MTANGAZAJI

BUNDA:WALIMU WAHAMISHWA KUWAEPUSHA NA USHIRIKINA

Halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara imewahamisha walimu wote
saba wa shule ya msingi Nambaza ya wilayani humo  inayodaiwa kushamiri
kwa vitendo vya kishirikina huku ikiwataka wakazi wa kijiji hicho
kuachana na vitendo hivyo vinginevyo hawatopelekwa walimu.

Hatua hiyo ya halmashauri inakuja  zikiwa zimepita siku sita
tangu kuwepo kwa madai ya walimu wawili wa kike wa shule hiyo
kudhalilishwa kimwili kwa njia ya kishirikina usiku wa kuamkia Juni 29
mwaka huu hali iliyopelekea walimu wote kufungasha mizigo yao
kujinusuru na vitendo hivyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Lucy Msoffe amesema  kuwa
hatua hiyo imefikiwa kama njia ya kuwarejeshea walimu hao saikolojia
yao inayoonekana kuathiriwa na vitendo hivyo vilivyowadhalilisha na
kuwaondolea utu wao mbele ya jamii.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo,mara baada ya tukio hilo kutokea na
kamati ya ulinzi na usalama kufika shulkeni hapo, walimu hao
walionekana kusononeshwa na vitendo hivyo hata kuwasilisha kilio chao
kwa mwajiri cha kuwahamisha mahala hapo jambo lililozingatiwa na
uongozi wa halmashauri hiyo.

Msoffe amesema mbali na kudhalilishwa huko pia walimu wa shule hiyo
wamekuwa wakifanyiwa vitendo kadhaa vya kishirikina shuleni hapo ikiwa
ni pamoja na kukuta mifupa na makombo ya chakula vitandani kwao
nyakati za usiku huku wengine wakijikuta wamelala chini bila kujijua.

Kwa upande wake,mwenyekiti wa chama cha walimu(CWT) wilayani humo,
Mongson Kabeho licha ya kuupongeza uamuzi huo wa halmashauri akisema
ni busara lakini pia ameitaka jamii ya kijiji cha Nambaza kujijengea
utamaduni wa kuwaheshimu watumishi kwa kutowatendea vitendo vya jinsi
hiyo.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.