WAZIRI MKUU WA TANZANIA APONGEZA UBUNIFU WA MIFUMO YA FEDHA NA KUDHIBITI MAKOSA YA BARABARANI
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alitembelea banda la
Serikali katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNICC) hivi karibuni na kujionea namna mifumo ya kielektroniki ya kukusanya maduhuli ya
Serikali wa GePG unaosimamiwa na Wizara ya Fedha na mfumo wa Jeshi la Polisi wa
kudhibiti wasiolipa faini za barabarani (TMS) inavyofanya kazi.
Waziri Mkuu aliwapongeza wabunifu wa mifumo hiyo ambayo kwa sasa inasaidia
Serikali kupata mapato yake kwa wakati pamoja na kupunguza makosa ya barabarani
ambayo yamekuwa yakiongeza ajali na kupunguza nguvu kazi ya Taifa.
Alisema uwekezaji katika Sekta ya Tehama ni muhimu kwa nchi wanachama wa SADC ili kudhibiti
uhalifu wa mtandaoni pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za umma.
Naye Mkuu wa Uendeshaji wa Mfumo wa GePG kutoka Wizara
ya Fedha na Mipango, Bw. Basil Baligumya, alisema Wizara imeshiriki mkutano huo
ili kuzionesha nchi mbalimbali zinazoshiriki mkutano huo namna Tanzania imepiga
hatua katika maendeleo ya teknolojia hususani katika usimamizi wa fedha na
ukusanyaji mapato ya Serikali kupitia mfumo wa GePG.
Bw. Basil alisema mfumo huo unadhibiti fedha za umma, umeongeza
makusanyo na uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, pamoja na kuongeza
usahihi wa taarifa za mapato.
Alisema kwa kuwa kubadilishana uzoefu ni miongoni mwa malengo
ya mkutano huo, wako tayari kujifunza mbinu mpya za kuendeleza mifumo nchini
pamoja na kuzielekeza nchi zitazokuwa tayari kujifunza namna ya kutengeneza
mifumo ya kusimamia mapato ya nchi zao.
Kwa nyakati tofauti, washiriki mbalimbali
waliotembelea banda hilo wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha mifumo hiyo ambayo
itasaidia kudhibiti ubadhilifu wa fedha za umma, kukusanya mapato ya serikali
kwa wakati pamoja na kudhibiti makosa ya barabarani.
Washiriki hao wamewapongeza watumishi wote
walioshiriki katika kutengeneza mifumo hiyo kwani wameonesha uzalendo wa dhati
kwa kuiwezesha Serikali kuweza kisimamia mapato yake kwa wakati.
Post a Comment