MTANGAZAJI

WAZIRI NCHEMBA AHIMIZA UFUGAJI WA KISASA TANZANIA



Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt Mwigulu Lameck Nchemba amesema utaratibu wa sasa wa wafugaji kuhamahama na mifugo kwa ajili ya kutafuta malisho na maji umepitwa na wakati na kuahidi kuwa Wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mipango ya kuendeleza sekta ya mifugo nchini humo.


Waziri huyo amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, jijini Dodoma kujadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuboresha sekta ya mifugo ili iweze kuongeza mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

 “Tutakavyo weka mipango ya kisasa ya kukuza uzalishaji katika eneo hili la mifugo, tutatengeza wigo mkubwa wa walipakodi, tutabadilisha maisha ya watu wetu, tutakuza uchumi na ajira” alisema Dkt. Nchemba

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, alimshukuru Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kwa kukutana na vingozi wa Wizara hizo mbili na kuahidi kuwa ushauri uliotolewa utafanyiwa kazi kikamilifu ambapo ameunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kuchambua mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa katika kikao hicho alichosema kilikuwa ni cha muhimu.

“Tutaangalia namna ya kupanua na kuwa na  maeneo maalum ya malisho ya mifugo yetu pamoja na kuboresha ufugaji ili ubadilike kutoka ufugaji wa kiasili kwenda ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija” alifafanua Mhe. Ndaki

Alisema kuwa wafugaji watakaokuwa tayari kubadilisha namna ya ufugaji wao watapelekwa kwenye maeneo hayo yatakayowekewa miundombinu yote muhimu ya ufugaji ikiwemo maji, majani ya malisho na maji.

Wakizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, aliishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha maeneo ya ufugaji (Runch) kila mkoa na kujenga miundombinu itakayowasaidia wafugaji kufuga mifugo yao kisasa ili waweze kuongeza kipato chao, kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuondokana na umasikini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole-Gabriel aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuiwezesha Wizara yake kifedha kwa ajili kufanya utafiti katika sekta ya mifugo ili kuongeza mbinu za kisasa za kuongeza uzalishaji.

 Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), kwenye kikao hicho Prof. Elisante Ole-Gabriel, Tanzania ni ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika kwa kuwa na ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, Kondoo milioni 5.65, Punda 657,380, lakini tija yake bado ni ndogo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.