SHADRACK SAGATI UMETUACHIA PENGO
Na Derek Murusuri
AKIWA
anafundisha katika mojawapo ya shule za msingi za jiji la Dar es
Salaam, zaidi ya miaka 22 iliyopita, niliuona uwezo mkubwa wa uchambuzi
ndani ya SHADRACK SAGATI, Afisa wa habari katika Wizara ya Biashara,
Viwanda na Uwekezaji ambaye amefariki ghafla usiku wa Jumatatu
(30-7-2018).
“Unastahili
kuwa mwandishi wa habari. Kuna fursa nyingi za kujiendeleza katika
uandishi wa habari. Jiandae, nitakusaidia kama utakuwa tayari ili uje
usome katika chuo cha uandishi wa habari ninachofundisha,” nilimwambia
Sagati.
Tulikuwa
tumemaliza ibada ya Sabato, katika Kanisa la Waandventista wa Sabato la
Magomeni Mwembechai ambapo yeye alikuwa akihudumu kama mwanakwaya katika
kwaya ya Kanisa hilo.
Mwalimu
Sagati alinisikiliza kwa makini na maneno yangu yalimwingia na kuuchoma
moyo wake. Alitaka kujua ni namna gani ataweza kumudu kulipa ada na pia
kazi yake ya ualimu wa shule ya msingi.
“All
things are possible,” nilimwambia. Alishawishika palepale. Ndani ya
muda mfupi alikuwa mwanafunzi wa cheti wa chuo cha uandishi wa habari
cha Serikali (TSJ) na kuanza safari yake ya mafanikio makubwa katika
fani ya uandishi wa habari hapa Tanzania.
Akiwa
kijana mwenye akili nyingi, fikra pevu, mwenye bidii na hekima,
Shadrack Sagati aliitumikia vema sana fani ya uandishi hadi kuwa
mwandishi wa kutegemewa katika habari zinazohusu matukio makubwa ya
kitaifa katika gazeti la Serikali la Habari Leo.
Wakati
nikiwa nawakilisha taasisi Uingereza ya elimu ya biashara hapa nchini,
The Association of Business Executives (ABE), Sagati alinipa ushirikiano
wa hali ya juu sana. Nilizidi kugundua kuwa alikuwa mtiifu na pia
hakusita kutoa ushauri wa kuboresha pale ilipobidi.
Siku
moja nilimpigia simu kumpa habari. Wakati sakata la “the northen
corridor”, pale “coalition of the willing”, wakiwa wamezimia kwenda bila
Tanzania, nikatoa maoni yangu kuhusu ushirikiano mbadala wa Tanzania,
Burundi, DRC na Comoro.
Aliandika
habari katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la Habari Leo. Bungeni
Marehemu Kepteni Komba na wabunge wenzake wakaibeba hoja hiyo na
kulifanyia kazi.
Rais wa
wakati huo, Mhe Dk Jakaya Kikwete aliona vema kwenda Bungeni na kwa
hekima yake akalihitimisha suala hilo. Sagati alijaaliwa akili na wepesi
wa kuchakata habari. Alijua habari nzuri iko wapi. Hakika aliendeleza
kipaji cha ualimu katika fani ya habari.
Sagati
hakuwa mwandishi wa kawaida. Alivuka viwango hivyo. Alikuwa mtu mwenye
malengo makubwa. Kwanza alianza kwa kujiendeleza kielimu. Mbali na
kurudi tena chuoni ili kuwa mahiri katika uandishi wa habari, Sagati
alikwenda mbali zaidi na kupata Shahadi ya usimamizi wa biashara
(Bachelor of Business Administration) katika chuo cha elimu ya biashara
(CBE). Alianza masoma ya Shahada ya Uzamili.
Elimu
ya biashara ilimsaidia kufanya tathmini nzuri na za kuvutia ambazo pia
zilitumiwa na viongozi mbalimbali wa biashara na siasa. Wengi walimwita
kwa ushauri na kuripoti habari zao kwa vile waliamini katika weledi wake
na tunu zilizomuongoza katika maamuzi yake.
Alijijengea
mazingira ya kuaminiwa. TRUST huja baada ya mwandishi kujipambanua
katika uandishi wake na kuonesha umahiri. Weledi wa Sagati ulikuwa
kielelezo cha uandishi bora nchini.
Takriban
wiki tatu zilizopita, nilimpigia simu Shadrack kuhusu jambo moja.
Aliniambia kuwa alikuwa safarini akitokea Dodoma kurudi Dar. Aliniambia
habari njema na alikuwa mwenye furaha sana. Mwanafalsafa Abraham Maslow,
anasema, “self actualization,” kiwango cha juu unachofika katika wakati
maalum.
“Nimepewa
mapumziko ya wiki moja kupisha mchakato wa kunihamishia Wizara ya
Biashara, Viwanda na Uwekezaji,” alinieleza kwa furaha.
Lakini,
alinishangaza sana kuhusianisha mafanikio yake na mimi. “Kaka, siku
zote nakushukuru sana, japo huwa sikwambii, lakini wewe ndiye
uliyenishauri na kunisaidia kuingia katika fani ya uandishi wa habari,
nakushukuru sana,” alisema.
Furaha
ile ilimfungua zaidi. Kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote Yule, nilifurahi
sana kwa utambuzi huo. Lakini lilikuwa fumbo. Hakika lilikuwa fumbo.
Tuliongea
mawili matatu kuhusu mambo ya miongo miwili iliyopita na jinsi
nilivyofanikiwa kumshawishi kubadili fani kutoka ualimu wa shule ya
msingi hadi kuwa mwana habari mahiri, akitoka katika kufundisha darasa
moja hadi kufundisha umma wa watanzania kupitia media.
Tulifurahi
na kuahidi kukutana tena ili kuweka mikaka mipya ya maisha ya hapa
duniani. Sikujua simu ile ndiyo ilikuwa ya mwisho kwetu kuongea katika
uhai huu.
Sasa ndiyo
ninaelewa kwa nini Roho wa Mungu alimwongoza Shadrack Sagati kukumbushia
mambo yaliyotokea zaidi ya miongo miwili wakati akiingia katika fani ya
uandishi wa habari. Sikujua kuwa alikuwa anatoa shukurani akijiandaa
kuhitimisha safari yake katika dunia hii.
Mwenyezi
Mungu alitupatia nafasi nzuri ya kuagana. Hapo ndipo ninaamini katika
Roho wa Mungu ndani ya wanadamu. Mambo mengi yanaongozwa na Mungu pasipo
sisi kufahamu. Hili ni mojawapo. Mimi nimejifunza.
Ni rahisi kusema kuwa maisha ya Sagati yamezimika mapema na ghafla kama mwanga wa mshumaa.
Hata
hivyo Imempendeza Mwenyezi Mungu ameona heri kumpa pumziko mdogo wangu
Sagati. Jina la Bwana lihimidiwe.
Tunapokuwa
tunamshukuru sana Mungu kwa maisha ya utumishi ya Sagati, wakati mioyo
ikijaa huzuri nyingi na machozi kuchuluzika machoni na mioyoni,
tuinamishe vichwa kumshukuru Mungu kwa zawaji njema ya Sagati hapa
duniani. Hata hivyo, mwisho bado.
Ni
wakati kama huu, mioyo yetu inapojawa na huzuni kubwa, Elvis Presley,
mwimbaji wa zamani wa Marekani alisema na anaeleza mustakabali wenye
faraja kubwa…anaimba na kusema;
*“si
mbali sana tutafika mwisho wa safari ya maisha. Yawezekaza kamwe
hatutakutana tena. Hadi tutakakusanyika katika jiji ling’aalo la
mbinguni, kule mbali kabisa katika pwani ile nzuri sana.*
*Mahali
ambapo maua huchanua milele zote bila kunyauka na kule hapatakuwa na
kuagana tena. Kama hatutaonana tena katika ng’ambo hii ya mbingu,
nitakutana na wewe katika pwani ile nzuri ya mbinguni.”*
Post a Comment