COSOTA YAMTOZA FAINI YA MILIONI 5 MWIGIZAJI WA FILAMU KWA KUGHUSHI
Taasisi ya Haki miliki Tanzania yamtoza faini ya shilingi milioni tano Mwigizaji wa Filamu kwa kughushi nyaraka mbalimbali za filamu isiyo ya kwake na kuisajili kama mmililiki halali.
Akizungumza katika kikao hicho cha kupata suluhu ya Mmiliki halali wa Filamu ya ‘Mama Nongwa’ iliyokuwa imesajiliwa COSOTA na Mwigizaji Sabrina Abdallah kwa kughushi umiliki na mikataba mbalimbali, Kaimu Meneja Idara ya Usajili na Ugawaji Mirabaha COSOTA Bw. Philemon Kilaka amesema kitendo alichokifanya mwigizaji huyo ni kosa kisheria na ni ukiukwaji wa Sheria mbalimbali za nchi ikiwepo Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki na Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai.
Katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam baada ya mmiliki wa Filamu hiyo Bw.Jotham Ngulika kufika kusajili kazi hiyo na kuonekana filamu hiyo ilikwisha sajiliwa na Mwigizaji huyo kama mmiliki halali.
"Kitendo alichokifanya Sabrina cha kughushi nyaraka mbalimbali ikiwemo mkataba wa Muongozaji,(Director),Mkataba wa Mwandishi wa stori pamoja na Mkataba wa Mpiga picha huku akiwa anafahamu kuwa ni kosa,tunampa onyo kali pamoja na faini hiyo na akirudia kosa hili tunamfutia uanachama, hii ikawe fundisho kwa watu wengine wenye kufikiria kufanya hivi au wenye tabia
kama hii,’’alisema Bw.Kilaka.
Kwa upande wa Mwigizaji huyo Sabrina Abdallah alikiri kufanya kosa hilo la kusajili filamu hiyo kwa kughushi mikataba mbalimbali kinyume na sheria, ambapo alieleza kuwa filamu hiyo alipewa na Mpiga picha wa kazi hiyo (Cameraman).
"Nakiri kweli nimefanya kosa la kughushi nyaraka mbalimbali kuhusu umiliki wa kazi hii hivyo naomba msamaha kwa mmiliki wa kazi hii na COSOTA kwa usumbufu niliyosababisha na ahidi kuwa balozi wa kukemea matumizi ya kazi usiyo na umiliki nayo bila ridhaa ya mmiliki"alisema Sabrina.
Halikadhalika nae Mmiliki wa Filamu hiyo Bw. Jotham Ngulika aliishukuru COSOTA kwa kufanikisha kurudisha umiliki wa kazi yake na kufanikisha kumpata mhusika aliyekuwa amesajili kazi hiyo kwa kughushi kinyume na utaratibu.
Wito wa COSOTA kwa wadau wa kazi za ubunifu ni kuacha kuibiana kazi kwani hilo kosa kisheria na linahatarisha ukuaji wa kisekta
Post a Comment