MTANGAZAJI

KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO LATOA MSAADA KWA WAFUGAJI WALIOCHOMEWA NYUMBA

Mchungaji Alphonce Mayo akikabidhi magunia ya vyakula kwa waathirika wa moto

 
 Moja ya nyumba zilizoteketea

Mchungaji Mayo akimwaangalia mtoto aliyekuwa anaumwa, katika moja ya nyumba zilizoathirika na moto
 
Askofu Mkuu wa kanisa la Wa-Adventista wa Sabato, Jimbo la Kaskazini-Mashariki mwa Tanzania (NETC) Mchungaji Alphonce Mayo, jumatano hii ametoa msaada kwa niaba ya jimbo la kaskazini mashariki mwa Tanzania kwa nyumba 16 zilizochomwa moto wafugaji wa kimasai
 
Tukio hili la kuchomwa nyumba za wafugaji limeleta hasara kubwa ya Nyumba 16, Mifugo, Vyombo, baiskeli, viti, Nguo kwa nyumba 16 za wafugaji, na kati ya nyumba hizo 12 ni za waumini wa kanisa la Waadventista wa Sabato, wanaosali katika kundi la Chang’andu-Mtaa wa Handeni,Tanga.
 
 Msaada huo  ni madebe 24 ya unga wa mahindi, madebe 24 ya Mahindi, kilo 100 za Maharage, Maturubali ya mahema 10. 
 
 Katika hotuba yake ya kuwatia moyo baada ya kushuhudia nyumba zilizochomwa moto, Mchungaji Mayo alisema, katika Biblia uko mfano wa Ayubu ambaye alipatwa na majanga makubwa na mazito ya kupotelewa na watoto pamoja na vitu alivyokuwa navyo lakini kamwe hakumuacha Mungu. 
 
Mayo aliwasihi wahanga hao waendelee kumtegemea Mungu hasa katika wakati huu mgumu, kwa kudumu katika maombi na ibada bila kulipa kisasi.
 
 Akihitimisha hotuba yake Mchungaji Mayo ameyaomba makanisa ya WaAdventista jimbo la kaskazini mashariki, kukusanya misaada mbalimbali ya  vyakula, nguo, mahema, ili kuwasaidia ndugu zetu hawa, ameomba misaada hiyo ipitie kwa wachungaji wa mitaa katika mitaa 37 ya jimbo hilo, ili iwafikie wahanga hao. 
 
Naye mchungaji Kiongozi wa mtaa wa Handeni Mchungaji Wilbert Sambeke pamoja na Kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho, wameshukuru kwa kanisa kutoa msaada huo kwani wananchi hao wapo katika shida  ya kukosa mahitaji yao muhimu hasa wakati huu ambapo mvua zinaendelea kunyesha kwa wingi katika eneo hilo
 
 Tukio hili la kusikitisha lilitokea usiku wa kuamkia Alhamis  machi 28,2013  saa nne usiku katika kijiji cha Chang’andu, Mombo wilaya ya Korogwe, kwa kundi kubwa la watu wanaotuhumiwa kuvamia kwa sababu za uhasama wa wafugaji na wakulima.

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.