MTANGAZAJI

TCRA YATAKIWA KUOBORESHA VITENGO NA KUTOA ELIMU KWA UMMA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Tanzania  Dkt. Faustine Ndugulile ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC) kuboresha vitengo vyao vya mawasiliano ili kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano kwa kuzingatia haki na wajibu pamoja na matumizi sahihi ya simu janja na
mtandao.


Dkt. Ndugulile amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao chake chakazi cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha kujadili na kufanya mapitio ya taarifa za mapato na matumizi za taasisi hizo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 Kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Dkt. Ndugulile ameziagiza taasisi hizo kuboresha mifumo ya wananchi kutolea
malalamiko yanayohusu huduma za mawasiliano na kushughulikia malalamiko hayo kwa wakati na taarifa ya malalamiko hayo itakuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vya kila robo mwaka baina ya Wizara hiyo na taasisi zake.


Ameongeza kuwa elimu kwa umma ikitolewa kwa kiwango kinachojitosheleza kitapunguza baadhi ya malalamiko ya wananchi kwa mfano malalamiko ya vifurushi vya data kuisha haraka ambapo kwa namna moja ama nyingine inasababishwa na settings za simu janja kuruhusu programu zake kujiboresha zenyewe (automatic Updating).


“Kuna mambo ambayo ni muhimu wananchi kuyafahamu kwa mfano matumizi makubwa ya data yanayosababishwa na settings za simu janja ambazo zinaruhusu baadhi ya programu kujiboresha zenyewe nazo zinachangia vifurushi vya data kuisha haraka”, alizungumza Dkt. Ndugulile


Aliongeza kuwa Serikali inatengeneza mazingira wezeshi ya kuhakikisha mawasiliano yanafika kwa wananchi wote lakini kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kutokuwa na matumizi sahihi ya huduma hii, hivyo wananchi wanahitaji kuelemishwa ili kuhakikisha wanajua wajibu wao na haki zao na kuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).


Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, Naibu wake Dkt Jim Yonazi, Wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya Taifa ya Tehama (ICTC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), Menejimenti ya Wizara pamoja na baadhi ya watendaji wa taasisi zake.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.