MTANGAZAJI

SAMWELI SITTA AITAKA JAMII KUJITOLEA KUSAIDIA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU



Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Samuel John Sitta ameitaka jamii ya kitanzania kujitolea kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu,ili waweze kujikwamua katika lindi la umaskini.

Waziri Sitta amesema vyama vya hiari vya kijamii vina jukumu la kuwatambua watu wanaoishi katika mazingira magumu hususani watoto wanaoishi mitaani ili kuwasaidia kuishi na kuwapeleka shule.

Akizungumza mwishoni mwa juma lililopita jijini Mwanza wakati  akizindua kikundi cha Thamani Utu,Waziri huyo ameitaka jamii kuacha kuwategemea wafadhili katika masuala yaliyo ndani ya uwezo wa watanzania  kama kuwasaidia watoto,vijana na jamii inayoishi katika mazingira magumu ili kuipatia huduma za afya,elimu na malezi.

Mwenyekiti wa kikundi cha Thamani ya Utu ,Elizabeth Mukama amesema nia ya kuanzisha kikundi hicho ni kuelimisha umma kujua thamani ya utu katika kipindi hiki ambacho jamii imejiingiza katika lindi la ulevi,ukahaba,uhalifu na madawa ya kulevya.

Elizabeth Mukama  mshiriki wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato Pasiansi jijini Mwanza pia ameandika kitabu kiitwacho Thamani ya Utu chenye kurasa 80 kwa nia ya kuiasa jamii kuwalea na kuwatunza vyema watoto wa kike ili watimize ndoto zao za kimasomo  kilichozinduliwa na Waziri Sitta siku ya tukio hilo.

Kitabu hicho kinachokemea janga la mimba mashuleni na thamani ya watoto wa kike kimeshaanza kusambazwa katika ukanda wa Ziwa Vitoria ambako wanafunzi wengi wa kike huachishwa masomo kutokana na mimba za mapema kwa kushawishiwa na watu wanaojihusisha na uvuvi.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.