MBUNGE ATAKA MAWAZIRI,AG NA DPP WAWAJIBISHWE
Mbunge wa Jimbo la Kisesa nchini Tanzania Luhaga Mpina ameliomba Bunge kuwawajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) kwa kitendo cha kudharau Mahakama iliyoamuru wafugaji wa maeneo mbalimbali nchini walioshinda kesi mahakamani warudishiwe mifugo yao 6,000 iliyokamatwa na Serikali nchini humo.
Akichangia
hotuba ya Makadirio ya mapato na Matumizi ya Wizara ya Malisiali na Utalii nchini Tanzania kwa
mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni Dodoma, Mpina amesema hadi leo viongozi hao
wamekataa kutii amri hiyo ya Mahakama na kuwadhulumu haki wananchi hao na kwa
makusudi wamevunja Katiba ibara ya 107A (i) inayoitaja Mahakama kuwa ndio yenye
kauli ya mwisho ya utoaji haki.
“Suala
la wafugaji walioshinda kesi mahakamani lakini Serikali imekaidi kurudisha
mifugo yao, katika Pori la Akiba la Maswa na WMA ya Makao ng’ombe walikamatwa
1,739 walipoenda kwenye Mahakama Kuu Shinyanga wafugaji hao walishinda,
wakaenda kwenye Mahakama ya Rufaa Tabora wakashinda ngombe jumla ya 1,739 mpaka
leo hii hawajarejeshwa na Serikali” alisema Mpina.
Mpina
alisema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwa kesi ya Jinai 136 ya mwaka 2017
ng’ombe 466 walikamatwa katika Pori la akiba la Swagaswaga ambapo ni ng’ombe
113 tu walirudishwa lakini wengine wote katika 466 hawajarudishwa mpaka sasa.
“Pori
la Akiba la Muyowosi ambako ng’ombe 216 walikamatwa mpaka leo hawajarudishwa na
Serikali katika ile hesabu ya ng’ombe 6,000 hii ni mifano tu Mh. Mwenyekiti ya
wafugaji wetu ambao wameshashinda kesi mahakamani lakini Serikali haijarudisha
mifugo yao”alihoji Mpina
Mpina alisisitiza kuwa sio mara ya kwanza kulizungumza suala hilo bungeni kwani
hata wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu alilizungumza suala hilo kwa uchungu
mkubwa akiamini Serikali italizingatia.
Mpina
alihoji iweje Mahakama imeshaamua ng’ombe warudishwe kwa wahusika lakini Serikali
hawajarudisha mpaka leo ng’ombe hao wa wafugaji jambo lilioacha huzuni na
umasikini mkubwa kwa wananchi hao.
“Waziri
wa Malisiali na Utalii hajarudisha mifugo ya wananchi, Waziri wa Katiba na
Sheria amekataa kurudisha mifugo ya wananchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
amekataa kurudisha mifugo ya wananchi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali
(DPP) amekataa kurudisha mifugo ya wananchi hawa wote Mh. Mwenyekiti wamevunja
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wao wameapa kuitetea na
kuilinda” alisema Mpina.
Mpina
alihoji tayari wananchi hawa wameshinda kesi Mahakamani, Mahakama za Kuu
zimeamua mifugo warudishwe, Mahakama ya rufaa imeamua mifugo warudishwe nani
tena mtoa haki mwingine ambaye anasubiriwa.
“Mwenyekiti naomba Bunge lako liamua leo hatma ya mifugo ya wananchi hawa
irudishwe kwa wananchi ambao wamepata mateso makubwa sana kwa muda mrefu na
Serikali imeshindwa kurudisha mifugo yao hawa Mawaziri wamevunja Katiba ya
Jamhuri ya Muungano Ibara ya 107A(i) na Kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano
imevunjwa na mawaziri hawa Mh. Mwenyekiti Bunge lako lichukue nafasi”alisema
Mpina.
Akihitimisha
bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujibu hoja za wabunge kuhusu
bajeti hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro ameliambia Bunge
kuwa wafugaji wote walioshinda kesi Mahakamani watarudishiwa mifugo yao kama
hukumu zilivyoelekeza.
“Mh.
Naibu Spika imeongelewa hapa watu wameshinda kesi lakini mifugo yao haijulikani
ilipo hawajakabidhiwa Mh Naibu Spika nchi hii inaongozwa na utawala wa sheria
na sheria inatafsiriwa Mahakamani mtu akienda mahakamani ameshinda kesi lazima
apate kile alichokishinda mahakamani” alisema Waziri Ndumbaro.
Hivyo
Waziri Ndumbaro akaahidi kupitia Bunge kuwa Serikali itafuatilia kwa karibu
kesi zote ili kila mmoja aweze kupata haki inayostahili.
“Mimi
niwaahidi waheshimiwa wabunge na niliahidi bunge lako tukufu tutafuatilia kesi
zote hizi ili haki za wale walioshinda kesi mahakamani zisipotee, nimelichukua
jambo hilo kwa umakini wa hali ya juu na niwaahidi tutakwenda
kutekeleza”alisema Waziri Ndumbaro.
Bunge
limepitisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa
2021/2022 ya jumla ya sh 571,623,424,000.
Post a Comment