MTANGAZAJI

MALIPO YA MBUNGE WA TANZANIA SAWA NA YA MWALIMU KWA MIAKA MITATU

WAKATI wabunge wakiendelea kuongezewa posho za vikao, imebainika kuwa fedha anazolipwa mbunge mmoja kwa mwezi ni sawa na mishahara ya mwalimu wa shule ya msingi ya miaka mitatu.  Malipo hayo pia yanaonekana kuwa sawa na mshahara wa mwaka mmoja wa daktari msaidizi mwenye shahada moja, anayeanza kazi.

 Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi umebaini kuwa mbunge mmoja hulipwa Sh7.3 milioni kwa mwezi, ikiwa ni jumuisho la mshahara na malipo mengine ikiwamo posho za vikao.  Jumuisho hilo ni pamoja na posho mbalimbali kila mwezi kama vile za mafuta ya magari, ubunge, kukaa jimboni, kuendesha ofisi na simu.  Posho ya mafuta ni Sh2 milioni kwa mwezi ikikadiriwa kuwa atatumia lita 1,000 ambazo makisio ni Sh2,000 kwa lita moja.  Nyingine ni posho ya kukaa jimboni Sh800,000, posho ya ubunge Sh1 milioni, kuendesha ofisi Sh700,000, simu Sh500,000 na mshahara ni Sh2.3 milioni. 

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wakati mbunge akiwa hayupo bungeni inaelezwa bado analipwa posho hizo pamoja na mshahara na kumfanya ajikusanyie Sh7.3 milioni kila mwezi.  Wakati wa vikao bungeni, posho zao huongezeka ambazo uchunguzi unaonyesha mbunge hupewa posho  nyingine za aina tatu; za kikao, kujikimu na usafiri. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, posho hiyo ya usafiri hupewa bila kujali kuwa ana posho ya kila mwezi ya mafuta ya Sh2 milioni.  Viwango vya fedha kwa posho anazopewa mbunge anapokuwa Bungeni kila kikao kwa sasa imeongezeka kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 ya posho ya kujikimu Sh80,000 na usafiri Sh50,000.

Mwalimu Lakini, wakati wabunge wakifurahia neema hizo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, mshahara wa mwalimu wa shule ya msingi  anayeanza kazi, ambaye yupo kwenye daraja la mshahara la TGTS B ni Sh200,000 kwa mwezi.

Kwa mwalimu wa sekondari mwenye stashahada ambaye yupo kwenye daraja la TGTS C, mshahara wake ni Sh300,000  huku yule mwenye shahada wa daraja TGTS D analipwa Sh400,000, mishahara yote ikiwa ni ya kuanza kazi.

Mchanganuo huo unaonyesha kwamba, pia viwango hivyo vya mshahara vilivyoorodheshwa hapo, ni vile ambavyo havijakatwa kodi zozote zile.Kutokana na hali hiyo, mapato ya Mbunge kwa mwezi mmoja yanaweza kumlipa mwalimu mmoja  wa shule ya msingi mishahara ya miezi 36 sawa na miaka mitatu.


Mshahara huo pia utaweza kumlipa mwalimu mmoja wa sekondari mwenye stashahada  mshahara wa miezi 24, huku yule mwenye shahada akilipwa kwa muda wa miezi 18 kwa mapato ya mwezi mmoja ya mbunge. Fedha hizo zinaweza kumlipa mfanyakazi wa idara nyingine ya umma, ambaye mshahara wake upo kwenye daraja hilo kwa kipindi kama hicho.

 Daktari Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, mishahara ya madaktari wasaidizi ya kuanzia ni kati ya Sh480,000 na Sh600,000 ambayo ili ifikie malipo ya mbunge kwa mwezi, itabidi iwe kati ya mara 15 na 12.  Madaktari wasaidizi wenye shahada moja wanapoanza kazi, inaelezwa wanalipwa mshahara wa Sh800,000.

 Kauli ya Spika  Hata hivyo, Spika wa Bunge Anne Makinda, alisema posho ya vikao kwa wabunge iliongezwa kutokana na hali ngumu ya maisha mjini Dodoma.  Wabunge  Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema ongezeko hilo linatakiwa kusitishwa kwa kuwa mchakato wake umefanyika kinyume na taratibu na kwamba halina uhalali wala halijazingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi.

 Mnyika alifafanua kwamba kauli ya Spika Makinda kwamba nyongeza hiyo inatokana na kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo. Akamtaka Rais Jakaya Kikwete kutolea kauli kuhusu jambo hilo.  Alisema utetezi wa Spika Makinda kuhalalisha kupandishwa kwa posho hizo, hauna maana na kwamba kama sababu ingekuwa kupanda kwa gharama ya maisha, ingepandishwa posho ya kujikimu (subsistence allowance) ambayo imebaki pale pale Sh 80,000.

Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila, alisema suala la kupishana kauli kwa viongozi wawili wa taasisi moja, ni udhaifu mkubwa kwa taasisi hiyo. “Suala la posho inatakiwa litazamwe upya katika mihimili yote ya dola, panapokuwa hakuna kanuni ya kuweka uwiano miongoni mwa mihimili hii, kunasababisha manung’uniko na malalamiko kwa wananchi,” anasema Kafulila.

“Inatakiwa itazamwe upya,  hili suala la posho lipatiwe ufumbuzi kabisa, ukiangalia huko serikalini kuna mashirika ya umma ambayo wanalipa posho za Sh400,000 mpaka 500,000, mishahara wanalipa Sh10 mpaka 15 milioni,” alisema Kafulila  Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, alisema kitendo cha wabunge kuongezewa posho za vikao kwa asilimia 185.7, kinaibua  jazba kwa wananchi ambao wanahangaika kila kukicha kwa ugumu wa maisha.  “Kwenye jamii lazima kuwe na usawa, kama watu tupo kwenye hali mbaya (ugumu wa maisha) lazima wote tuenende sawa.

Wabunge kuongezewa posho kwa asilimia 185 siyo sawa kabisa, tunajiweka mbali na wananchi na wanatuona tunafaidika sana wakati wao wanateseka kwa ugumu wa maisha,” alisema Makamba.

Alisema kutokana na msimamo wake huo, Juni mwaka huu alikataa posho iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini baada ya kuhudhuria semina iliyoandaliwa na wizara hiyo. “Tulikaa  kwenye semina kwa saa mbili, tunamaliza naletewa karatasi nisaini posho ya Sh280,000 nilikataa. Nilikataa kwa sababu nilitambua kuwa ile ni kazi yangu kama mbunge, sasa unanilipa hela ya kazi gani?” Alihoji Makamba.

Shibuda adai posho muhimu Hata hivyo, Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda, alisema suala la wabunge kuongezewa posho halina ubaya wowote kwa kuwa litawafanya wasiwe ombaomba.

Shibuda ambaye katika mkutano wa Bunge la Bajeti alipingana na  sera ya chama chake iliyokuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 kuhusu posho za vikao, alisema ili mbunge atekeleze majukumu yake vizuri ni lazima alipwe fedha ya kutosha.
  “Umefikia wakati Waafrika tulinde fedheha kwa viongozi wetu ili wasiwe ombaomba. Viongozi wakilipwa vizuri wataweza kuitumikia nchi na jamii inayowazunguka, ipasavyo. Kutokulipwa vizuri ndio mwanzo wa viongozi kusaini mikataba mibovu,” alisema Shibuda.

 Chanzo:gazeti la Mwananchi

No comments

Mtazamo News . Powered by Blogger.