MTANGAZAJI

WAFIKISHWA MAHAKAMANI BAADA YA KUKUTWA NA NYAMA YA PUNDAMILIA

Watu wawili wakazi wa wilaya ya Serengeti leo wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bunda wakikabiliwa na mashtaka ya kukutwa ndani ya hifadhi ya Serengeti wakiwa na shehena ya nyama ya pundamilia kwenye pikipiki yao.

Waliofikishwa mahakamani hapo ni Nindwa Dindai na Mperwa Halili ambao walikamatwa Machi 22 mwaka huu wakiwa na shehena hiyo ya nyama yenye thamani ya sh.1,920,000 waliyokuwa wameipakia kwenye pikipiki namba T 111 AMG.


Mwanasheria wa mamlaka ya hifadhi za taifa (TANAPA) Emmanuel Zumba amedai mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wameelezewa kuwa ni wawindaji sugu kwa kutumia pikipiki, walikutwa na kisu kimoja na panga moja.


Zumba ameiomba mahakama hiyo iliyokuwa chini ya hakimu mfawidhi Safina Semfukwe kutowapa dhamana washtakiwa hao kwa vile maelezo yao ya awali yanaonesha kuwepo kwa mtandao wa uwindaji huo jambo ambalo bado linachunguzwa na mamlaka husika.


Washtakiwa kwa pamoja wamekana mashtaka yao na kurudishwa mahabusu hadi Aprili 4 mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.


Wizi wa kutumia pikipiki umeonekana kushika kasi katika maeneo ya vijiji jirani na hifadhi ya taifa ya Serengeti ambapo wawindaji hao humfukuza mnyama kwa kutumia pikipiki hata kumfanya achoke ndipo humkatakata kwa panga na kumchoma mikuki hadi kufa.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.