MTANGAZAJI

MIAKA 19 YA KUZAMA MV BUKOBA:MELI ZA ZIWA VICTORIA NI MAJENEZA YANAYOELEA


 

 



Na Conges Mramba,Mwanza.

Leo alhamisi,Mei 21mwaka huu wa 2015 ni Kumbukumbu ya 19 tangu Meli ya Mv.Bukoba ilipozama umbali wa kilomita 12 hivi za majini,kutoka Bwiru jijini hapa.

Mv.Bukoba ilipozama Mei 21 mwaka 1996,walikufa watu kama 1,000 hivi,wengine zaidi ya 100 waliokolewa.

Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini,SUMATRA,Mkoani Mwanza,Michael Rodgers,anasema hivi sasa meli zinazosafirisha abiria Ziwa Victoria,lazima kutimiza vigezo vilivyowekwa na sheria.

 Katika Ziwa Victoria,SUMATRA wana ofisi Mwanza, Bukoba na Musoma.

Ziwa Victoria kuna visiwa takriban 60, Ukerewe pekee kuna visiwa 38; vingine hukaliwa na wavuvi tu.

  Mei 21, mwaka 1996,Meli iliyomilikiwa na Shirika la Reli(TRC) ilizama umbali wa maili nane(kilomita 12) za majini, jirani na Bandari ya Mwanza, uelekeo wa Bwiru.

 Mv. Bukoba, ilipinduka kisha kuzama,ikasababisha vifo vya zaidi ya watu 800.Wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa,wakipoteza mali nyingi za mamilioni ya shilingi,hususan mikungu mingi ya ndizi.

 Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Robert Kissanga, iliyochunguza chanzo cha Ajali hiyo,usiku wa kuamkia siku ya ajali,(Mei 20 mwaka huo)Mv.Bukoba ilipakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37 wa Meli hii.

  Kati ya hao, 114 waliokolewa wakiwa hai, wakati 391 waliopolewa wakiwa   wamefariki  dunia,wakazikwa katika Makaburi ya Igoma,nje kidogo ya Jiji la Mwanza.

Miili mingine ilichukuliwa na jamaa zao kwenda kuzikwa kwao. Jumla ya miili 332 haikupatikana.

Kila mwaka, ifikapo Mei 21, wadau mbalimbali huongozana na viongozi wa madhehebu ya dini na waganga huenda eneo la ajali,kufanya ‘matambiko’ na kumwaga mchanga eneo hilo la  majini!

  Serikali iliwashitaki  katika Mahakama Kuu  aliyekuwa Nahodha wa Mv.Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru, (ambaye sasa ni Marehemu),Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari(wakati huo THA),Gilbert Mokiwa, aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.Kesi hiyo Nambari 22 ya mwaka 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14 mwaka 2001.

Miongoni mwa waendesha mashitaka katika kesi hiyo ni Eliezer Feleshi, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini(DPP) na William Magoma.

  Hukumu ya kesi hii ilitolewa Ijumaa, Novemba 29 mwaka 2002,majira ya saa sita mchana hadi saa 9 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Juxton Mlay(amestaafu).

 Washitakiwa wote walishinda kesi hiyo,kufuatia Hukumu yenye kurasa 118 iliyosomwa kwa dakika 160 na Jaji Mlay,kusema Mv.Bukoba ilizama kwa sababu haikuwa na uwiano wa majini, na siyo uzembe wa washitakiwa.

 Serikali ikakata rufaa, hadi leo majaliwa na rufaa hiyo hayajulikani,na baadhi ya washitakiwa wamefariki dunia,bila kujua hatma ya kesi hiyo na stahili zao.

   Mv.Bukoba ilikuwa ‘Kaburi’ lenye kuelea Ziwa Victoria. Ilikwishapigwa marufuku,kwa kuwa haikuwa na viwango vya ubora-sea   worthiness.

Ilijengwa na Kampuni ya Kibelgiji,ikazinduliwa  Julai 27 mwaka 1979.

Siku ya uzinduzi, ilibainika haikuwa thabiti,na ilikosa uwiano,ilitaka kumtosa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Rais wa nchi wakati huo.

 Meli nyingine ya mizigo, Mv.Nyamageni,ilizama ziwa Victoria ikiwa na abiria zaidi ya 20 waliosafirishwa pamoja na masanduku ya soda kwenda visiwani.

 Miaka michache iliyopita,  Mv. Pacific iliyokuwa ikisafiri kati ya Mwanza na kisiwa cha Ghana ilizama, ilikuwa na abiria 17, mmoja alifariki wengine wakaokolewa.

 Kwa mujibu wa SUMATRA, Boti nyingine iliyokuwa na abiria 31 ilizama huko Musoma,mkoani Mara,abiria   wote wakaokolewa kwa kutumia zana za uokozi.

 Kwa sasa Meli ya MV.Victoria haiendi Bukoba mamlaka ikichelea kuweza kusababisha ajali nyingine,meli hiyo inafanyiwa ukarabati.

Isipokuwa,Mwaloni Kirumba,wasafiri na wasafirishaji wanaendelea kupakia abiria na mizigo tena wakati mwingine huwachanganya abiria na mafuta ya taa,dizeli na petrol.

Naam hii ndiyo miaka 19 ya Mv Bukoba, Mwanza bado kuna majahazi,boti na meli zisizo na viwango;ni sawa na majeneza yenye kuelea.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.