Rais
mstaafu wa awamu ya pili nchini Tanzania,Alhaji Ally Hassan Mwinyi amesema kila mtu ana
haki ya kuchinja kutokana na imani yake ilimradi tu asivunje sheria za
nchi .
Alisema anashangaa watu kugombania kitu kidogo kama cha kuchinja ilihali Tanzania ni nchi yenye utamaduni wa kuwa na amani siku zote na kwamba kila mtu ana imani yake ya dini anayoiamini.
Hayo aliyasema jana katika hoteli ya Kilimanjaro wakati wa kongamano juu ya utamaduni wa kiislamu Afrika Mashariki ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo .
“Imani
ni nafsi ya mtu na haitakiwi mtu kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa
na mwenzio na kama unaona aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile
chinja yako kula hata ukitaka kula chura, mjusi konokono kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie katika jinai,”alisema Alhaji Mwinyi.
Pia
alisema majaribu kama hayo yaliwahi kumtokea wakati wa
utawala wake lakini alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia kila mtu ale
kile anachofikiri ni chakula bila kumlazimisha mwenzake ale anachokitaka
yeye.
Alisema
watanzania wamezaliwa ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni kuwa na
misingi ya kuvumiliana na kwamba sifa ya uislamu ni pamoja na kuwa na
uvumilivu si kufanya vurugu kama inayotafsiriwa na makundi ya wanaotaka
kuvunja amani ya nchi kwa kutumia jina la dini ya kiislamu.
Pia alimshukuru Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ulimwengu wa Kiislamu Duniani (RABITA) Dk.Abdullah Mohsin Al-Turki kwa kuichagua Tanzania katika kuhubiri amani pia.
Naye Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe ambaye alimwakilisha
Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal amesema utamaduni wa kiislamu wa Afrika
Mashariki na duniani kwa ujumla ni kuvumiliana katika dini huku akitolea
mfano wakati wa kumaliza kuswali ndio maana mtu anageuza shingo huku na
kule.
Pia
aliwataka waislamu kujiendeleza katika elimu huku akieleza kuwa hata
mtume alihamasisha hayo lakini waislamu wameshindwa kuyafuata.
Akitolea
mfano alisema waislamu wanachuo kimoja kikuu huku dhehebu moja la
Lutherani wanavyuo vikuu 11 hivyo ni vyema wakaungana na kujenga vyuo
kwa ajili ya kusaidia kuongeza wasomi kutoka katika taaluma mbalimbali.
“Suala
la elimu ya Dunia pia ni muhimu lakini mfano mzuri wa elimu kushuka ni
katika mikoa ya pwani ambapo ndio ilipoanzia mwaka 1995 wanafunzi
walioanza darasa la kwanza walikuwa 35,000 lakini walikuja kumaliza
darasa la saba 9000 hapa inaonesha kua waislamu tunarudi nyuma badala
kwenda mbele,”alisema Profesa Maghembe.
Hata
hivyo alisema kua suala la kuporomoka kwa elimu wakati mwingine wa
kulaumiwa ni wazazi kwa kushindwa kuwasimamia watoto wao katika maadili
ya taaluma na wazazi kushindwa kuwasimaia katika misingi ya dini zote.
Dk.Abdullah
Mohsin Al-Turki alisema katika nchi ya Saudia wanaishi watu tofauti
tofauti lakini wakiwa katika upendo huku akisisitiza kikubwa ni
kuheshimiana tu.
Alisema
RABITA imekuwa ikifanya kazi katika nchi mbalimbali za
Nigeria,Gabon,Jamhuri ya Kongo na baada ya ziara yake nchini hapa
atahitimisha kwa kuitembelea Sudan.
Kongamano
la RABITA limeandaliwa na Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu
Nchini ikiwa na lengo la kusisitiza amani nchini ambapo Alhaji Mwinyi
ndio mlezi wao.
Post a Comment