MAENDELEO YA AFYA YA RAIS KIKWETE
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumanne Novemba
11, 2014, aliendelea kufanya kazi ndogo ndogo wakati akiendelea na matibabu
katika Hospitali ya Johns Hopkins.
Kwa mujibu wa
ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa facebook na twitter Rais Kikwete
ameandika kuwa anaendelea na kazi ndogo ndogo kukiwa na maelezo yaliyoambana na picha
inayomwonesha akiandika ujumbe katika kitabu kidogo cha kumbukumbu mbalimbali
za kiofisini.
Taarifa ya
kurugenzi ya mawasiliano ya Rais iliyotolewa jana jijini Dar es salaam ilieleza
kuwa Kikwete alianza kuwasiliana na mamia kwa mamia ya wananchi mbali mbali
nchini kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wa kumpa pole, kumtakia heri na
nafuu ya haraka ambao amekuwa anatumiwa na wananchi tokea mwishoni mwa wiki.
Aidha, Rais
Kikwete juzi alizungumza kwa simu na uongozi wa juu wa Tanzania kwa mara ya
kwanza tokea afanyiwe upasuaji. Rais alizungumza na Makamu wa Rais Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein
na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda.
Madaktari
wanaondelea kumtibu Rais Kikwete juzi waliondoa bandeji kwenye sehemu ambako
alifanyiwa upasuaji wakieleza kuwa hali yake inaendelea vizuri na anapata nafuu
kwa kasi
Post a Comment