala wagombea, linawasilisha  michakato ya kupiga kura inayopatikana kwa wote, uchaguzi huru na wa haki, na uwakilishi wa usawa kama masuala yanayohusiana na haki, usawa, na maadili ya kibiblia. 

Konferensi hiyo iliwahimiza raia wenye sifa za kupiga kura kubaki na taarifa sahihi, kushiriki kikamilifu, na kujitolea kwa ushiriki wa amani na uwajibikaji katika mchakato wa kidemokrasia.

Konferensi ya Kusini ya Kati ya  Kanisa la Waadventista wa Sabato ni moja ya konferensi kubwa za kikanda za Waadventista  Kusini mwa Marekani. Kufikia mwaka 2025, Konferensi hiyo ina idadi ya  waumini takribani 30,369 na makanisa 143, huku ikihudumia eneo lenye wakazi zaidi ya milioni 20.9 katika majimbo ya Alabama, Kentucky, Mississippi, Tennessee, pamoja na sehemu ya Florida iliyoko magharibi mwa Mto Apalachicola.

 Uwiano wa waumini katika eneo hilo ni karibu Muadventista mmoja kwa kila watu 690. Ni moja ya eneo lenye umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa sababu ni sehemu ya kile kilichojulikana kuwa  “Regional Conferences,” zilizoanzishwa kihistoria kuhudumia hasa Wamarekani Waadventista weusi wakati wa zama za ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Kutokana na historia hiyo, Konferensi hii imekuwa na sauti yenye uzito katika masuala ya haki za kiraia, haki za kupiga kura, na usawa wa kijamii. Mbali na huduma za kiroho, Waadventista katika eneo hilo wana ushawishi mkubwa kupitia makanisa, shule, na huduma mbalimbali za kijamii zinazohudumia jamii za Kusini mwa Marekani.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.