MTANGAZAJI

MAANDALIZI YA SIKUU YA MASHUJAA NA ZIARA YA RAIS JAKAYA KIKWETE MKOANI KAGERA


HALI YA MAANDALIZI YA MAADHIMISHO YA MASHUJAA KITAIFA JULAI 25, 2013 
NA 
ZIARA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 
MKOANI KAGERA


Ndugu Wananchi, kama ambavyo nimewahi kuwajulisha mara nyingi kupitia vyombo vyetu vya habari juu ya Mkoa wetu wa Kagera kupewa heshima kubwa ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kitaifa mwaka 2013, leo napenda kuwajulisha juu ya maandalizi ya maadhimisho hayo ambayo yataadhimishwa tarehe 25/07/2013 hapa mkoani kwetu katika Wilaya ya Muleba katika Kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya. Pia nawajulisha kuwa maadhimisho hayo yataambatana na ziara ya kikazi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkoa wa Kagera.


MAADHIMISHO YA MASHUJAA MWAKA 2013
Ndugu Wananchi, Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kumbumbu ya Mashujaa mkoani Kagera yanaendelea vizuri kamati mbalimbali za maandalizi zinatekeleza majukumu yake ya mwisho ili kufanikisha maadhimisho siku ya Alhamisi ya wiki hii tarehe 25 Julai, 2013. Kamati zinazoandaa maadhimisho hayo   ni Kamati ya Mapokezi, Usafiri na Malazi; Kamati ya Ujenzi Uwanja na Mapambo; Kamati ya Chakula na Afya; Kamati ya Ulinzi na Usalama; na Kamati ya Burudani, Habari na Uhamasishaji.
Ndugu wananchi, Kwa kiwango kikubwa maandalizi yote yamekamilika na tunatarajia kuanzia leo kupokea wageni kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa, pia nje ya nchi watakaohudhuria maadhimisho hayo.


Mkoa wetu umejipanga vizuri kuwapokea wageni wote watakofika mkoani hapa kwa ukarimu na bashasha kubwa.

Wajibu wa Wananchi
Ndugu wananchi, Napenda kutumia fursa hii kuwaomba kuwa wakarimu kwa wageni wetu  wote tunaowatarajia kuanzia leo  kwa kutekeleza majukumu yenu kama  Wanakagera kama ifuatavyo;
Ø Kila mwananchi kuhakikisha maeneo yake na mazingira yanayomzunguka yanaendelea kuwa katika hali ya usafi kama utamaduni wetu. Pia kumwajibisha mtu yeyote atakaeonekana anachafua mazingira yetu. Hili ni jukumu la kila mwananchi.


Ø Kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha Siku yenyewe ya Kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai, 2013   huko Kaboya Wilayani Muleba.  Kwani hatuna budi kuwakumbuka Mashujaa wetu kwa sababu ya historia ya mkoa wetu kushiriki katika vita ya kumwondoa adui aliyekuwa amevamia nchi yetu kupitia ardhi ya mkoa huu mwaka 1978 hadi 1979.
Ø Kila mwananchi kuhakikisha anaitunza amani na utulivu kama destuli ya mkoa wetu kwa wakati wote wageni wetu watakapokuwepo hapa mkoani na baada ya maadhimisho ya Mashujaa. Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imejipanga vizuri kuhakikisha  amani na utulivu vinatawala wakati wote. Kwa mwananchi yeyote atakayeona viashiria vya uvunjifu wa amani atoe taarifa mara moja ili taarifa hizo zifanyiwe kazi mara moja.

Wajibu wa Vyombo vya Habari
Ndugu Wananchi, Vyombo vyetu vya habari vina wajibu wa kuhakikisha vinaendelea kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kuhusu Maadhimisho ya Mashujaa kama ambavyo vimekuwa vikifanya kuanzia mwezi Mei, 2013.

Aidha, nawaombeni Waandishi, Wahariri na Wamiliki wa vyombo vya habari kutumia fursa hii kuutangaza mkoa wetu wa Kagera katika sekta mbalimbali za uwekezaji na fursa mbalimbali zinazopatikana katika mkoa wetu.
Vilevile nawaombeni Wamiliki wa vyombo vya habari hasa redio zetu za jamii  kutoa muda wa kutosha  katika vituo vyenu vya redio kurusha habari na matukio ya Kumbukumbu za Mashujaa papo kwa papo  (live coverage) siku ya maadhimisho ili wananchi ambao hawatapata muda wa kufika Kaboya wazipate habari hizo kupitia redio zetu za Jamii.

ZIARA YA MHE. RAIS MKOANI KAGERA
Ndugu Wananchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye atakayekuwa mgeni Rasmi Katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai, 2013. Pia Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika mkoa wetu wa Kagera.

Ndugu Wananchi, Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais Kikwete anatarajia kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wetu kama ifuatavyo:
§  Kuweka jiwe la msingi katika ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.
§  Kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Kagoma - Rusahunga
§  Kuweka jiwe la msingi barabara ya kiwango cha lami Kyaka hadi Bugene
§  Kufungua Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
§  Kufungua jengo la kitega uchumi la Chama Kikuu cha Ushirika (KCU Ltd)
§  Kuzindua mradi wa maji Muleba
§  Kuzindua kivuko kipya Rusumo  (Ngara)
§  Kuzindua mradi wa usambazaji umeme vijijini Nyaishozi (Karagwe)
§  Kuzindua Wilaya Mpya ya Kyerwa

Ndugu Wananchi,Vilevile Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataongea na wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara katika Wilaya zetu ndani ya mkoa.

Ndugu Wananchi, nawaombeni kujitokeza kuanzia tarehe 24/07/2013 uwanja wa ndege wa Bukoba ili kumpokea Mheshimiwa Rais, pia atakapokuwa anafanya ziara katika Wilaya zetu tujitokeze kwa wingi kumsikiliza.

Mwisho; Nawatakia ushiriki mzuri katika kuadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa na mapokezi mazuri ya wageni wetu hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kagera: Amani na Maendeleo.
Amani na Maendeleo; Kagera.

Imetolewa na: Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe
Mkuu wa Mkoa wa Kagera

22 JULAI, 2013
                  

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.